Macharia Gaitho: Mwandishi maarufu Kenya asimulia utekaji nyara wake baada ya kuachiliwa
Polisi nchini Kenya wamemwachilia mwanahabari mkongwe baada ya "kumkamata kimakosa" katika kituo cha polisi na kumsukuma kwa kasi ndani ya gari binafsi.
Muhtasari
Aisha Masaka: Mtanzania wa kwanza kusajiliwa na timu ya ligi kuu ya wanawake ya England
Aliyekwama kwenye lifti kwa saa 42 nchini India alidhani angekufa
Mawakili wa Guinea walalamikia ukandamizaji wa jeshi
Macharia Gaitho: Mwandishi maarufu Kenya asimulia utekaji nyara wake baada ya kuachiliwa
UN, Mashirika ya kimataifa yasiitupe Sudan:MSF
Wafanyakazi watafutwa baada ya lori la mafuta kuzama pwani ya Oman waendelea
Fernandez kuadhibiwa kwa madai ya kutumia wimbo wenye kauli za kibaguzi
Wanafunzi walazwa hospitalini kwa kula vibanzi vyenye 'pilipili nyingi'
Sita waliofariki walikunywa chai yenye sumu ya sianidi
Israeli na Hezbollah wanakaribia kujiingiza katika vita
Shirika la Ford lakanusha kufadhili maandamano nchini Kenya
Guo:Tajiri wa China apatikana na hatia kwa kashfa ya zaidi ya $1bn Marekani
Mtu mmoja auawa katika maandamano ya kumtaka rais wa Kenya kuondoka madarakani
Usalama wa Trump uliimarishwa wiki kadhaa zilizopita kutokana na njama ya Iran ya kumuua
Moja kwa moja
Asha Juma
Aisha Masaka: Mtanzania wa kwanza kusajiliwa na timu ya ligi kuu ya wanawake ya England
Chanzo cha picha, Aisha Masaka Instagram
Mwanasoka Aisha Masaka ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza
mwanamke kutoka Tanzania kusajiliwa na timu ya ligi kuu ya wanawake ya England.
Aisha amesaini kandarasi na klabu ya Brighton akitokea BK
Hacken ya kutoka Sweden aliyojiunga nayo mnamo mwaka 2022 akitokea kwenye klabu
ya Yanga Princess inayoshiriki ligi kuu ya wanawake nchini Tanzania
Mwaka mmoja uliopita Aisha aliweka rekodi ya aina yake kuwa mchezaji wa kwanza mwanamke kutoka Tanzania kucheza michuano ya klabu bigwa
ulaya kwa wanawake wakati timu yake ya BK Hacken iliposhiriki michuano hiyo.
Masaka licha ya kuwa mchezaji wa kwanza mwanamke kusaiji mkataba
kwenye klabu hiyo anaungana na nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania Mbwana
Samatta ambaye aliwahi kupita kwenye klabu ya Aston Villa mnamo mwaka 2019.
Aliyekwama kwenye lifti kwa saa 42 nchini India alidhani angekufa
Chanzo cha picha, Courtesy: Ravindran Nair
Mwanaume mmoja kutoka jimbo la Kerala kusini mwa India, ambaye
alinasa kwenye lifti ya hospitali kwa saa 42 bila chakula wala maji, ameiambia
BBC kuwa alihofia angefia humo.
Ravindran Nair, 59, aliingia kwenye lifti ili kwenda kukutana na
daktari Jumamosi mchana, kisha alikwama ndani hadi Jumatatu asubuhi, wakati
msimamizi wa lifti alipomkuta.
Sasa yuko hospitali na anatibiwa upungufu wa maji mwilini na
maumivu ya mgongo.
Watu wa familia yake hapo awali walidhani alikuwa kazini, lakini
baadaye waliwasiliana na polisi na kuanza kumtafuta.
Tukio hilo limegonga vichwa vya habari, na kusababisha serikali
ya jimbo hilo kuwasimamisha kazi mafundi watatu na kuanzisha uchunguzi.
Maafisa kutoka Chuo cha Serikali cha Matibabu,
Thiruvananthapuram, na waziri wa afya wa jimbo hilo wamemwomba Bw Nair
msamaha.
Bw Nair aliiambia BBC kwamba aliponasa, alijaribu kupiga nambari
ya dharura iliyowekwa kwenye lifti lakini hakujibiwa. Pia alijaribu kumpigia
simu mke wake Sreelekha CP, ambaye anafanya kazi hospitalini, na "mtu
mwingine yeyote ambaye aliweza kumfikiria", lakini simu
hazikuunganishwa.
"Nilianza kuogopa na kuanza kugonga milango ya lifti ili
kuwashtua watu. Hapo ndipo simu yangu ilipoanguka sakafuni na kuacha kufanya
kazi," asema.
"Nilipiga kelele na kupiga mayowe kuomba msaada na
nilijaribu kung'oa milango kwa mikono yangu. Sasa kulikuwa na giza ndani ya
lifti, lakini cha kushukuru, kulikuwa na hewa ya kutosha ya
kupumua."
Kisha akazunguka kwenye lifti, akibonyeza kengele ya hatari tena
na tena, akitumaini kwamba ingelia, lakini bila mafanikio yoyote.
“Saa zilizidi
kwenda sikujua ni mchana au usiku kwani ndani kulikuwa na giza totoro,
nilipochoka nililala pembeni, ikabidi nitumie kona nyingine kujisaidia haja
ndogo,” anasema.
Mawakili wa Guinea walalamikia ukandamizaji wa jeshi
Chanzo cha picha, AFP
Mawakili nchini Guinea wamegoma wakilalamikia ukandamizaji wa upinzani unaofanywa na utawala wa kijeshi.
Siku ya Jumanne, chama cha wanasheria nchini kilishutumu kile kilichoeleza kama "kukamatwa kiholela" na kuwekwa kizuizini kwa siri kwa raia.
Mawakili watasusia vikao vya mahakama hadi tarehe 31 Julai, ilisema.
Shughuli za mahakama zinasemekana "kulemezwa" na mgomo huo, ambao unaweza kuvuruga kesi ya kihistoria kuhusu mauaji ya mwaka 2009 ambayo yanachukuliwa kuwa moja ya nyakati mbaya zaidi katika historia ya taifa hilo la Afrika Magharibi.
Mahakama inatazamiwa kutoa uamuzi wake kwa mtawala wa zamani wa kijeshi wa nchi hiyo, Moussa Dadis Camara, kuhusu uhalifu dhidi ya binadamu kuhusiana na mauaji ya mwaka 2009 ya zaidi ya watu 150 katika uwanja wa michezo tarehe 31 Julai.
Mamlaka imesisitiza kusikilizwa kwa kesi hiyo, lakini haijafahamika iwapo hukumu itasomwa tarehe hiyo kwa sababu ya mgomo huo.
Mgomo huo umekuja baada ya kukamatwa tarehe 9 Julai kwa Oumar Sylla na Mamadou Bah, viongozi wa vuguvugu la wananchi ambalo limekuwa likiikosoa serikali inayoongozwa na jeshi na kutaka kurejeshwa kwa utawala wa kiraia.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeitaka serikali "mara moja" kuwaachilia huru.
Macharia Gaitho: Mwandishi maarufu Kenya asimulia utekaji nyara wake baada ya kuachiliwa
Chanzo cha picha, X
Maelezo ya picha, Mwandishi wa muda mrefu nchini Kenya Macharia Gaitho
Polisi nchini Kenya wamemwachilia mwanahabari mkongwe baada ya "kumkamata kimakosa" katika kituo cha polisi na kumsukuma kwa kasi ndani ya gari binafsi.
Macharia Gaitho alisema alifuatwa karibu na nyumba yake katika mji mkuu, Nairobi, na watu waliokuwa kwenye magari mawili, ambao walikataa kujitambulisha.
Alikuwa na mwanawe, ambaye alikwenda naye hadi kituo cha polisi kilicho karibu kwa usalama wake, ambapo alisukumwa kwa nguvu ndani ya gari na kukimbizwa.
Polisi baadaye walisema ni kisa cha "utambulisho wa makosa" na kwamba wamekuwa wakimsaka mtu mwingine ambaye wanamtuhumu kwa kudharau uchunguzi wa polisi kuhusu mshukiwa wa mauaji ya mfululizo.
"Polisi wangependa kufafanua kwa umma kwamba asubuhi ya leo, tulimkamata mwanahabari Macharia Gaitho katika kesi ya utambulisho kimakosa, iliyokusudiwa kumkamata Francis Gaitho ambaye ni mtu tuliyekuwa tukimchunguza," walisema katika taarifa.
Wawili hao hawana uhusiano.
Video iliyosambazwa sana kwenye mitandao ya kijamii inaonesha mwanahabari huyo akilazimishwa kuingia kwenye gari jeupe na maafisa waliovalia sare na wengine waliovalia kiraia.
Tukio hilo liliibua hasira kutoka kwa Wakenya mtandaoni, baada ya wimbi la shutuma kwamba maafisa wa usalama walikuwa wamewateka nyara watu walioonekana kuhusishwa na maandamano ya hivi karibuni dhidi ya serikali.
Bw Gaitho aliwaambia wanahabari kuwa ndani ya gari hilo, "alikuwa katikati ya wanaume wawili waliovalia kiraia".
"Nilifungwa pingu na kushambuliwa," alisema.
Alisema watu hao walitaka kufahamu kwa nini anakataa kukamatwa.
UN, Mashirika ya kimataifa yasiitupe Sudan:MSF
Maelezo kuhusu taarifa
Author, Caro Robi
Nafasi, BBC Swahili
Chanzo cha picha, Getty Images
Mkuu wa shirika la Kimataifa la madaktari
wasio na mipaka MSF amesema mashirika ya Umoja wa Mataifa na mashirika mengine
ya kimataifa ya kutoa misaada ya kibinadamu yanapaswa kurudi na kuwasaidia watu
wa Sudan.
Vita vililivyozuka mwezi Aprili mwaka jana nchini Sudan vimsababisha
mzozo unaotajwa na Umoja wa Mataifa kuwa mbaya zaidi duniani na taifa hilo
limetumbukia katika msukosuko mkubwa.
Mkuu wa MSF Christos Christou amesema
baada ya miezi kumi na tano ya vita vikali Sudan,takriban mtu mmoja kati ya
watatu waliojeruhiwa nchini humo ni mwanamke au mtoto wa chini ya umri wa miaka
kumi na kuongeza kuwa mashirika mengi yameuamua kuchukua msimamo wa kusubiri na
kuona jinsi mzozo huo utakavyokwenda.
Bwana Christou amesema MSF inazungumza na
pande zote mbili zinazozona kujaribu kupata ridhaa ya kupitishwa kwa misaada ya
kiutu kwa mamilioni ya wasudan wanaohitaji kwa dharura chakula,maji na makazi.
MSF inasisitiza mzozo wa kibinadamu
unaoikumba Sudan kuwa mkubwa zaidi duniani na kusema kuwa licha ya hali kuwa
ngumu na inayohusisha changamoto lukuki,hatua zaidi zinahitaji kuchukuliwa
kulisaidia taifa hilo na watu wake.
Wito huo unakuja huku wajumbe wa
pande zinazozozana Sudan wakifanya mazungumzo na mjumbe wa Umoja wa Mataifa
mjini Geneva tangu wiki iliyopita.
Sudan kwa sasa inakabiliwa na ukame
mkali,wengi nchini humo ambao wameachwa bila ya makazi wakiripoti kuwa hawana
uwezo wa kujikimu kimaisha kwani wameishiwa fedha,chakula na njia karibu zote
za kujipatia riziki.
Mashirika mengi ya kutoa misaada yamesitisha
shughuli zao kwa kuhofia usalama wa wafanyakazi wake,kushambuliwa kwa vituo
vyao,kuporwa kwa misaada,kunyimwa ruhusa ya kufikia maeneo yanayohitaji misaada
na kutopata ufadhili wa kutosha kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.
Umoja wa Mataifa umezishutumu pande zote
mbili zinazopigana,jeshi la Sudan na kikosi maalumu cha wanamgambo RSF kwa
kuzuia kimakusudi misaada kufikishwa kwa waathiriwa,miongoni mwa visa vingine
chungunzima vya ukiukaji wa haki za binadamu.
Kwa mfano katika mji wa El Fasher,vituo vya
MSF vimeshambuliwa mara tisa tangu tarehe kumi mwezi Mei na karibu kila kona ya
Sudan,wahudumu wa afya wanatishwa,wagonjwa wanauawa na vituo vya afya
vinalipuliwa kwa mabomu. Inaripotiwa zaidi ya asilimia sabini ya vituo vya afya
nchini humo havifanyi kazi.
Mzozo
wa Sudan umesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kuwaacha takribani watu
milioni kumi na moja bila ya makazi.
Zaidi ya nusu ya idadi, jumla ya wasudani milioni 48 hawana chakula cha kutosha na hali inabashiriwa kuwa itazidi
kuzorota.
Wafanyakazi watafutwa baada ya lori la mafuta kuzama pwani ya Oman waendelea
Chanzo cha picha, Getty Images
Operesheni ya kuwatafuta wafanyakazi 16 waliotoweka, 13 kati yao wakiwa Wahindi, baada ya meli ya mafuta kupinduka katika pwani ya Oman inaendelea.
Afisa mmoja wa India aliiambia BBC kwamba wizara ya mambo ya nje ilikuwa ikiratibu operesheni hiyo na mamlaka ya masuala ya bahari ya Oman.
Maafisa wa Oman walisema Jumatatu kwamba meli ya mafuta, Prestige Falcon, ilikuwa imepinduka maili 25 kusini mashariki mwa rasi yake ya Madrakah.
Wafanyakazi watatu kati ya 16 waliotoweka ni raia wa Sri Lanka.
Meli hiyo iliyokuwa na bendera ya Comoro ilikuwa ikielekea katika bandari ya Aden nchini Yemen ilipopinduka.
Maafisa kutoka Kituo cha Usalama cha Baharini cha Oman waliliambia shirika la habari la Reuters Jumanne kwamba meli hiyo ilisalia "imezama, ikiwa imepinduka"
Wizara ya ulinzi ya Oman, ambayo inasimamia kituo hicho, haikujibu maswali ya BBC kuhusu iwapo yaliyomo ndani ya meli hiyo ya mafuta yalikuwa yamemwagika baharini.
Meli hiyo yenye urefu wa 117.4m iliundwa mwaka wa 2007, kulingana na marinetraffic.com.
Idadi kubwa ya wafanyakazi wa Kihindi wa baharini ulimwenguni mara nyingi huwa waathiriwa wa ajali au uharamia.
Wafanyakazi 17 wa India wa MSC Aries, meli ya kibiashara yenye uhusiano na Israel, walikwama wakati wanajeshi wa Iran walipoikamata meli hiyo mnamo Aprili.
Waliachiliwa baada ya mazungumzo kati ya India na Iran.
Mnamo mwaka wa 2022, wafanyakazi 16 wa meli ya India walizuiliwa chini ya ulinzi wa jeshi la wanamaji la Guinea ya Ikweta kwa miezi tisa.
Fernandez kuadhibiwa kwa madai ya kutumia wimbo wenye kauli za kibaguzi
Chanzo cha picha, Getty Images
Chelsea
wameanza kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya kiungo Enzo Fernandez baada ya kuweka
video kwenye mtandao wa kijamii ambayo Shirikisho la Soka la Ufaransa lilisema ilijumuisha
wimbo unaodaiwa kuwa wa "kibaguzi".
