Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa mazungumzo ya kumaliza vita kati ya Marekani na Iran yanaendelea kwa sasa, akisisitiza kuwa utawala wake unazungumza na “watu sahihi” ndani ya Iran.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ikulu ya White House, Trump alisema Iran inaonesha utayari mkubwa wa kufikia makubaliano, akidai kuwa wanataka “kufanya makubaliano kwa nguvu zote”.
Aliongeza kuwa maafisa wakuu wa utawala wake, akiwemo Makamu wa Rais JD Vance na Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio, wanahusika moja kwa moja katika mazungumzo hayo, ingawa hakutoa maelezo ya kina kuhusu hatua iliyofikiwa.
Hata hivyo, kauli za Trump zinakuja siku moja baada ya maafisa wa Iran kukanusha kuwepo kwa mawasiliano yoyote na Marekani, wakizitaja taarifa za mazungumzo kama “za uongo”.
Wakati huo huo, mashambulizi kati ya Israel na Iran yanaendelea, huku jeshi la Israel likitoa onyo kwa wakazi wa kusini mwa Lebanon kuondoka katika maeneo yao kutokana na hatari ya mashambulizi zaidi.
Aidha, wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon, inatarajiwa kupeleka wanajeshi kutoka kikosi cha 82nd Airborne kwenda Mashariki ya Kati, kwa mujibu wa taarifa ya CBS News.