Je, unapaswa kufanya nini ikiwa umekwama kwenye lifti iliyokatika umeme?

Tukio kutoka kwa filamu "Between Heaven and Earth" kuhusu kundi lililokwama kwenye lifti

Chanzo cha picha, CINEMA.COM

Iliyochapishwa

Zaidi ya miaka 60 iliyopita, mwandishi mashuhuri wa Kimisri Naguib Mahfouz aliwaza jinsi kikundi cha watu kilivyokwama ndani ya lifti ya jengo, katika hadithi ambayo iligeuka kuwa sinema maarufu "Between Heaven and Earth."

Ingawa wazo lenyewe lilikuwa la kifalsafa kushughulikia masuala ya kijamii, na ingawa sababu ni hitilafu na sio kukatika kwa umeme, kifo cha mmoja wa wahusika ndani ya lifti bado ni tukio ambalo limewatia hofu hadi leo.

Kutokana na kukatika kwa umeme mara kwa mara nchini Misri ajali za lifti zilizosababisha vifo vya baadhi ya watu zimejirudia mara kwa mara, pengine ajali ya hivi karibuni ikiwa ni kifo cha mfanyakazi katika eneo hilo. "Al-Marg" eneo la Cairo, wakati akijaribu kutoka kwenye lifti kati ya sakafu mbili, ambayo ilisababisha ... kujeruhiwa kichwani na shingoni.

Kwa hivyo, ushauri mwingi ulitoka kwenye mitandao ya kijamii, katika jaribio la kuwaelekeza watu jinsi ya kuishi ikiwa mtu amekwama ndani wakati wa kukatika kwa umeme.

Miongoni mwa vidokezo muhimu zaidi ni kile kilichoelezwa kwenye tovuti za ukurasa wa "Jinsi ya kufanya kwa Kiarabu", ambayo inajitambulisha kuwa huduma ya kwanza ya Kiarabu ambayo hutoa mwongozo katika hali mbalimbali.

Maagizo yote yanasisitiza kujaribu kubaki katika hali ya utulivu iwezekanavyo, na kuepuka mafadhaiko kwa kujaribu kupumua. Hapa tumekusanya vidokezo muhimu zaidi ambavyo vitakusaidia kutoka kwenye lifti kwa amani:

Kaa mbali na mlango wa lifti na usijaribu kuruka ili kuisogeza!

Kuruka kwenye lifti hakuna uwezekano wa kuifanya ianze tena kusogea, na kwa kweli inaweza kusababisha shida kubwa zaidi, au kusababisha lifti kushuka ghafla.

Unapaswa kusimama au kukaa kimya , mbali na milango, na kusubiri msaada kufika.

Usijaribu kutoka peke yako kupitia dari ya lifti!

Usijaribu kutoka kwenye lifti kupitia dari, sakafu au njia nyingine yoyote, isipokuwa kwa usaidizi wa huduma za dharura, kwani hii inaweza kuwa hatari zaidi.

Ikiwa unahisi kizunguzungu katika maeneo jaribu kukaa chini!

Usisite kusimama au kukaa, chochote kinachofaa zaidi kwako, lakini ikiwa unahisi kizunguzungu, unapaswa kukaa kwenye sakafu ya lifti na unaweza kufanya mazoezi ya kujinyoosha ikiwa unahisi kufa ganzi katika sehemu nyingine za mwili wako au wasiwasi, lakini unapaswa kuwajali wengine kwenye lifti ikiwa hauko peke yako.

Epuka harakati zozote za ghafla au za kushangaza!

Tumia tochi kwenye simu yako ya mkononi ili kuona vitufe!

Tochi ya simu

Chanzo cha picha, Getty Images

Chanzo cha mwanga hukusaidia kupata vitufe vya dharura na kuamua mwelekeo, hasa ikiwa hakuna chanzo cha mwanga kutoka kwenye paa au upande wa lifti.

Ikiwa huna tochi, tumia mwanga kutoka kwa simu yako au mwanga kutoka kwenye skrini yake ili kutathmini mazingira yanayokuzunguka, lakini jaribu kutoitumia sana baada ya kuamua unachotaka, ili kuhifadhi betri yake.

Ikiwa huna chanzo cha mwanga, usiogope, kaa tu mbali na mlango wa lifti hadi msaada uwasili.

Usibonyeze vitufe vyote au kujaribu kufungua mlango kwa nguvu!

Usibonyeze vitufe vyote

Chanzo cha picha, AFP

Usijaribu kufungua mlango wa lifti kwa kubonyeza vitufe wakati huo huo, kwani hii inaweza kuharibu lifti zaidi na kufanya hali kuwa mbaya zaidi. Usijisumbue kufungua mlango kwa mikono!

Jaribu kutafuta kitufe cha dharura!

Vitufe

Chanzo cha picha, Getty Images

Kila lifti ina kitufe cha dharura, ambacho mara nyingi huwekwa alama nyekundu au alama ya kengele au kitufe cha kupiga simu. Jaribu kuitafuta na uibonyeze kwa sekunde mbili au tatu, na kurudia jaribio hilo kwa muda sawa hadi upate jibu!

Wasiliana na mtunza lifti

Ukiwasiliana na mtunza mali kupitia kitufe cha dharura, mwombe kwanza akate umeme kutoka kwenye lifti ili kuepuka kurudi kwa ghafla kwa umeme, kisha akuinue au akushushe mwenyewe hadi kwenye ghorofa ya karibu ili kukuondoa.

Ikiwa mlango unafunguliwa ghafla, usijaribu kutoka!

Ikiwa lifti imekwama kati ya sakafu mbili na unaweza kufungua mlango, usijaribu kutoka nje na kusubiri usaidizi hadi uwasiliane na mlinzi wa mali ili kukata umeme kutoka kwenye lifti, kwani lifti inaweza kuanza kusogea tena bila kutarajia. kuyaweka maisha yako hatarini.

Toa taarifa kwa namba ya dharura iliyo karibu nawe!

Ikiwa kitufe cha dharura haifanyi kazi, au huwezi kuwasiliana na mtunza mali, jaribu kuwasiliana na mtu wa familia yako, majirani au wafanyakazi wenzako, kulingana na jengo ambalo umekwama! Weka nambari ya dharura kila wakati kwa ulinzi wa raia, kulingana na nchi yako.

Ikiwa una mtandao wa simu, unaweza kutuma ujumbe kwa mtu wa karibu unayemjua anaweza kukusaidia wakati huo.

Piga simu kwa msaada kwa sauti!

usipige kelele! Jaribu kwa kupiga makofi, kugonga ukuta wa lifti, na kuita kwa sauti kuomba usaidizi! Lakini jaribu kutopaza sana sauti yako ili usidhuru afya yako mahali ambapo hakuna njia za dharura za kutosha.

Ikiwa unaogopa kwamba lifti itaanguka, lala chali

Katika hali nadra, lifti inaweza kupata kuanguka, katika hali ambayo ni bora kulala chali kwenye sakafu hatua ambayo itakulinda vizuri kutokana na madhara.

Wasaidie walio karibu nawe!

Ikiwa kuna zaidi ya mtu mmoja ndani ya lifti, baki mtulivu ili kuchukua hatua zinazofaa bila mvutano, na jaribu kumsaidia mtu anayehitaji msaada kwa kumkalisha sakafuni au kutuliza woga wake.

Kwa ujumla, inashauriwa kila mara kuhakikisha kuwa simu yako ya mkononi imechajiwa kabla ya kuondoka nyumbani au mahali pa kazi, ili uitumie wakati wa dharura.

Inashauriwa pia kuuliza mtunzaji wa mali yoyote kuhusu wakati wa kukatika kwa umeme kabla ya kuingia kwenye lifti.

Unaweza pia kuweka nambari ya simu ya mtunza nyumba unayoishi au nambari ya mmoja wa majirani zako. Ili kuitumia ikiwa umekwama ili kupata usaidizi wa haraka.

Ni muhimu kuandika maelezo kwenye lifti ya kila jengo yenye tarehe za kukatika kwa umeme, ili kumwongoza mgeni yeyote anayejaribu kupanda lifti katika kipindi ambacho kinashuhudia kukatika kwa umeme mara kwa mara.

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga