Vita vya Ukraine: Urusi yakubali kulipa kundi la Wagner silaha za kuuteka mji wa Bakhmut.

Kundi hilo la Wagner lilitishia kujiondoa Bakhmut ifikapo tarehe 10 Mei, 2023 kama Urusi isingekubali kutoa silaha za kulisaidia.

Moja kwa moja

  1. Urusi yakubali kuipa silaha Wagner iliyotishia kujiondoa vitani Ukraine

    Ukraine war

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Bosi wa kundi la Wagner la Urusi anasema Serikali ya Moscow imekubali mahitaji yake ya kuongezewa nguvu zaidi ikiwemo risasi, ikiwa ni siku chache baada ya kutishia kuwaondoa wanajeshi wa kundi hilo walioko Bakhmut.

    Siku ya Alhamisi, Yevgeny Prigozhin aliwashambulia washirika wake wa Urusi kwa maneno ya kutisha na yaliyojaa uchokozi, yaliyorekodiwa katikati ya makumi ya maiti za wanajeshi wa Wagner.

    Siku iliyofuata alisema wapiganaji wa Wagner wangeondoka Bakhmut ifikapo tarehe 10 Mei. Lakini leo Jumapili Prigozhin ilisema Moscow imekubali kutoa vifaa "vinavyohitajika ili kuendelea kupigana" katika jiji hilo.

    Ukraine war

    Chanzo cha picha, CONCORD PRESS SERVICE

    Kubadili kwa msimamo huo kwa Prigozhin sio jambo la kushangaza. Yeye hupenda kujitangaza. Wanajeshi wa Urusi na wapiganaji kutoka Wagner, kampuni ya kijeshi ya kibinafsi, wamekuwa wakijaribu kuuteka mji wa Bakhmut kwa miezi kadhaa sasa- licha ya thamani yake ya kimkakati ikitiliwa shaka.

    Maafisa wa nchi za Magharibi wanaamini kuwa maelfu ya wanajeshi wa Urusi na Wagner wameuawa katika mapigano hayo. Licha ya wanajeshi wa Urusi na wapiganaji wa Wagner kuwa upande mmoja dhidi ya Ukraine - ni muungano usio na utulivu.

    Prigozhin amewakosoa maafisa wa Urusi mara kwa mara kwa kile anachodai kuwa ni ukosefu wa uungwaji mkono wa kikosi chake kilicho mstari wa mbele.

    Ukraine war

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Katika taarifa yake mpya, Prigozhin alidai kuwa Jenerali Sergei Surovikin - ambaye aliongoza vikosi vya Urusi nchini Ukraine kati ya Oktoba na Januari - aliteuliwa kuwa mtu wa kati, kati ya jeshi la kawaida la Urusi na mamluki wa Wagner.

    "Huyu ndiye mtu pekee aliye na nyota ya jenerali wa jeshi ambaye anajua kupigana," Prigozhin alisema. "Hakuna jenerali mwingine wa jeshi mwenye busara."

  2. Mapigano Sudan: 'Nilikimbia na kaptula tu na nmerudi Nigeria na blanketi tu'

    Charles Collins

    Chanzo cha picha, Charles Collins

    Charles Collins alikuwa anajiandaa na mechi yake inayofuata katika Ligi Kuu ya Sudan wakati mapigano yalipozuka nchini humo tarehe 15 Aprili, na kuligeuza jiji aliloishi kuwa eneo la vita.

    Mchezaji soka huyo raia wa Nigeria mwenye umri wa miaka 28, na anayechezea klabu ya Haidob en Nahud ya Khartoum, alisema alilazimika kuacha mali zake zote, na kukimbia akiwa na kaptula nyeusi tu aliyokuwa amevaa, wakati mapigano kati ya jeshi na kundi kubwa la wanamgambo yalipomfikia jirani na mji mkuu wa Sudan.

    Alikuwa miongoni mwa Wanigeria 396 waliorejea Abuja kutoka Misri wiki hii, baada ya kutoroka kutoka Sudan katika kile ambacho wengi walieleza kuwa ni safari hatari iliyochukua siku kadhaa.

    Sudan

    Chanzo cha picha, Getty Images

    "Ninarudi nyumbani na hiki tu, blanketi langu tu," aliiambia BBC katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abuja, akizunguka huku akifunua mkoba wake mweusi.

    "Nilitoka nje ya nyumba yangu nikiwa nimevaa kaptula tu, ulikuwa ni uzoefu mbaya," alisema. Haidob, ambaye imepandishwa daraja kucheza ligi kuu msimu huu, ilikuwa mbioni kufuzu Kombe la Mashirikisho la Caf - michuano ya pili kwa ukubwa barani Afrika.

    Timu hiyo ilichapwa 1-0 na Kober SC Bhari wiki moja kabla ya mapigano kuanza lakini ikasalia katika nafasi ya nne kwenye ligi ambayo sasa imesimama.

    Lakini anasema baada ya yale aliyopitia, Collins haoni akirejea Sudan kuendelea na soka lake.

  3. Aua watu 8 kwa risasi dukani wakiwemo watoto

    USA

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mtu mwenye silaha amewashambulia kwa risasi na kuwauwa watu wanane waliokuwa wakifanya ununuzi katika moja ya maduka makubwa kaskazini mwa Dallas, Texas.

    Mamia ya watu waliondolewa kutoka kwa maduka ya Allen Premium Outlets huku watu walioshuhudia wakieleza mtu huyo alikuwa akiwafyatulia risasi wapita njia kiholela.

    Afisa wa polisi aliyekuwa karibu na eneo la tukio alimuua mtu huyo mwenye bunduki baada ya kusikia milio ya risasi. Baadhi ya walioshambuliwa wanaripotiwa kuwa watoto.

    Takriban watu saba wanatibiwa hospitalini, watatu kati yao ni wakiwa mahututi. Mkuu wa Zimamoto Allen Jonathan Boyd alisema watu saba - ikiwa ni pamoja na mshambuliaji huyo - walitangazwa kufariki katika eneo la tukio na wawili walikufa baadaye hospitalini.

    Afisa usalama katika jengo la maduka "alisikia milio ya risasi, akaenda kwenye eneo la tukio, na kufanikiwa kumzuia mshukiwa," Mkuu wa Polisi wa Allen Brian Harvey alisema.

    Watu walioshambuliwa wanatajwa kuwa na umri kati ya miaka 5 hadi 51, kulingana na msemaji wa hospitali.

  4. Rais Samia ataka Baraza la vyama vya siasa kukutana kuhusu Katiba mpya

    Samia

    Chanzo cha picha, Ikulu

    Baraza la Vyama vya Siasa nchini Tanzania limetakiwa kukutana ili kutathimini utekelezaji wa mapendekezo ya kikosi kazi kilichokuwa kikiratibu maoni ya watu mbalimbali kuhusu demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini.

    Rais Samia Suluhu Hassan amemuagiza Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kuitisha kikao hicho cha baraza linaloundwa na vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu Tanzania.

    Rais Samia ametoa agizo hilo Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma alipofanya kikao na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Jaji Mutungi na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Bunge na Uratibu) Jenista Mhagama na Waziri wa Katiba na Sheria Dk Damas Ndumbaro.

    Mbali ya mchakato wa Katiba, masuala mengine yanayotarajiwa kushughulikiwa ni marekebisho ya sheria mbalimbali zinazohusiana na uchaguzi, zikiwemo sheria za Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Msajili wa vyama vya Siasa.

  5. Vita vya Ukraine: Urusi yahamisha raia karibu na Kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia hofu ikitanda ya mashambulizi

    UKRAINE

    Chanzo cha picha, EPA

    Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) ameelezea wasiwasi wake kuhusu usalama wa kinu kikubwa zaidi cha nyuklia barani Ulaya huku vikosi vya Urusi vikiwahamisha raia kutoka mji wa karibu wa Enerhodar nchini Ukraine.

    Rafael Grossi alisema hali katika kinu cha Zaporizhzhia "inazidi kuwa isiyotabirika na inayoweza kuwa hatari".

    Uhamisho huo wa kuondoa watu unakuja kabla ya shambulio linalotarajiwa kufanywa na Ukraine.

    Lakini wafanyakazi kwenye kinu hicho cha nyuklia wameendela kusalia hapo.

    Taarifa ya IAEA ilisema kwamba "wakati wafanyakazi wanaofanya kazi wanasalia kwenye kunu hicho, Mkurugenzi Mkuu Grossi alionyesha wasiwasi mkubwa kuhusu hali inayozidi kuwa ya wasiwasi, hofu, na changamoto kwa wafanyakazi hao na familia zao".

    Alisema wataalam wa IAEA waliokuwepo kwenye kiwanda hicho "wamepokea taarifa kwamba uondoaji wa wakaazi tu umeanza kutoka mji wa karibu wa Enerhodar - ambapo wafanyakazi wengi wa kinu hicho wanaishi".

    BBC haikuweza kuthibitisha ukubwa wa zoezi hilo lilioripotiwa na idadi ya watu waliohamishwa.

    Bw Grossi alisema "lazima tuchukue hatua sasa ili kuzuia tishio la ajali mbaya ya nyuklia".