Waziri wa Israeli ashutumiwa kwa wito wa maombi ya Wayahudi katika eneo takatifu la Jerusalem
Waziri wa siasa kali za mrengo wa kulia wa Israel amewaongoza mamia ya Waisraeli wa Kiyahudi kwenye eneo takatifu linalozozaniwa mjini Jerusalem, huku wengi wakienda kinyume na marufuku ya muda mrefu ya serikali ya Israeli ya kuomba sala za Kiyahudi eneo hilo.
Ziara ya Waziri wa Usalama wa Kitaifa Itamar Ben-Gvir katika eneo la Msikiti wa al-Aqsa, unaojulikana kwa Wayahudi kama Mlima wa Hekalu, kumeshutumiwa kuwa kitendo cha uchochezi na viongozi wa Palestina, Marekani, Ufaransa, Umoja wa Mataifa na mataifa kadhaa ya Kiarabu.
Bw Ben-Gvir alisema kwenye video kwamba "sera yetu ni kuwezesha maombi ya Wayahudi".
Lakini afisi ya waziri mkuu wa Israeli ilisisitiza kwamba hakuna mabadiliko katika makubaliano ya hali ya sasa ambayo inaruhusu Waislamu pekee kufanya sala zao katika eneo hilo.
Mahali hapa ni patakatifu zaidi kwa Wayahudi kwa sababu palikuwa na mahekalu mawili yaliyopo kwenye Biblia. Ni sehemu ya tatu takatifu kwa Waislamu, wanaoamini kuwa ni mahali ambapo Mtume Muhammad alipaa hadi mbinguni.
Ikiwa liko katika Jerusalem Mashariki, eneo hilo lilitwaliwa kimabavu na Israeli kutoka Jordan katika vita vya Mashariki ya Kati vya 1967.
Chini ya hali ilivyo kwa sasa, Jordan iliruhusiwa kuendelea na jukumu lake la kihistoria kama mlinzi wa eneo hilo, huku Israeli ikichukua udhibiti wa usalama na ufikiaji wake.
Wapalestina wanaishutumu Israeli kwa kuchukua hatua za kuhujumu mipango hiyo na kulalamika kwamba katika miaka ya hivi karibuni Wayahudi mara nyingi wameonekana wakisali bila kuzuiwa na polisi wa Israeli.
Video zilizoshirikishwa kwenye mitandao ya kijamii siku ya Jumanne, zilionyesha makundi ya Waisraeli wa Kiyahudi wakiimba wimbo wa taifa wa Israeli, wengine wakiwa wamebeba bendera za Israeli na kadhaa wakiwa wanafanya sala kwenye ukingo mwa eneo takatifu.
Akitembelea eneo hilo akiwa anasindikizwa na polisi wa Israeli, Itamar Ben Gvir, alisema "hatua kubwa" imepigwa na serikali ya Israeli katika "utawala na uhuru" kwenye eneo hilo. "Sera yetu ni kuwezesha maombi ya Wayahudi," aliongeza.
Pia alitangaza kwamba Israeli "lazima ishinde vita" katika Ukanda wa Gaza, na haipaswi kuhusika katika mazungumzo ya kusitisha mapigano na kuachiliwa huru kwa mateka ili "kuisambaratisha Hamas".
Hata hivyo, baadaye, ofisi ya Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu ilisema tukio hilo "limeenda kinyume na hali ilivyo."
“Sera ya Israeli kuhusu Mlima wa Hekalu haijabadilika; hivi ndivyo imekuwa na hivi ndivyo itakavyokuwa,” ilisisitiza.
Pia unaweza kusoma: