Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Zaidi ya watu 20 wachomwa moto wakiwa kwenye basi Nigeria

Takriban abiria 21, wakiwemo watoto, waliteketea hadi kufa wakati basi lao lilipovamiwa na watu wenye silaha katika jimbo la Sokoto, kaskazini-magharibi mwa Nigeria, polisi walisema.

Moja kwa moja

  1. Na kufikia hapo tunatamatisha matangazo haya ya moja kwa moja. Hadi kesho kwaheri.

  2. Walinda amani Saba wa Umoja wa Mataifa wauawa katika mlipuko huko Mali

    Wanajeshi saba wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wameuawa katika mlipuko nchini Mali Jumatano, ujumbe wa kikosi hicho nchini humo unasema.

    Walikuwa safarini katika eneo la katikati mwa Mali msafara wao uliposhambuliwa kwa vilipuzi vya kujitengenezea, au IED.

    Wengine watatu walijeruhiwa vibaya katika mlipuko huo.

    Ni vifo vya hivi punde zaidi wa wanajeshi wanaohudumu katika Umoja wa Mataifa nchini Mali.

    Siku ya Jumatatu mlinda amani alifariki wiki mbili baada ya gari lake kulipiliwa na kwa guruneti.

  3. Wachezaji wanane wa Tottenham wapatikana na corona

    Mkufunzi wa Tottenham Antonio Conte anasema wachezaji wanane na maafisa watano wa klabu hiyo wamepatikana na ugonjwa wa Covid-19.

    Spurs wamepangiwa kucheza mechi dhidi ya Rennes katika michuano ya Ligi Europa siku ya Alhamisi na Uefa inasema "mechi hiyo itaendelea kama ilivyopangwa".

    Baada ya hapo watachuana na Brighton Jumapili katika mechi ya Ligi Kuu ya England ambayo inaaminiwa kuwa inafanyiwa tathmini.

    "Kila siku watu zaidi wanathibitishwa kuwa na virusi," alisema Conte.

    "Hali sio nzuri kabisa."

    Kufuatia mchezo dhidi ya Brighton, Tottenham watamenyana na Leicester City tarehe 16 Desemba na Liverpool tarehe 19 Disemba katika ligi ya daraja la kwanza kabla ya robo fainali ya Kombe la EFL dhidi ya West Ham mnamo Disemba 22.

    "Kuzungumzia soka leo haiwezekani. Hali ya mwisho ilinifadhaisha sana," alisema Muitaliano huyo.

    "Hali ni mbaya, kuna maambukizi makubwa.

    “Tunajiandaa kwa ajili ya mchezo dhidi ya Rennes, lakini ni mgumu sana.

  4. Waziri Mkuu wa Ethiopia arejea ofisini 'kwa muda mfupi'

    Ofisi ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed inasema amerejea ofisini "kwa muda mfupi".

    Hii wanasema ni "kufuatia kukamilika kwa mafanikio kwa awamu ya kwanza ya 'Operesheni ya Umoja wa Kitaifa".

    Ofisi hiyo iliweka kwenye mtandao wa Twitter taarifa ya Waziri Mkuu:

    Waziri Mkuu amekuwa mstari wa mbele katika vita vinavyoendelea vya wenyewe kwa wenyewe , ambavyo vilianza Tigray mwaka jana.

    Jeshi la taifa limekuwa likipigana na waasi kutoka kaskazini.

    Katika siku za hivi karibuni Bw Abiy ametangaza ushindi huku wanajeshi wa wa muungano wakikomboa tena maeneo yaliyokuwa chini ya udhibiti wa waasi.

    Waasi hao hata hivyo wamekuwa wakisisitiza kuwa wamejiondoa kimkakati kutoka katika maeneo hayo.

  5. Olaf Scholz wa Ujerumani achukua nafasi ya Merkel kama kansela

    Olaf Scholz ameapishwa kama kansela mpya wa Ujerumani, na kuhitimisha miaka 16 ya kihistoria ya Angela Merkel kama kiongozi.

    Alipigiwa kura na bunge la Ujerumani, ambapo muungano wake wa vyama vitatu una wabunge wengi.

    Wanademokrasia wake wa mrengo wa kati wa Social Democrats watatawala pamoja na Greens na Free Democrats-rafiki wa kibiashara.

    Kukabidhiwa madaraka kunaashiria mwisho wa maisha ya kisiasa ya Bi Merkel ya miaka 31.

    Bw Scholz, mwenye umri wa miaka 63, alikiongoza chama cha Social Democrats kupata ushindi wa uchaguzi mwishoni mwa Septemba, akijinadi kama mgombeaji wa kuendelea kwa sababu alikuwa na jukumu muhimu katika serikali ya Merkel kama makamu wa kansela.

    Bunge la Ujerumani, Bundestag, liliunga mkono uteuzi wake kwa kura 395 dhidi ya 303, na kisha akateuliwa rasmi kama kansela wa tisa wa Ujerumani na Rais Frank-Walter Steinmeier.

  6. Jeshi la Uganda laghadhabishwa na vikwazo vya Marekani dhidi ya mkuu wake wa ujasusi

    Jeshi la Uganda limelalamikia vikwazo vya kifedha vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Meja Jenerali Abel Kandiho, mkuu wa ujasusi wa kijeshi wa nchi hiyo.

    Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda lilisema katika taarifa yake Jumanne kwamba vikwazo hivyo viliwekwa bila kufuata utaratibu na kwa kupuuza kabisa kanuni ya kusikilizwa kwa haki.

    Ilisema imesikitishwa kwamba hatua kama hiyo imechukuliwa na nchi ambayo Uganda inaiona kuwa rafiki na mshirika mkubwa.

    Katika kuweka vikwazo hivyo, Hazina ya Marekani ilisema kuwa Bw Kandiho na maafisa wengine wa kijasusi wa kijeshi walikamata, kuwaweka kizuizini na kuwanyanyasa kimwili watu "kutokana na utaifa wao, mitazamo ya kisiasa, au ukosoaji wa serikali ya Uganda".

    Ilisema kwamba waliokamatwa "walipigwa na kufanyiwa vitendo vingine vya kutisha... ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kijinsia na kupigwa na umeme, mara nyingi kusababisha majeraha makubwa ya muda mrefu na hata kifo".

    Vikwazo hivyo vimekuja baada ya ripoti kuwa programu za ujasusi zilizotengenezwa na kampuni ya mtandao ya Israel ya NSO Group, zilitumika kudukua simu za wafanyakazi wa ubalozi wa Marekani nchini Uganda.

    Mwezi Aprili, Marekani iliweka marufuku ya usafiri dhidi ya maafisa wa Uganda ikisema walihusika na ukiukaji wa haki za binadamu unaohusishwa na uchaguzi mkuu wa Januari.

  7. Bendera ya Tanzania kusimikwa kwenye kilele cha mlima Kilimanjaro

    Bendera ya Tanzania itasimikwa kwenye kilele cha mlima Kilimanjaro kushajihisha sherehe za miaka 60 ya uhuru.

    Kundi la watu 150 likiongozwa na askari wa jeshi la wananchi wa Tanzania wanatarajia kuisimika bendera ya Tanzania kwenye kilele cha mlima kilimanjaro ikiwa ni sehemu ya shamrashara za maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru.

    Kwa mara ya kwanza bendera hii ya Tanganyika ilipandishwa na disemba 9 mwaka 1961 wakati wa sherehe za uhuru, utamaduni ambao umedumu mpaka leo.

  8. Zaidi ya 100 wauawa katika mapigano ya Darfur Magharibi mwa Sudan

    Zaidi ya watu 100 wameuawa kufuatia mapigano ya kikabila katika jimbo la Dafur Magharibi nchini Sudan.

    Mapigano kati ya Waarabu na wapiganaji wa Kiafrika kutoka jamii ya Masalit inayoungwa mkono na waasi wa zamano yamekuwa yakiendelea kwa siku kadhaa sasa.

    Mapigano katika eneo la Kreinik yamesababisha maelfu ya watu kutoroka makwao, wengine wakivuka mpaka na kuingia nchi jirani ya Chad, tUmoja wa Mataifa unasema.

    Mmoja wa manusura wa ghasia hizo anasema wanaume waliyojihami walishambulia vijiji vyao magharibi mwa Kreinik, na kuanza kupiga risasi kabla ya kuchoma moto nyumba zao.

    Pia waliweka vizuizi katika barabara kuu kuwazuia watu kutoroka.

    Waliyojeruhiwa hawana njia ya kupata matibabu ya dharura.

    Mapigano mapya ya kikabila yalianza Jumapili kati ya jamii hizo mbili, karibu watu 55 wameuawa.

    Miili zaidi ilipatikana msituni na kuongeza idadi ya vifo hadi zaidi ya 100. Makumi ya wengine hawajulikani waliko.

    Mwezi uliopita, watu 43 waliuawa katika sehemu tofauti ya Darfur Magharibi.

    Mapigano ya kikabila pia yameripotiwa kusini mwa eneo hilo lenye machafuko.

    Serikali imetuma kikosi cha pamoja cha vitengo vya kijeshi, jeshi na polisi huko Darfur Magharibi na Kusini ili kujaribu kuzuia ghasia.

  9. Ethiopia yakanusha kuwakamata maelfu ya watu

    Serikali ya Ethiopia imekanusha madai ya mataifa ya Magharibi kwamba imewakamata maelfu ya watu kwa misingi ya makabila yao hata kama Marekani ilionya kuwa inaweza kuwawekea vikwazo wale wanaochochea vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

    Waziri wa Habari (Billene Seyoum) amekiri kwamba mamia ya watu wamekamatwa tangu nchi hiyo ilipotangaza hali ya hatari mwezi uliopita lakini amekanusha kuwa madai kuwa kuwekwa kwao kizuizini kulikuwa na msukumo wa kikabila.

    Haya yanajiri huku serikali ikiendelea kurejesha maeneo zaidi yanayoshikiliwa na waasi katika maeneo ya Afar na Amhara.

    Serikali ya Ethiopia imesema kuwa watu waliokamatwa tangu mwanzoni mwa mwezi uliopita wamehojiwa na wengine kuachiliwa baada ya uchunguzi.

    Lakini ilikanusha madai kwamba vizuizi hivyo vililenga watu wa kabila la Tigrayan.

    Msemaji wa Waziri Mkuu Abiy Ahmed alisema madai ya Marekani, Uingereza na mataifa mengine ya magharibi ni sehemu ya taarifa potofu na shinikizo zisizofaa za kimataifa dhidi ya serikali.

    Lakini huko Marekani, wizara ya mambo ya nje wa Marekani ilipunguza maradufu madai hayo na kuitaka serikali kukomesha mara moja kukamatwa kwa watu hao.

    Wakati huo huo Umoja wa Mataifa na serikali ya Ethiopia wamebadilishana shutuma juu ya ufikiaji wa kibinadamu katika maeneo yenye migogoro kaskazini mwa nchi.

    Serikali inasema kuwa ilipeleka msaada wa chakula kwa watu milioni mbili tangu kukomboa miji na majiji kutoka kwa TPLF siku kadhaa zilizopita.

    Lakini Umoja wa Mataifa umesisitiza kuwa mafanikio haba katika upatikanaji na utoaji yamekuwa yakirudi nyuma haraka tangu mashambulizi ya waasi na mashambulizi ya serikali kuanza mwezi Oktoba.

    Takriban watu milioni 4 wamekimbia makazi yao kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa mwaka mzima.

