Watu 153 wameripotiwa kuuawa katika shambulio la shule, Jeshi la Israel lasema “halijui” kuhusu operesheni katika eneo hilo

Chanzo cha picha, Reuters
Afisa mmoja wa Iran amesema kuwa watu 153 wamefariki baada ya shule ya wasichana katika mji wa Minab kushambuliwa katika mashambulizi ya jana, kulingana na Mizan News Agency inayohusishwa na mahakama ya Iran.
Afisa mwingine wa Iran alikuwa amesema awali kuwa shule hiyo, iliyoko takribani mita 600 kutoka kituo cha Islamic Revolutionary Guard Corps, ilikuwa imelengwa kwa mashambulizi matatu ya makombora.
BBC imethibitisha video za tukio hilo, zikionesha moshi ukipaa kutoka kwenye jengo huku umati wa watu ukikusanyika karibu na eneo hilo na sauti za watu wakipiga mayowe kwa hofu zikisikika.
Hata hivyo, idadi ya waliokufa haijaweza kuthibitishwa kwa uhuru, kwani mara nyingi mashirika ya kimataifa ya habari hukataliwa kuingia Iran, jambo linalozuia kwa kiasi kikubwa uwezo wao wa kukusanya taarifa huko.
Msemaji wa Israel Defense Forces amesema “hafahamu” operesheni yoyote katika eneo hilo. Ameongeza kuwa pia ameona taarifa kutoka kwa maafisa wa Marekani wakisema wanachunguza tukio hilo.





















