Biden amuunga mkono Kamala Harris kuwa mgombea urais wa Democratic

"Leo nataka kutoa usaidizi wangu kamili na uidhinishaji kwa Kamala kuwa mteule wa chama chetu mwaka huu'

Muhtasari

  • Kifundo cha nywele za mwanzilishi wa fani ya uuguzi chauzwa kwa pauni 3,500
  • Mahakama ya Bangladesh yafutilia mbali nafasi nyingi za kazi baada ya machafuko
  • Mwanasiasa wa upinzani Kenya, Raila Odinga awataka vijana kufanya mazungumzo na serikali
  • Donald Trump ameuambia mkutano kuwa 'alipigwa risasi kuitetea demokrasia'
  • Israel yawashambulia waasi wa Houthi nchini Yemen baada ya ndege isiyo na rubani kupiga Tel Aviv

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga & Yusuf Jumah ; Mhariri: Athuman Mtulya

  1. Mwanasiasa wa upinzani Kenya, Raila Odinga awataka vijana kufanya mazungumzo na serikali

      • Author, Laillah Mohammed
      • Nafasi, BBC Swahili
    Bw. Raila Odinga

    Chanzo cha picha, Reuters

    Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga amewataka vijana nchini humo kubuni kikundi kitakachoshiriki kwenye mazungumzo ya kitaifa katika kongamano ambalo ametaja litawaleta pamoja wadau mbalimbali ikiwemo serikali.

    Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii mapema Jumapili, bwana Odinga amesema kwamba kongamano hilo linatarajiwa kufanyika kaitka eneo ambalo halina uhusiano na upande wowote unaojadiliana.

    ''Ninapendekeza kwamba kongamano hilo liwahusishe watu kutoka sekta mbalimbali, kama vile serikalini, viongozi wa kidini, watu kutoka sekta ya afya, mawakili, waalimu na vijana. Ni sharti tuje pamoja kuzungumzia masuala ya kitaifa na yanayohusu katiba ambayo ni muhimu'', alisema Odinga.

    Kiongozi huyo ambaye ameshutumiwa na vijana hivi maajuzi kwa kutaka kushirikiana na Rais William Ruto, amesema kwamba masuala ya uongozi bora, gharama ya juu ya maisha, kumaliza ukabila, kukabiliana na ufisadi na kujadili kuhusu suala la deni la kitaifa ni makuu ambayo yanapaswa kuangaziwa katika kikao hicho.

    Kiongozi huyo wa chama cha upinzani cha ODM, hakuwa katika kikao cha wanahabarf siku ya Ijumaa Julai 19 ambapo viongozi wenzake katika muungano wa AZIMIO walitangaza kwamba hawatokubali kushirikishwa katika serikali ya amseto na chama tawala cha Kenya Kwanza kinachoongozwa na Rais Ruto.

    ''Yeyote atakaye kubali kuhudumu katika serikali ya Kenya Kwanza kutoka muungano wa Azimio, basi atafanya hivyo kama mtu binafsi'', Alisema Kalonzo Musyoka, katika kikao hicho cha Ijumaa kilichohudhuriwa na viongozi wengine katika muungano huo, Eugene Wamalwa na Jeremiah Kioni.

    Vijana wamesisitiza kwamba wataendelea na maaandamano Jumanne Julai 23, ambapo wamepanga kufunga maeneo muhimu ikiwemo uwanja wa ndege wa kimtaiafa wa Jommo Kenyatta kama njia moja ya kumshinikiza Rais Ruto kuyasikia malalamishi yao.

    Maandamano yameshuhudiwa nchini Kenya kwa wiki tano sasa, huku kilichowasha moto huu kikiwa mswada tata wa fedha 2024 ambao wengi walisema unaleta kodi nyingi ambazo wakenya hawawezi kamwe kumudu.

    Unaweza kusoma;

  2. Donald Trump ameuambia mkutano kuwa 'alipigwa risasi kuitetea demokrasia'

    Trump

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Donald Trump ameuambia mkutano wa kisiasa kwamba 'alipigwa risasi kuitetea demokrasia'wakati jaribio lilipofanywa dhidi yake juma lililopita.

    Ukiwa umehudhuriwa na maelfu ya watu, ulikuwa ni mkutano wa kwanza wa Trump na mgombea mwenza mpya JD Vance na wa kwanza tangu aliponusurika kwenye jaribio la mauaji.

    Aliambia uwanja uliojaa watu kwamba Wanademocrat wamemshutumu kuwa "tishio kwa demokrasia" , amesema yuko tayari "kuichukua tena Ikulu ya White House".

    Uchunguzi unaendelea kuhusu tukio hilo la kupigwa risasi mwishoni mwa juma lililopita, ambalo lilimwacha Trump na jeraha la sikio.

    Wengi wa waliohudhuria hafla hiyo, katika jimbo la Michigan waliiambia BBC kwamba jaribio la mauaji, ambalo liliua mshiriki mmoja na kuwajeruhi wengine wawili, halitawazuia kumuunga mkono mgombea huyo wa urais wa Republican.

    Wachunguzi bado hawajataja sababu za mtu huyo mwenye umri wa miaka 20 ambaye aliuawa na maafisa wa usalama.

    Tangu wakati huo, nchi imekuwa ikikabiliana zaidi na vitisho kwa wagombea wote wawili wa urais.

    Polisi huko Jupiter, Florida, Ijumaa walimkamata mwanaume mmoja kwa madai ya kutuma vitisho kwa Trump kwenye mitandao ya kijamii, huku mtu tofauti kutoka Florida alikamatwa siku chache mapema kwa madai ya kumtishia Rais Joe Biden.

    Unaweza kusoma;

  3. Israel yawashambulia waasi wa Houthi nchini Yemen baada ya ndege isiyo na rubani kupiga Tel Aviv

    Athari za mashambulizi

    Chanzo cha picha, AP

    Israel imefanya mashambulizi ya anga kwenye bandari ya Hodeidah inayodhibitiwa na Wahouthi nchini Yemen, siku moja baada ya ndege isiyo na rubani iliyorushwa na kundi hilo kupiga Tel Aviv.

    Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant alisema nchi yake inalenga kutuma ujumbe kwa vuguvugu la Houthi.

    "Moto unaowaka kwa sasa huko Hodeidah, unaonekana kote Mashariki ya Kati ," alisema.

    Vyombo vya habari vyenye uhusiano na Houthi vilisema watu watatu waliuawa na zaidi ya 80 kujeruhiwa katika mashambulizi ya Israel.

    Afisa wa Houthi Mohammed Abdulsalam aliripoti "uchokozi wa kikatili wa Israeli dhidi ya Yemen".

    Alisema mashambulizi hayo yanalenga kuwashinikiza Wahouthi kuacha kuwaunga mkono Wapalestina huko Gaza, jambo ambalo alisema halitafanyika.

    Ni mara ya kwanza kwa Israel kujibu moja kwa moja kile inachosema kuwa ni mamia ya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Yemen na makombora yaliyolenga ardhi yake katika miezi ya hivi karibuni.

    Picha kutoka Hodeidah zilionesha moto mkubwa ukiwaka Jumamosi jioni. Serikali inayoongozwa na Wahouthi mjini Sanaa ilisema Israel ilipiga vituo vya kuhifadhi mafuta karibu na ufuo, pamoja na mtambo wa kuzalisha umeme.

    Katika taarifa yake, Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilisema: "Baada ya miezi tisa ya mashambulizi ya mfululizo ya angani ya Houthis nchini Yemen kuelekea Israel, ndege za kivita za IAF [Jeshi la Wanaanga la Israel] zilifanya shambulizi kubwa umbali wa kilomita 1,800 [maili 1,118) dhidi ya maeneo ya kijeshi ya kigaidi ya Houthi" katika eneo la bandari ya Hodeidah.

    Unaweza kusoma;

  4. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu