Siku moja baada ya Rais Gotabaya Rajapaksa kuondoka nchini humo, Waziri mkuu wa Sri Lanka Ranil Wickremesinghe ametangaza hali ya hatari na kutangaza amri ya kutotoka nje huko magharibi, taarifa ofisi ya waziri mkuu imesema.
Huko Galle Face Green - kitovu kikuu ya maandamano ya Sri Lanka - waandamanaji wamekasirishwa kwa kitendo cha kuondoka kwa Rais wa nchi hiyo Gotabaya Rajapaksa.
Maelfu ya waandamanaji wamepambana na polisi leo, wakiandamana kwenye ofisi ya waziri mkuu wakimtaka aondoke.
Waziri mkuu huyo alitangaza wiki iliyopita kung;atuka madarakani lakini hakusema ni lini hasa atafanya hivyo. Hali hiyo kumefanya kuwa na ombwe la uongozi, kutokana na wananchi kutomuunga mkono waziri mkuu na hata spika wanaopaswa kikatiba kushika hatamu kwa muda kutokana ukaribu wao na rais Rajapaksa.
“Hatupendi. Tunataka asalie hapa. Tunataka kurudishiwa pesa zetu! Na tunataka kuwaweka Rajapaksa wote katika gereza la wazi ambapo wanaweza kufanya kazi za mashambani,” alisema mwandamanaji GP Nimal ambaye ametumia siku 43 zilizopita kuandamana katia eneo la Galle Face Green.
"Hakuna haki," alisema.
Tulipokuwa tukizungumza, tuliunganishwa na kijana mmoja ambaye alisema alikuwa anatoka Maldives na alihamia Sri Lanka hivi majuzi.
Alipoambiwa kwamba Bw. Rajapaksa alikuwa amekimbilia Maldives, alinung'unika kwa maneno ya upole na kucheka.
"Hii ni aibu sana," alisema. "Hii sio nzuri. Hata Maldives ni kuna ufisadi na inaelekea upande uleule.”
Ndugu kutoka familia moja ya Rajapaksa, Mahinda na Gotabaya, walisifiwa na wengi kuwa mashujaa kwa kushinda vita vya wenyewe kwa wenyewe lakini sasa wanatukanwa kama viongozi walioshindwa kusaidia Sri Lanka.
Ni anguko kubwa la neema kwa familia hiyo ambayo imetawala siasa za Sri Lanka kwa zaidi ya muongo mmoja.
Mahinda Rajapaksa aliwahi kuonekana shujaa kwa kukomesha takriban miongo mitatu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe wakati waasi wa Tamil Tiger walipoangamizwa mwaka wa 2009 wakati wa muhula wake wa kwanza kama rais.
Baba yake alikuwa mbunge na Mahinda mwenyewe polepole alipanda kutoka kuwa kiongozi wa upinzani bungeni hadi kuwa Waziri mkuu mnamo 2004.
Alipokuwa rais mwaka mmoja baadaye, alimteua ndugu yake Gotabaya (rais wa sasa aliyekimbia nchi) kuwa waziri wa ulinzi.
Ilikuwa kazi kubwa kwa kaka mdogo huyo ambaye alikuwa akiishi maisha ya utulivu huko Marekani baada ya kustaafu jeshi la Sri Lanka.
Gotabaya alipata umaarufu, na kupata sifa ya ukatili.
Muda si muda, ndugu na jamaa wengine wakaanza kupewa nafasi na kujiunga na serikali. Sasa wananchi wanaoandamana wanataka ndugu wote wa familia ya Rajapaksa wakamatwe na waswekwe ndani kwa shutuma za kujilimbikizia mali na kuwaaacha wananchi kuwa na hali mbaya kutokana na mdororo wa kiuchumi.