Siku ya
Jumanne FFF ilisema itawasilisha malalamiko kwa shirikisho la soka duniani Fifa,
juu ya video hiyo iliyo na wimbo ulioimbwa na baadhi ya kikosi cha Argentina
kuhusu wachezaji wa Ufaransa.
Mchezaji
mwenzake wa Chelsea Fernandez Wesley Fofana, alichapisha picha ya video hiyo
kwenye mtandao wa Instagram, akiielezea kama "ubaguzi wa rangi usiovumilika".
Fernandez
alisema "anasikitika sana" kwa video aliyochapishwa mtandaoni wakati
Argentina ikisherehekea kushinda Copa America.
"Wimbo huo una maneno ya kukera sana na hakuna sababu
kabisa ya maneno haya," alisema.
"Ninapinga ubaguzi wa aina zote na ninaomba radhi kwa
kutekwa na shangwe za sherehe zetu za Copa America.
"Video hiyo, nyakati hizo, maneno hayo, hayaakisi
imani yangu au tabia yangu."
Taarifa ya
Chelsea ilisema: "Tunatambua na kuthamini msamaha wa mchezaji wetu na
tutatumia hii kama fursa ya kuelimisha.
"Klabu
imeanzisha utaratibu wa ndani wa kumpa nidhamu."
FFF
itawasiliana na Chama cha Soka cha Argentina (AFA) kuhusu video ya moja kwa
moja iliyotumwa kwenye mitandao ya kijamii na Fernandez baada ya Argentina
kuifunga Colombia 1-0 kwenye fainali ya Copa America Jumapili.
Wanafunzi walazwa hospitalini kwa kula vibanzi vyenye 'pilipili nyingi'
Chanzo cha picha, Isoyama Corp
Wanafunzi
kumi na wanne wa shule ya upili huko Tokyo walikimbizwa hospitalini baada ya
kula vibanzi "vyenye pilipili nyingi", polisi walisema.
Takriban
wanafunzi 30 walikula vibanzi hivyo baada ya mmoja wao kuja nazo shuleni,
vyombo vya habari vya nchini humo viliripoti.
Muda si
muda, baadhi yao walianza kulalamika kuwa na kichefuchefu na maumivu makali
mdomoni, na kusababisha idara ya zimamoto na polisi kupigiwa simu.
Wasicha 13 na mvulana mmoja ambao walipelekwa hospitali
walikuwa wamepoteza fahamu.
Kampuni inayotengeneza kitafunio hicho,
Isoyama Corp, alitoa taarifa akiomba radhi kwa "tatizo lolote" kwa
wateja, na kuwatakia wanafunzi afueni ya haraka.
Shule na kampuni bado hazijasema lolote tangu BBC
ilipowasiliana nazo.
Tovuti ya kampuni hiyo inaonya yeyote ambaye angependa kula
vibanzi hivyo.
Pia, " inakataza wale walio na umri chini ya miaka
18 kutokula vibanzi hivyo ambavyo vina pilipili sana – na wale ambao wanapenda
kula vyakula vya pilipili "kula kwa tahadhari". Vibanzi hivyo vina pilipili kiasi
kwamba vinaweza kusababisha maumivu", ilisema.
Pia, kampuni
hiyo inashauri watu kutokula vibanzi hivyo "wakiwa peke yao" na kuongeza
kuwa zinaweza kusababisha kuhara zikiliwa "kwa wingi".
Sita waliofariki walikunywa chai yenye sumu ya sianidi
Chanzo cha picha, Royal Thai Police
Watu sita waliofariki dunia katika hoteli ya kifahari
nchini Thailand walitiliwa sumu ya sianidi kwenye chai, polisi wamesema.
Polisi wanashuku mmoja kati ya waliofariki ndiye aliyetekeleza
kitendo hicho kutokana na deni kubwa alilokuwa anadaiwa.
Watu hao walipatikana wamefariki dunia na wafanyakazi wa
hoteli ya kifahari ya Hyatt Erawan katika mji mkuu wa Bangkok, Jumanne.
Wachunguzi wanaamini hadi wakati wanapatikana, walikuwa wameshafariki
saa 24 zilizopita.
Wawili kati ya sita walikuwa wamekopeshwa "mamilioni"
ya pesa ikiwa ni takriban $280,000 (£215,000) na mmoja wa waliofariki kwa ajili
ya uwekezaji, mamlaka ilisema.
Awali kulikuwa na hali ya mkanganyiko na sintofahamu baada
ya ugunduzi wa kutisha wa miili hiyo, huku ripoti za ndani zikiashiria kwamba kulikuwa na ufyatuaji risasi. Polisi
baadaye walitupilia mbali taarifa hizi.
Katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumatano,
Naibu mkuu wa polisi wa Bangkok Jenerali Noppassin Poonsawat alisema kundi hilo
lilikuwa limeingia katika hoteli hiyo kila mmoja kivyake na walipewa vyumba vitano - vinne kwenye ghorofa
ya saba, na kimoja kwenye ghorofa ya tano.
Siku ya Jumatatu, walikwenda kwenye chumba cha ghorofa ya
tano.
Wawili kati ya waathiriwa, Sherine Chong, 56, na Dang
Hung Van, 55, ni raia wa Marekani.
Wengine wanne walikuwa raia wa Vietnam Thi Nguyen Phuong,
46, mumewe Hong Pham Thanh, 49, Thi Nguyen Phuong Lan, 47, na Dinh Tran Phu,
37.
Israeli na Hezbollah wanakaribia kujiingiza katika vita
Chanzo cha picha, BBC / Goktay Koraltan
Wakati vita huko Gaza
vikiendelea, kuna hofu inayoongezeka huenda vikazuka vita vingine vya Mashariki
ya Kati - na matokeo mabaya kwa eneo hilo, na kwingineko.
Israel na kundi la Lebanon Hezbollah (linaloungwa mkono
na Iran) wamekuwa wakifyatuliana risasi na makombora katika mpaka wao wa pamoja kwa muda wa miezi
tisa iliyopita.
Iwapo mzozo huu utazidi kuwa vita vya pande zote, unaweza
kupunguza uharibifu ambao umeonekana Gaza, kuwaingiza vitani wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran nchini
Iraq, na Yemen, kueneza mzozo Mashariki
ya Kati na kuihusisha Marekani. Iran yenyewe inaweza kuingilia moja kwa moja.
Umoja wa Mataifa umeonya kuhusu "janga lisiloweza
kufirika".
Shirika la Ford lakanusha kufadhili maandamano nchini Kenya
Shirika la
Ford Foundation lenye makao yake nchini Marekani limekanusha madai ya Rais
William Ruto kwamba linafadhili maandamano ya kupinga serikali.
Katika
taarifa walioitoa kwenye mtandao wao, Ford Foundation imesema, "Ingawa
tunatambua haki ya Wakenya kutetea kwa amani nchi yenye haki na usawa,
tunakanusha vitendo au matamshi yoyote ambayo yana chuki au kuunga mkono
unyanyasaji dhidi ya taasisi yoyote, mtu binafsi au jamii yoyote. Hatukufadhili
maandamano ya hivi majuzi dhidi ya mswada wa fedha na tuna sera isiyopendelea
upande wowote kwa utoaji wetu wote wa ruzuku."
Haya yanajiri baada ya Rais William Ruto hususan kulitaja
shirika hilo na kulitaka kuambia Wakenya ukweli juu ya nani anayefadhili
maandamano ya Kenya ya kupinga serikali.
Bw. Ruto aliongeza kuwa wote wanaohusika watakabiliwa na
mkono wa sheria.
Shirika la Ford ni la kibinafsi lililoanzishwa mwaka 1963
na Edsel Ford, mtoto wa mwanzilishi wa Kampuni ya Ford Motor Henry Ford.
Shirika hilo linalenga kuendeleza haki na maadili ya
demokrasia na linaendesha shughuli zake duniani kote.
