Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Kambi ya mafunzo ya kijeshi Urusi yavamiwa 11 wauawa

Watu wawili walilifyatulia risasi kundi la askari waliojitolea kupigana nchini Ukraine, wakiwa kwenye mafunzo

Moja kwa moja

  1. Tumefika mwisho wa matangazo ya habari zetu za moja kwa moja, tukutane kesho majaliwa

  2. EPL: Arsenal haishikiki, United yalazimishwa sare nyumbani

    Arsena imeendelea kukaa kileleni baada ya ushindi wake wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Leeds United. Bao la Bukayo Saka anayefunga mabao 4 katika mechi 3 za mashindnao yote zilizopita, zinaifanya Arsenal kufikisha alama 27.

    Patrick Bamford wa Leeds alikosa penati katika dakika ya 64 baada ya William Saliba kuunawa mpira katika eneo la hatari. Ulikuwa mchezo mgumu kwa Arsenal.

    Arsenal iliyoanza vizuri zaidi ligi ya msimu huu pengine kuliko msimu wowote wa karibu muongo mmoja uliopita, itakutana na Southampton iliyotoka sare leo dhidi ya West ham, katika mchezo ujao.

    Katika michezo mingine Manchester United imelazimishwa sare ya 0-0 na Newcastle United, Chelsea imeichapa Aston Villa ugenini 2-0. Machester City iko ugenini sasa inacheza na Liverpool. Mchezo umeanza na matokeo yakiwa 0-0.

  3. Simba yatinga makundi fainali Afrika, yaichapa de Agosto 1-0

    Klabu ya Simba ya Tanzania imefanikiwa kufuzu hatu ya makundi ya klabu bingwa Afrika baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Primeiro de Agosto ya Angola.

    Mchezo huo umemalizika punde katika uwanja wa taifa kwa bao la Moses Phiri.

    Katia mchezo wa kwanza Angola, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-1, na sasa imefuzu kwa jumla ya mabao 4-1.

  4. Rais Samia ataka wananchi kupunguza kasi ya kuzaa Tanzania

    Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi wake kupunguza kasi ya kuzaa, kutokana ongezeko la idadi kubwa ya watoto wanaozaliwa kwa sasa.

    Ametoa kauli hiyo baada ya kushtushwa na taarifa aliyopewa kuhusu idadi kubwa ya watoto wanaozaliwa kwa mwezi.

    Akizungumza na wananchi hao wa Bukombe, magharibi mwa Tanzania, Rais Samia alitoa kauli hiyo akiwata wapunguze kasi. ''Jana nimesimama Buselesele pale, nikaambiwa kituo kimoja (cha afya) kinazalisha watoto 1,000 kwa mwezi, sasa hayo madarasa baada ya miaka 3 ni mangapi?, kama ni vituo vya afya ni vingapi? tani za chakula ni ngapi,? kidogo speed (kasi) tupunguze kidogo'', alisema rais Samia.

    Rais Samia aliyasema hayo wakati wa ziara yake ya kawaida ya kiserikali ndani ya nchi hiyo.

    Katika kiwango cha sasa cha ukuaji wa idadi ya watu, idadi ya watu huongezeka mara mbili katika kipindi cha miaka 25.

    Wakati ikisubiriwa taarifa rasmi ya sensa ya watu iliyofanyika mwaka huu, nchi hiyo inakadiriwa kuwa na watu zaidi ya milioni 60, kutoka kadirio la watu milioni12.5, katika miaka ya 1960.

  5. Maelfu waandamana dhidi ya rais Tunisia

    Maelfu ya waandamanaji wamejitokeza katika mitaa ya mji mkuu wa Tunisia kuandamana dhidi ya rais wa nchi hiyo.

    Maandamano kama hayo ya makundi ya kisiasa yanayopingana vikali yalifanyika Tunis.

    Makundi yote mawili yalimkashifu rais Kais Saied kama mbabe ambaye anabadilisha na kufifisha maendeleo ya kidemokrasia yaliyopatikana tangu ghasia za 2011.

    Pia walitaka uwajibikaji kutokana na mdodoro wa kiuchumi nchini humo ambao umeshuhudia uhaba mkubwa wa chakula na mafuta.

    Wakosoaji wa Bw Saied wanamtuhumu kwa kufanya mapinduzi na kujaribu kurudisha Tunisia katika utawala wa kiimla - mfumo wa serikali unaoendeshwa na mtu mmoja mwenye mamlaka kamili.

  6. Tuzo za WTA 2022: Serengeti yashinda tuzo ya hifadhi bora Afrika mara nne mfululizo

    Hifadhi ya Taifa Serengeti nchini Tanzania imeshinda tuzo ya Hifadhi bora zaidi Afrika kwa mwaka 2022 .

    Hii ni kwa mara ya nne mfululizo tangu 2019,2020,2021 na sasa 2022, hifadhi hiyo inashinda

    Hifadhi hiyo imezibwaga hifadhi za Central Kalahari ya Botswana, Kruger National Park ya Afrika Kusini, Kidepo Valley Nationa Park (Uganda), Etosha National park (Namibia) na Masai Mara National Reserve ya Kenya.

    Tuzo hizo zilizoanzishwa mwaka 1993 kutambua na kutunza ubora wa urithi huo wa rasilimali za hifadhi, zinatolewa World Travel Award (WTA) na zinatambulika kimataifa.

  7. Wanne wafariki 61 hoi moto mkubwa ukizuka katika gereza maarufu Iran

    Wafungwa wanne na wengine 61 wamethibitika kufariki dunia baada ya kuzuka kwa moto mkubwa siku ya Jumamosi katika gereza maarufu la Evin nchini Iran, linalojulikana kwa kuhifadhi wafungwa wa kisiasa, waandishi wa habari na raia wa kigeni.

    Video zilizosambaa mtandaoni zilionyesha moto na moshi mkubwa kwenye gereza hilo huko Tehran, huku milio ya risasi na milipuko ilisikika.

    Afisa aliyenukuliwa na vyombo vya habari vya serikali alisema hali imedhibitiwa, lakini picha za video zilionekana kuonyesha moto huo ukiendelea.

    Kwa wiki kadhaa sasa Irani imekumbwa na maandamano makubwa dhidi ya serikali. Kwa mara ya kwanza maandamano hayo yalianza mwezi uliopita baada ya kifo cha Mkurdi wa Irani Mahsa Amini mwenye umri wa miaka 22 akiwa chini ya ulinzi wa polisi.

    Maafisa walisema alikufa kwa mshtuko wa moyo, lakini familia yake ilipinga hili, ikisema alipigwa na polisi wa maadili.

    Mwandishi wa BBC Mwajemi Rana Rahimpour alisema bado haijajulikana iwapo tukio hilo linahusishwa na maandamano ya hivi majuzi. Lakini hii inaweza kuwa hivyo kwa urahisi, Rana alisema, kwani mamia ya waandamanaji wanashikiliwa kwenye gereza hilo la Evin.

    Vyombo vya habari vya serikali vinakanusha hilo, vikimnukuu afisa mmoja ambaye alilaumu "wahalifu" kwa moto huo.

    Akizungumza kutoka ndani ya gereza hilo, gavana wa Tehran aliiambia televisheni ya taifa kwamba kulikuwa na ghasia katika gereza hilo na imedhibitiwa. Athari za moto huo hazijathibitishwa inhawa taarifa za awali zinaonyesha watu 8 wamejerubiwa.

  8. Marekani: Urusi imesaini mkataba mpya na Iran wa kusambaza ndege zisizo na rubani

    Urusi inaweza kuwa imetia saini mkataba mpya na Iran wa usambazaji wa ndege zisizo na rubani aina ya Arash-2, ripoti ya Taasisi ya Marekani ya Utafiti wa Vita (ISW) inasema.

    Wataalamu wa kijeshi wamenukuu taarifa kutoka chaneli za Telegram za Urusi na Kiukreni ambazo "zimevuja" na taarifa kutoka kwa vyanzo vya Iran ambavyo havikutajwa.

    Idadi kamili ya ndege zisizo na rubani zilizonunuliwa bado hazijulikani. Mnamo Septemba, Brigedia Jenerali Kiomars Heydari, Kamanda wa Vikosi vya Ardhi vya Iran, alisema kuwa ndege zisizo na rubani za Arash-2 zina uwezo wa kipekee wa masafa marefu na zinaweza kushambulia miji ya Israel kama vile Tel Aviv na Haifa kutoka kambi za Iran. Walakini, wataalam wa kijeshi wana shaka kuwa vikosi vya Urusi vitaweza kutumia Arash-2 kwa ufanisi zaidi kuliko walivyotumia Shahed-136.

    '' Kuna ripoti kwamba Moscow inaendelea kutegemea Tehran kwa mabomu haribifu, ripoti kutoka Idara ya Hazina ya Marekani ambayo inapendekeza kwamba Urusi inapanua haraka usambazaji wake wa vifaa vya elektroniki ambavyo ni muhimu kwa eneo la kijeshi na viwanda kwa sababu haiwezi kuchukua nafasi ya vifaa muhimu ambavyo havipatikani kwa sababu ya vikwazo. Urusi itaendelea kuinua uhusiano wake na Iran ili kukwepa vikwazo, ingawa kuna uwezekano mkubwa kwamba vikosi vya Urusi vitatumia Arash-2 kwa athari kubwa zaidi kuliko vile vilivyotumia modeli ya Shahed''. Ilisema taarifa hiyo.

  9. Mason Greenwood wa Man United kufikishwa Mahakamani tena

    Mshambuliajii wa Manchester United Mason Greenwood atafikishwa mahakamani kesho baada ya kukamatwa tena kwa madai ya kukiuka masharti ya dhamana yake.

    Greenwood, mwenye umri wa miaka 21, alikamatwa kwa mara ya kwanza mwezi Januari kwa tuhuma za ubakaji na kushambulia lakini pia akahojiwa kuhusu madai ya vitisho vya kuua.

    Na hiyo ilikuwa baada ya picha na video kusambaa mtandaoni zikimuonyesha mchezaji huyo wa Kiingereza.

    Mnamo Februari 2021, Greenwood alisaini mkataba wa miaka minne kusalia Manchester United, akiichezea pia timu ya taifa ya England mara moja.

    Kesi ya msingi ya Greenwood bado haijafanyika, na alikamatwa jana akiwa nyumbani kwake jijini Manchester. Akionekana kukiuka masharti hayo ambayo hajawekwa wazi.

  10. Kambi ya mafunzo ya kijeshi Urusi yavamiwa 11 wauawa

    Watu wenye silaha wamewaua askari 11 wa Urusi wanaojitolea, katika shambulizi moja kwenye eneo la mafunzo ya kijeshi la Urusi siku ya Jumamosi.

    Wakati wa mafunzo ya kutumia silaha, watu wawili walilifyatulia risasi kundi la askari hao lililojitolea kupigana nchini Ukraine, shirika la habari linalomilikiwa na serikali Ria liliripoti.

    Washambuliaji hao wanatajwa walitoka katika jamhuri ya zamani ya Soviet, wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema, lakini haikutoa maelezo zaidi.

    Watu hao waliuawa kwa kupigwa risasi wakati wa tukio hilo katika eneo la Belgorod nchini Urusi, ambalo linapakana na Ukraine. Watu wengine 15 walijeruhiwa.

    Gavana wa eneo hilo alisema hakuna wakaazi wa eneo la Belgorod aliyeuawa au kujeruhiwa.

    Mwezi uliopita Rais wa Urusi Vladimir Putin aliamuru kukusanywa kwa Warusi 300,000 ambao hapo awali walikuwa wamefanya kazi ya lazima ya kijeshi. Agizo hilo lilizua maandamano kote Urusi, na kuongezeka kwa idadi kubwa ya watu wanaojaribu kuondoka nchini.

    Muda mfupi tu baada ya uhamasishaji huo kutangazwa, mmoja wa watu wanaiajiri wanajeshi wa nchi hiyo alipigwa risasi katika ofisi ya uandikishaji ajira huko Siberia.

    Wiki iliyopita, Putin alitangaza kwamba zaidi ya watu 200,000 walikuwa tayari wamehamasishwa kujiunga, hata hivyo alisema kuna haja ya uhamasishaji zaidi.

  11. Ebola Uganda: Wilaya mbili zawekewa zuio la watu kutotoka nje, masharti 21 yakitangazwa

      • Author, Isaac Mumema
      • Nafasi, BBC Swahili

    Rais wa Uganda Yoweri Museveni ametangaza amri ya kutotoka nje ya wiki tatu kwa wilaya mbili zilizoathirika kuzuia maambuzi ya ugonjwa wa Ebola ya Sudani.

    Amri hiyo ni sehemu ya masharti 21 ya kukabiliana na mlipuko mpya wa ugonjwa huo uliotangazwa nchini humo Septemba 20, 2022.

    Mpaka kufikia jana watu 58 wamethibitishwa kuambukizwa Ebola, 19 wamefariki na 20 wamepona wakiwemo Madaktari na wafanyakazi wa sekta ya afya.

    Katika hotuba yake kwa taifa usiku wa kuamkia leo masharti hayo aliyoweka ni pamoja na kuweka zuio kuanzia leo Jumapili la watu kutotoka nje katika wilaya za Mubende na Kasanda kuliko bainika mgonjwa wa kwanza.

    Nyumba za Ibada zote zimefungwa pamoja na maeneo ya starehehe ikiwemo Baa, kumbi za disko, vibanda vya filamu pamoja na shughuli zote za michezo.

    Usafiri wa umma na binafsi yaani mabasi, dalala, magari ya watu binafisi na boda boda kuuanzia leo zimezuiwa kutotembea usiku kuanzia saa moja jioni hadi saa kumi na mbili asubuhi.

    Hatua hii ya Rais Museveni inafutiia ombi la chama cha Madaktari nchini humo mwezi jana kupitia kwa rais wao Samuel Oledo waliomba Rais Museveni kuziweka karantini wilaya zilizo na maambukizi.

    Hata hivyo mpaka sasa wilaya tano ndizo zilizo na maambukizi lakini zikizoguswa ni mbili kunakotajwa ndiko chimbuko la mlipuko wa sasa.