Trump: lazima tufikie makubaliano na Iran ama tutaiangamiza
Rais wa Marekani Donald Trump amesema hahitaji msaada wa China katika juhudi za kumaliza vita dhidi ya Iran.
Akizungumza wakati akiondoka kuelekea ziara rasmi nchini China, Trump alisema atakuwa na mazungumzo ya kina na Rais Xi Jinping katika mkutano wao wa wiki hii.
Hata hivyo, Trump amesisitiza kuwa hahitaji msaada wa Xi Jinping katika kutatua mzozo ulioanza miezi miwili na nusu iliyopita kufuatia mashambulizi makubwa ya Marekani na Israel, ambayo baadaye yalizua mvutano mkali kuhusu udhibiti wa Mlango wa Hormuz.
“Tunazungumzia mambo mengi. Kwa kweli, siwezi kusema Iran ni mojawapo, kwa sababu tunaidhibiti Iran kikamilifu,” alisema Trump.
Kiongozi huyo wa Marekani aliongeza kuwa: “Ima tufikie makubaliano na Iran, au itaangamizwa kabisa.”
Kauli hiyo imejiri huku kukiwa na ripoti zinazoeleza kuwa China inaendelea kuisaidia Iran kupitia biashara ya mafuta na ushirikiano mwingine licha ya vikwazo vya kimataifa.
Trump, hata hivyo, alimpongeza Xi Jinping akisema kuwa “amekuwa akifanya kazi nzuri sana.”
China inaripotiwa kuwa mmoja wa washirika muhimu zaidi wa kiuchumi wa Iran, hasa kupitia ununuzi mkubwa wa mafuta ya nchi hiyo, huku Beijing ikionekana pia kuipa Tehran uungaji mkono wa kisiasa na kiuchumi.
Pia unaweza kusoma: