Mwanasiasa wa upinzani Kenya, Raila Odinga awataka vijana kufanya mazungumzo na serikali
- Author, Laillah Mohammed
- Nafasi, BBC Swahili
Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga amewataka vijana nchini humo kubuni kikundi kitakachoshiriki kwenye mazungumzo ya kitaifa katika kongamano ambalo ametaja litawaleta pamoja wadau mbalimbali ikiwemo serikali.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii mapema Jumapili, bwana Odinga amesema kwamba kongamano hilo linatarajiwa kufanyika kaitka eneo ambalo halina uhusiano na upande wowote unaojadiliana.
''Ninapendekeza kwamba kongamano hilo liwahusishe watu kutoka sekta mbalimbali, kama vile serikalini, viongozi wa kidini, watu kutoka sekta ya afya, mawakili, waalimu na vijana. Ni sharti tuje pamoja kuzungumzia masuala ya kitaifa na yanayohusu katiba ambayo ni muhimu'', alisema Odinga.
Kiongozi huyo ambaye ameshutumiwa na vijana hivi maajuzi kwa kutaka kushirikiana na Rais William Ruto, amesema kwamba masuala ya uongozi bora, gharama ya juu ya maisha, kumaliza ukabila, kukabiliana na ufisadi na kujadili kuhusu suala la deni la kitaifa ni makuu ambayo yanapaswa kuangaziwa katika kikao hicho.
Kiongozi huyo wa chama cha upinzani cha ODM, hakuwa katika kikao cha wanahabarf siku ya Ijumaa Julai 19 ambapo viongozi wenzake katika muungano wa AZIMIO walitangaza kwamba hawatokubali kushirikishwa katika serikali ya amseto na chama tawala cha Kenya Kwanza kinachoongozwa na Rais Ruto.
''Yeyote atakaye kubali kuhudumu katika serikali ya Kenya Kwanza kutoka muungano wa Azimio, basi atafanya hivyo kama mtu binafsi'', Alisema Kalonzo Musyoka, katika kikao hicho cha Ijumaa kilichohudhuriwa na viongozi wengine katika muungano huo, Eugene Wamalwa na Jeremiah Kioni.
Vijana wamesisitiza kwamba wataendelea na maaandamano Jumanne Julai 23, ambapo wamepanga kufunga maeneo muhimu ikiwemo uwanja wa ndege wa kimtaiafa wa Jommo Kenyatta kama njia moja ya kumshinikiza Rais Ruto kuyasikia malalamishi yao.
Maandamano yameshuhudiwa nchini Kenya kwa wiki tano sasa, huku kilichowasha moto huu kikiwa mswada tata wa fedha 2024 ambao wengi walisema unaleta kodi nyingi ambazo wakenya hawawezi kamwe kumudu.
Unaweza kusoma;