Guo:Tajiri wa China apatikana na hatia kwa kashfa ya zaidi ya $1bn Marekani
Chanzo cha picha, Getty Images
Mfanyabiashara wa China aliyekimbia nchi yake
na kwenda uhamishoni Guo Wengui amepatikana na hatia na mahakama ya
Marekani kwa kosa la kuwalaghai wafuasi wake mtandaoni katika kashfa ya mabilioni
ya dola.
Alipatikana
na hatia katika makosa tisa kati ya 12 aliyokabiliwa nayo, ikiwa ni pamoja na
ulaghai na utakatishaji fedha.
Hukumu ya
Guo itatolewa tarehe 19 Novemba, ambapo anaweza kufungwa kwa miongo kadhaa.
Amekuwa gerezani tangu kukamatwa kwake Machi 2023.
Yeye ni
mkosoaji wa chama cha Kikomunisti cha China na alikuwa mshirika wa Stephen
Bannon, mwanamkakati mkuu wa zamani wa Ikulu ya White House chini ya rais wa
zamani Donald Trump.
Guo ana majina mengi ikiwa ni pamoja na Miles Guo, Miles
Kwok na " Brother Seven". Alitajwa kama Ho Wan Kwok alipofunguliwa
mashtaka mwaka 2023.
Waendesha mashtaka walisema Guo alichangisha zaidi ya
$1bn (£770bn) kutoka kwa wafuasi wake mtandaoni, ambao walijiunga naye katika miradi
ya uwekezaji nasarafu za kidijitali (cryptocurrency) kati ya 2018 na 2023.
Pesa alizochangisha zilitumika kufadhili maisha yake ya ambayo
yalijumuisha jumba la futi za mraba 50,000, Lamborghini ya $1m na boti ya $37m,
walisema.
"Maelfu ya wafuasi wa Guo mtandaoni walidhulumiwa
ili Guo aweze kuishi maisha ya kifahari," Mwanasheria wa Marekani huko
Manhattan, Damian Williams, alisema baada ya hukumu hiyo.
Mtu mmoja auawa katika maandamano ya kumtaka rais wa Kenya kuondoka madarakani
Chanzo cha picha, BBC/Mercy Juma
Waandamanaji
wanaoipinga serikali nchini Kenya walirejea barabarani wakiongeza madai ya kumtaka
Rais William Ruto ajiuzulu licha ya mabadiliko yake ya hivi majuzi.
Mwanamume
mmoja ameuawa kwa kupigwa risasi wakati wa makabiliano kati ya waandamanaji na
vikosi vya usalama viungani mwa mji mkuu, mwandishi wa BBC katika eneo hilo
anasema.
Katikati ya
jiji la Nairobi, maduka yalisalia kufungwa huku polisi wakifyatua gesi ya kutoa
machozi kuwatawanya mamia ya waandamanaji.
Maandamano
hayo yalianza mwezi uliopita kupinga mswada wa ushuru ambao haukupendwa na watu
wengi, na kutoka wakati huo umeondolewa na rais.
Lakini yamekuwa
yakiendelea kutokana na hasira zaidi juu ya utawala mbaya, rushwa na
uwajibikaji wa polisi kutokana na vifo vya makumi ya waandamanaji katika maandamano
ya hivi karibuni.
Wiki
iliyopita, Rais Ruto alitoa wito wa "mazungumzo" huku akifuta
baraza lake lote la mawaziri na mkuu wa jeshi la polisi kujiuzulu.
Harakati za
maandamano hayo kwa kiasi kikubwa zinaratibiwa mtandaoni na vijana wa Kenya,
ambao wengi wao wamekataa mazungumzo na wanamtaka Bw Ruto "aondoke"
madarakani.
Umati wa
watu ulibeba mwili wa muandamanaji aliyeuawa Jumanne huko Kitengela, kusini mwa
Nairobi, hadi kituo cha polisi kilicho karibu. Jeshi la polisi halijazungumzia
kifo cha mtu huyo.
Waandamanaji
hao waliimba "Ruto lazima aende", waliwasha moto barabarani na
kurusha mawe walipokuwa wakipambana na polisi, mwandishi wa BBC katika eneo la
tukio anasema.
Ghasia pia zilishuhudiwa katika maeneo mengine ya
nchi, yakiwemo Mombasa, Kisumu, Nakuru na Nyeri.
Makumi ya watu wameuawa hadi sasa tangu kuanza kwa
maandamano hayo, huku shirika linalofadhiliwa na serikali likisema idadi ya
vifo vilivyotokea kutokana na maandamano hayo si chini ya watu 50 huku wengine
413 wakijeruhiwa.
Mapema Jumanne, kaimu mkuu wa polisi alisema kulikuwa na
"intelijensia ya kuaminika" kwamba "makundi fulani ya wahalifu
waliopangwa" yalikuwa yamepanga "kupenya, kuvuruga na kuhatarisha"
maandamano hayo.
Usalama wa Trump uliimarishwa wiki kadhaa zilizopita kutokana na njama ya Iran ya kumuua
Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Maafisa wa huduma za siri walimlinda Trump baada ya kupigwa risasi Jumamosi
Ulinzi kwa
Donald Trump uliimarishwa wiki kadhaa zilizopita baada ya mamlaka ya Marekani
kujua kuhusu njama ya Iran ya kumuua, kulingana na maafisa wa usalama wa taifa.
Maafisa
wanasema hakuna uhusiano unaojulikana kati ya madai ya njama ya Iran na jaribio
la kumuua rais huyo wa zamani siku ya Jumamosi huko Pennsylvania.
Hata hivyo,
ufichuzi kwamba usalama umeimarishwa unazua maswali zaidi kuhusu jinsi Thomas
Matthew Crooks, 20, alivyoweza kupanda jengo na kukaribia vya kutosha
kumfyatulia risasi Trump.
Idara ya
Huduma ya Siri ya Marekani na kampeni ya Trump ziliarifiwa kuhusu tishio la
Iran, na usalama ukaimarishwa kutokana na hilo, kulingana na afisa wa usalama
wa taifa wa Marekani.
Vyanzo vya
kijasusi viliiambia CBS, mshirika wa habari wa BBC wa Marekani, kwamba Huduma
ya Siri iliimarisha usalama mwezi Juni ili kukabiliana na tishio la Iran. Hii
ilijumuisha afisa wa ziada wa kukabiliana na mashambulizi na mpiga risasi kwa
kuvamia, ndege zisizo na rubani na mbwa wa roboti.
CBS iliripoti kwamba maelezo ya uwezekano wa operesheni
ya Iran yalipatikana kupitia "intelijensia ya chanzo cha binadamu",
na yalipatikana huku kukiwa na ongezeko kubwa la mazungumzo ya Iran kuhusu
mashambulizi dhidi ya Trump.
Trump na maafisa akiwemo waziri wake wa zamani wa mambo
ya nje, Mike Pompeo, wamekabiliwa na vitisho kutoka Tehran tangu kuamuru kuuawa
kupitia ndege isiyo na rubani kwa Qassim Soleimani, kamanda wa kikosi cha Quds
cha Iran, nchini Iraq mwaka 2020.
Ujumbe wa Iran katika Umoja wa Mataifa uliita ripoti hiyo
"isiyo na uthibitisho na yenye nia mbaya", na kuongeza kuwa Trump ni
"mhalifu ambaye lazima ashtakiwe na kuadhibiwa katika mahakama ya
sheria".
Anthony Guglielmi, msemaji wa Huduma ya Siri ya Marekani,
alisema shirika hilo na mengine "yamekuwa yakipokea taarifa mpya za
vitisho na kuchukua hatua kama inavyohitajika".
"Hatuwezi kutoa maoni juu ya vitisho vyovyote, zaidi
ya kusema kwamba Huduma ya Siri inachukukulia vitisho kwa uzito na kujibu
ipasavyo."
Kampeni ya Trump ilisema haitoi maoni yoyote juu ya
maswala ya usalama na ilielekeza maswali ya BBC kwa Huduma ya Siri.