  10. Zaidi ya watu 20 wachomwa moto wakiwa kwenye basi, Nigeria

    Takriban abiria 21, wakiwemo watoto, waliteketea moto hadi kufa wakati basi lao lilipovamiwa na watu wenye silaha katika jimbo la Sokoto, kaskazini-magharibi mwa Nigeria, polisi walisema.

    Walikuwa wakisafiri kutoka mji wa Sabon Birni hadi mji wa Isa karibu na mpaka na Niger.

    Msemaji wa polisi Sanusi Abubakar aliiambia BBC kwamba wengine kadhaa wanapata matibabu hospitalini kutokana na majeraha ya moto.

    Baadhi ya ripoti zinaonesha kuwa idadi ya waliouawa ni karibu 30.

    Mmoja wa waliohusika katika kuwasaidia majeruhi alielezea tukio hilo kuwa la "kuogofya" na kwamba wengi wa waathiriwa walishambuliwa kiasi cha kutotambulika.

    Shambulio hilo lilitokea Jumatatu jioni lakini taarifa zimepatikana kwa kuchelewa kutokana na huduma duni za mawasiliano katika eneo hilo.

    Baadhi ya ripoti zinasema washambuliaji walichoma gari hilo kwa maksudi na kuwachoma watu waliokuwa ndani huku akaunti nyingine ikionesha moto huo uliwashwa kwenye basi hilo kutokana na milio ya risasi ya washambuliaji.

    Polisi wanasema wanachunguza mazingira ya shambulio hilo.

    Kuwachoma abiria wakiwa hai ndani ya gari lao na watu wenye silaha si jambo la kawaida katika eneo hilo.

    Ni mbinu ambayo kwa kawaida hutumika na kundi la wanamgambo la Boko Haram ambalo huendesha shughuli zake zaidi kaskazini mashariki mwa Nigeria.

  11. Wahadhiri wanne Morocco washtakiwa kwa kesi ya ngono

    Wahadhiri wanne wa vyuo vikuu nchini Morocco wamefikishwa mahakamani wakishutumiwa kwa kuwapa wanafunzi alama bora zaidi ili wafanye ngono.

    Wanashtakiwa kwa unyanyasaji wa kingono, ubaguzi wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya wanawake.

    Mhadhiri wa tano atafikishwa kortini Jumatano kwa tuhuma za unyanyasaji.

    Kashfa hiyo inayohusu Chuo Kikuu cha Kwanza cha Hassan katika jiji la Settat, ni kisa cha hivi karibuni katika mfululizo wa madai ya unyanyasaji wa kijinsia katika vyuo vikuu vya Morocco katika miaka ya hivi karibuni.

    Ingawa wengi hawajahudhuria kesi hiyo.

  12. Kombe la Mataifa ya Afrika: Caf yakanusha uvumi kwamba michuano hiyo inaweza kuhamishwa

    Shirikisho la Soka barani Afrika (Caf) limekanusha uvumi kwamba Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) mwezi ujao linaweza kuondolewa kutoka Cameroon kufuatia ugunduzi wa hivi majuzi wa aina mpya ya Omicron ya Covid-19.

    Aina hiyo mpya ya virusi vya corona imesababisha vikwazo vya usafiri kuanzishwa na baadhi ya nchi kwa mataifa kadhaa ya Afrika, huku Nigeria, ambayo jirani na Cameroon, ndiyo ya hivi punde zaidi kuongezwa kwenye 'orodha nyekundu' ya Uingereza.

    Katika siku za hivi karibuni, baadhi ya mashirika ya vyombo vya habari yamependekeza tarehe za mchuano huo wa timu 24 zinaweza kubadilika au hata eneo kuhamishwa,na kupelekwa Qatar.

    Mkurugenzi wa mawasiliano wa Caf Alex Siewe anasema sio shirikisho wala maafisa wakuu wa Cameroon ambao wamejadili matukio kama hayo. "Hatuwezi kuendelea kutumia muda kushughulika na uvumi," aliambia BBC Sport Africa.

