Jaji Kiongozi
Mustapha Siyani amejiondoa kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi Tanzania inayomkabili
Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na
mwenzake watatu.
Huyo ni jaji wa
pili kujiondoa katika kesi hiyo inayomkabili kiongozi huyo mkubwa wa upinzani
nchini humo, baada ya mapema mwezi uliopita Jaji Elinaza Luvanda naye kujitoa baada
ya mshtakiwa namba Nne, Mbowe kwa niaba ya wenzake kusema hawana imani nae.
Uamuzi wa kujiondoa Jaji Siyani
kusikiliza kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 16/2021, kunahusishwa na kuteuliwa
kwake na Rais Samia Suluhu kuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
uteuzi uliotangazwa Oktoba 8, 2021.
Katika uamuzi
wake leo oktoba 20, 2021 Mahakamani hapo, Jaji Siyani amesema sababu ya kujitoa
kusikiliza kesi hiyo kunatokana na majukumu aliyoyanayo
ambayo ameona yanaweza kumfanya ashindwe kuendesha kesi kwa haraka.
Wakati huo huo Mahakama hiyo Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa
na Uhujumu Uchumi imetupilia mbali pingamizi la kwanza lililowekwa kuhusu maelezo
ya mshtakiwa wa pili Adamu Hassan Kasekwa yaliandikwa nje ya muda.
Mahakama hiyo imekataa hoja ya pili kuwa Adamu Kasekwa aliteswa
kwani hakutatolewa ushahidi huo. Hivyo maelezo yalitolewa na mshtakiwa wa pili
kwa ridhaa yake.
Kama ilivyoripotiwa na mtandao wa gazeti la Mwananchi nchini
Tanzania, uamuzi huo umetolewa katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi
inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu.
Akisoma uamuzi huo Jaji Mustapha Siyani ameeleza kuwa
anakubaliana na Jamhuri kuwa mazingira yaliyokuwepo yana mantiki kuwa walikuwa
wakiendelea na upelelezi.
Freeman Mbowe na
wenzake watatu wanakabiliwa na mashtaka sita yakiwemo ya kula njama na
kufadhili fedha kwa ajili ya vitendo vya kigaidi.