Lavrov: 'Urusi sio safi sana kama pamba, na hatuoni haya kujionyesha sisi ni kina nani'

w

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Sergei Lavrov
Iliyochapishwa

Tangu jeshi la Urusi liliposhambulia Ukraine karibu miezi minne iliyopita, maelfu ya raia wameuawa na miji mizima kuwa vifusi, huku mamilioni ya raia wa Ukraine wakikimbia makazi yao.

Lakini siku ya Alhamisi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov alinitazama machoni na kuniambia mambo sivyo yalivyoonekana.

"Hatukuivamia Ukraine," alidai.

"Tulitangaza operesheni maalum ya kijeshi kwa sababu hatukuwa na njia nyingine kabisa ya kueleza nchi za Magharibi kwamba kuiburuza Ukraine katika Nato ni kitendo cha uhalifu."

"Tangu Urusi ilipoivamia Ukraine tarehe 24 Februari, Bw Lavrov ametoa mahojiano machache tu kwa vyombo vya habari vya Magharibi."

Alirudia tamko rasmi la Kremlin kwamba kulikuwa na Wanazi huko Ukraine.

"Maafisa wa Urusi mara nyingi hudai kwamba jeshi lao "linaondoa Wanazi waliopo" nchini humo.

Bw Lavrov alizua taharuki hivi majuzi alipojaribu kuhalalisha porojo za Wanazi kuhusu rais wa Ukraine ambaye ni Myahudi kwa kutoa madai ya kejeli kwamba Adolf Hitler alikuwa na "damu ya Kiyahudi."

Nilimnukulia ripoti rasmi ya Umoja wa Mataifa kuhusu kijiji cha Yahidne cha Ukraine, katika mkoa wa Chernihiv, ambayo inasema kwamba "Wakazi 360, wakiwemo watoto 74 na watu watano wenye ulemavu, walilazimishwa na jeshi la Urusi kukaa kwa siku 28 kwenye chumba cha chini cha ardhi ya shule… Hakukuwa na vyoo, maji…wazee 10 walikufa".

"Je, huko ndiko kupigana na Wanazi?," Niliuliza.

"Inasikitisha sana," Bw Lavrov alisema, "lakini wanadiplomasia wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na wawakilishi wengine wa Umoja wa Mataifa, wanawekwa chini ya shinikizo na Magharibi. Na mara nyingi sana wao wanatumiwa kukuza habari za uwongo zinazoenezwa na nchi za Magharibi."

"Urusi sio safi sana kama pamba. Urusi ndivyo ilivyo. Na hatuoni haya kujionyesha sisi ni kina nani."

Sergei Lavrov (R) accused the BBC of not uncovering the truth of Ukrainian actions in areas held by Russian separatists since 2014
Maelezo ya picha, Sergei Lavrov (kulia) aliishutumu BBC kwa kutofichua ukweli wa vitendo vya Ukraine katika maeneo yanayoshikiliwa na waasi wa Urusi tangu 2014.

Bw Lavrov, mwenye umri wa miaka 72, ameiwakilisha Urusi katika jukwaa la kimataifa kwa miaka 18 iliyopita, lakini vikwazo vya Magharibi sasa vimewekewa yeye na binti yake.

Marekani imemshutumu kwa kufuata maelezo ya uongo kuhusu Ukraine kama mchokozi, na kuhusika moja kwa moja na uvamizi wa Urusi kama mjumbe wa Baraza lake la Usalama.

Kisha nikageukia uhusiano wa Urusi na Uingereza.

Iko kwenye orodha rasmi ya Urusi ya nchi zisizo na urafiki, na nilipendekeza kwamba kusema mahusiano yalikuwa mabaya ilikuwa ni ujinga.

Sidhani kama kuna nafasi ya kufanya ujanja tena," Bw Lavrov aliniambia, "kwa sababu wote [Waziri Mkuu Boris] Johnson na [Liz] Truss wanasema wazi kwamba tunapaswa kuishinda Urusi, tunapaswa kuilazimisha Urusi ipige magoti. Endelea, basi, fanya hivyo!".

Ilikuwa mwezi uliopita ambapo waziri wa mambo ya nje wa Uingereza alisema Vladimir Putin wa Urusi anajidhalilisha katika jukwaa la dunia na kwamba "lazima tuhakikishe anakabiliwa na kushindwa nchini Ukraine".

Nilipomuuliza Bw Lavrov jinsi anavyoiona Uingereza sasa, alisema "kwa mara nyingine tena inabinya maslahi ya watu wake kwa ajili ya malengo ya kisiasa".

Nilimuuliza kuhusu wanaume wawili wa Uingereza waliohukumiwa kifo hivi majuzi na waasi wa Urusi waliojitenga mashariki mwa Ukraine.

Niliposema kwamba katika macho ya nchi za Magharibi, ni Urusi iliyohusika na hatima yao, alijibu: "Sipendezwi na macho ya Magharibi hata kidogo. Ninavutiwa tu na sheria za kimataifa. Kulingana na sheria kimataifa, mamluki hawatambuliwi kama wapiganaji."

Nilijibu kwamba watu hao walikuwa wamehudumu katika jeshi la Ukraine na hawakuwa mamluki, na Bw Lavrov alisema hilo linapaswa kuamuliwa na mahakama.

Kisha aliishutumu BBC kwa kutofichua ukweli wa kile kilichokuwa kikitokea kwa raia katika maeneo yanayoshikiliwa na watu wanaotaka kujitenga mashariki mwa Ukraine, "wakati raia walipokuwa wakipigwa mabomu na wanajeshi wa Kyiv kwa miaka minane".

Nilisisitiza kwamba katika kipindi cha miaka sita, BBC mara nyingi iliwasiliana na uongozi katika maeneo yanayosimamiwa na wanaotaka kujitenga wakiomba ruhusa ya kwenda kuona kinachoendelea.

Tulikataliwa kuingia kila mara.

Urusi imeishutumu Ukraine kwa mauaji ya halaiki.

Hata hivyo, mwaka wa 2021, raia wanane waliuawa katika maeneo yanayoshikiliwa na waasi, kulingana na waliojiita "viongozi" wa Urusi, na saba mwaka uliopita.

Ingawa kila kifo kilikuwa msiba, nilisema, hiyo haikusababisha mauaji ya halaiki.

Nilipendekeza kwamba ikiwa kweli mauaji ya halaiki yangetokea, basi wafuasi wa Luhansk na Donetsk wangependezwa na sisi kwenda huko.

Kwa nini hatukuruhusiwa kuingia, niliuliza.

"Sijui," alisema Bw Lavrov.

line

Unaweza pia kusoma

line