    "Hatukupokea ujumbe au taarifa nyingine yoyote kutoka kwa viongozi wetu - hakuna kitu kama hicho cha kubadilisha tarehe au nchi. Hatukujadili mambo kama hayo wakati wa mikutano yetu yote iliyopita."

    "Tuko kwenye tovuti. Tunafanya kazi." Michuano ya barani Afrika, ambayo tayari yamecheleweshwa kwa sababu ya janga la corona, yanatarajiwa kuanza Januari 9 huko Yaounde na kumalizika mnamo 6 Februari.

    Wafanyakazi wa Caf waliwasili Cameroon wiki hii kuandaa fainali za Afcon. "Ujumbe rasmi kutoka Caf umetolewa na katibu mkuu Veron Mosengo-Omba anajiunga nasi baada ya siku mbili," aliongeza.

    Chama cha Vilabu vya Ulaya, chombo huru kinachowakilisha vilabu Ulaya, kimeelezea "wasiwasi wake mkubwa" kuhusu ustawi wa wachezaji kabla ya mashindano, na kuongeza kuwa hali ya afya ya umma "inaendelea kuzorota kwa njia ya kutisha".

  13. Watoto 14 wagongwa na lori Nigeria

    Wanafunzi wawili nchini Nigeria wamekufa katika ajali ya gari huku wengine 12 wakiwa wamejeruhiwa wakati lori lilipowavamia siku ya Jumanne, polisi wamesema.

    Inasemekana kuwa lori hilo lilikuwa na shida ya breki na hivyo dereva akapoteza udhibiti wa gari hilo.

    Walioshuhudia tukio hilo wameiambia BBC kwamba watoto hao walikuwa wakirejea kutoka shuleni na waligongwa wakati wakivuka barabara.

    Tukio hilo lilitokea alasiri wakati ambao shule zilikuwa zimemaliza muda wake wa masomo.

    Taarifa zinaeleza kuwa dereva alijaribu kutoroka baada ya kuwagonga watoto hao, lakini alikimbizwa na kukamatwa.

    Tukio hilo lilizua ghasia katika eneo hilo huku wanafunzi wengine waliokasirishwa wakianza kuwashambulia madereva wengine na kuharibu magari.

    Kisa hicho kinajiri siku tatu baada ya watoto wanane kupatikana wakiwa wamefariki wakiwa wamefungiwa ndani ya gari katika sehemu nyingine ya jiji la Lagos.

  14. Biden amuonya Putin huku kukiwa na hofu ya uvamizi wa Ukraine

    Marekani imesema inajitayarisha na "majibu makali" kutokana na hofu ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, baada ya mazungumzo ya Rais Biden na Vladimir Putin.

    Katika video, Bw Biden alionesha wasiwasi mkubwa juu ya kuongezeka kwa wanajeshi wa Urusi na kutishia "hatua kali za kiuchumi na zingine", Washington ilisema.

    Urusi yasema haitaishambulia Ukraine.

    Bw Putin alishutumu Kyiv kwa uchochezi, na akataka hakikisho dhidi ya upanuzi wa Nato wa mashariki na kupelekwa kwa silaha za kukera karibu na Urusi.

    Walizungumza kwenye kiunga salama cha video kilichowekwa chini ya tawala zilizopita lakini hazikuwahi kutumika hapo awali, shirika la habari la Urusi Tass lilisema.

    Picha za video za matukio ya ufunguzi zilionesha salamu za kirafiki kati ya viongozi wa Marekani na Urusi.

    Mazungumzo hayo yakaendelea nyuma ya milango iliyofungwa, iliyochukua muda wa saa mbili.

    Bw Putin alifanya mazungumzo hayo kutoka katika makazi yake katika eneo la mapumziko la kusini la Sochi, kulingana na Tass.

  15. Habari...karibu katika matangazo ya moja kwa moja ya BBC Swahili leo ikiwa tarehe 08/12/2021