Jeshi la Jamuhuri ya Kidemokrasi
ya Congo, FARDC, limetangaza kuwa wanajeshi watatu
wa Tanzania wanaohudumu katika kikosi cha walinda amani cha Umoja wa Mataifa MONUSCO
wamejeruhiwa wakati wapiganaji wa M23 waliposhambulia ngome yao iliyopo Rutshuru.
MONUSCO imethibitisha kuwa
wanajeshi wake watatu wamejeruhiwa na kupelekwa kutibiwa katika hospitali ya
mjini Goma uliopo mashariki. Katika tangazo hilo jeshi la serikali ya Congo
limesema mmoja wa wanajeshi hao amejeruhiwa vibaya.
Kundi la M23 linasema kuwa
majeshi ya FARDC na MONUSCO ndio waliokuwa wa kwanza kufanya mashambulizi dhidi yao katika ngome yao iliyopo katika eneo la Jomba
Jumatatu.
Hii inakuja wakati mapigano
yakiendelea kwa siku ya nne mfulurizo kati ya pande hizo yaliyoibuka baada ya mapigano
hayo kusitishwa kwa muda wa wiki mmoja-
mapigano yanayoendelea katika eneo la Rutshuru katika eneo la Kivu ya Kaskazini.
MONUSCO ilitangaza kuwa ipo
katika mapigano ikilisaidia jeshi la Congo, FARDC linalopigana na wapiganaji wa M23.
Tanzania ina wanajeshi zaidi ya 800 katika kikosi cha MONUSCO kinachohudumu Mashariki mwa
DRC.
Katika taarifa yake iliyotolewa Jumatano usiku,
jeshi la DRC, FARDC linaishutumu Rwanda kutuma kikosi chake maalum
cha wanajeshi 500 kuwasaidia wapiganaji
wa M23, likisema kuwa walikuja wakiwa
wamevalia mavazi yenye rangi ya kijani kibichi na nyeusi.
Serikali ya Rwanda kwa upande wake imekuwa ikikana mara kwa mara kuwa inawasaidia M23, ikisisitiza kuwa tatizo
lao liko ndani ya nchi yao wenyewe ya
DRC.
Kikundi cha M23 Jumatano pia kilitoa
tangazo kikiishutumu serikali kwa ‘’kuchagua njia ya vita’’, kwa vikosi vyake
kushirikiana na wanajeshi wa MONUSCO na
wapiganaji wa kundi linaloshutumiwa na Rwanda kufanya mauaji ya kimbari ya
mwaka 1994 la FDLR kuwashambulia.
Tangazo hil la M23 linasema: “Kuchagua vita kwa serikali ya Congo badala ya kuchagua mazungumzo ya
amani, ni tatizo katika kurejesha amani katika mashariki mwa DRC”.
Wakati huo huo, jeshi la DRC- FARDC
limetangaza kuwa maazimio ya kikao cha wakuu wa majeshi kilichofanyika Goma ya kubuni kikosi maalumu cha kupigana na
makundi ya wanamgambo mashariki mwa
Congo, yatawasilishwa mbele ya kikao cha wataalamu wa masuala ya kijeshi na
wakuu wa majeshi kitakayofanyika kati ya
tarehe 15 na 19 mwezi huu mjini Nairobi Kenya, kabla ya kuidhinishwa na marais wa Kanda.
-
Mzozo wa DRC na Rwanda : M23, majirani na bahati mbaya ya DRC
-
Rwanda: Hatuhusiki na mashambulizi ya M23 DRC
-
DR Congo: FARDC yaishtumu Rwanda kwa kuisaidia M23