Takriban watu 16 wamefariki dunia baada ya moto mkubwa kuzuka katika kiwanda cha nguo nchini Bangladesh, huku maafisa wakionya kuwa huenda idadi hiyo ikaongezeka.
Miili kumi na sita imepatikana lakini ilichomeka kiasi cha kutotambulika, shirika la zima moto limesema.
Jamaa waliofadhaika walikusanyika nje ya kiwanda cha ghorofa nne katika eneo la Mirpur huko Dhaka siku ya Jumanne kuwatafuta wapendwa wao ambao bado hawajapatikana.
Moto huo uliozuka katika kiwanda hicho mwendo wa saa sita mchana, ulizimwa baada ya saa tatu. Lakini ghala la kemikali lililo karibu liliendelea kuwaka, serikali imesema.
Mkurugenzi wa huduma ya zima moto Mohammad Tajul Islam Chowdhury aliviambia vyombo vya habari vya ndani kuwa waathiriwa walikufa "papo hapo" baada ya kuvuta "gesi yenye sumu kali."
Polisi na maafisa wa kijeshi bado wanajaribu kuwatafuta wamiliki wa kiwanda na ghala hilo, Bw Chowdhury aliwaambia wanahabari.
Uchunguzi kuhusu iwapo ghala hilo lilikuwa likifanya kazi kihalali pia unaendelea, aliongeza.
Wanafamilia waliokuwa na machozi walisimama nje ya majengo yaliyokuwa yameungua, wengi wao wakiwa wameshikilia picha za jamaa zao waliopotea.
Miongoni mwao ni mwanaume anayemtafuta binti yake, Farzana Akhter.
"Niliposikia kuhusu moto, nilikuja mbio. Lakini bado sijampata....namtaka binti yangu," aliliambia shirika la habari la Reuters.
Mwaka 2021, moto katika kiwanda cha chakula na vinywaji uliwaacha watu wasiopungua 52 wakiwa wamekufa na wengine 20 kujeruhiwa. Kiwanda hicho kilijengwa kinyume cha sheria na hakikuwa na mlango wa dharura, uchunguzi ulieleza.
Ajali mbaya zaidi ya viwanda nchini humo hadi sasa ilitokea mwaka 2013, wakati jengo la biashara la ghorofa nane liliporomoka na kuua zaidi ya watu 1,100.