Urusi yakubali kuipa silaha Wagner iliyotishia kujiondoa vitani Ukraine
Bosi wa kundi la Wagner la Urusi anasema Serikali ya Moscow imekubali mahitaji yake ya kuongezewa nguvu zaidi ikiwemo risasi, ikiwa ni siku chache baada ya kutishia kuwaondoa wanajeshi wa kundi hilo walioko Bakhmut.
Siku ya Alhamisi, Yevgeny Prigozhin aliwashambulia washirika wake wa Urusi kwa maneno ya kutisha na yaliyojaa uchokozi, yaliyorekodiwa katikati ya makumi ya maiti za wanajeshi wa Wagner.
Siku iliyofuata alisema wapiganaji wa Wagner wangeondoka Bakhmut ifikapo tarehe 10 Mei. Lakini leo Jumapili Prigozhin ilisema Moscow imekubali kutoa vifaa "vinavyohitajika ili kuendelea kupigana" katika jiji hilo.
Kubadili kwa msimamo huo kwa Prigozhin sio jambo la kushangaza. Yeye hupenda kujitangaza. Wanajeshi wa Urusi na wapiganaji kutoka Wagner, kampuni ya kijeshi ya kibinafsi, wamekuwa wakijaribu kuuteka mji wa Bakhmut kwa miezi kadhaa sasa- licha ya thamani yake ya kimkakati ikitiliwa shaka.
Maafisa wa nchi za Magharibi wanaamini kuwa maelfu ya wanajeshi wa Urusi na Wagner wameuawa katika mapigano hayo. Licha ya wanajeshi wa Urusi na wapiganaji wa Wagner kuwa upande mmoja dhidi ya Ukraine - ni muungano usio na utulivu.
Prigozhin amewakosoa maafisa wa Urusi mara kwa mara kwa kile anachodai kuwa ni ukosefu wa uungwaji mkono wa kikosi chake kilicho mstari wa mbele.
Katika taarifa yake mpya, Prigozhin alidai kuwa Jenerali Sergei Surovikin - ambaye aliongoza vikosi vya Urusi nchini Ukraine kati ya Oktoba na Januari - aliteuliwa kuwa mtu wa kati, kati ya jeshi la kawaida la Urusi na mamluki wa Wagner.
"Huyu ndiye mtu pekee aliye na nyota ya jenerali wa jeshi ambaye anajua kupigana," Prigozhin alisema. "Hakuna jenerali mwingine wa jeshi mwenye busara."