Narva: Mji wa mpaka wa Estonia ambapo Nato na EU hukutana na Urusi

Chanzo cha picha, BBC
Narva ni mahali pa kushangaza, Pembezoni kabisa mwa mwambao wa mashariki wa Nato, ni jiji la tatu kwa ukubwa katika Estonia - lakini wakazi wake ambao ni karibu 60,000, 97% wanaozungumza Kirusi na kuifanya kuwa jiji kubwa zaidi linalozungumza Kirusi katika EU.
Ipo kwenye ukingo wa magharibi wa Mto Narva ambao unapita kwenye Bahari ya Baltic. Kwenye ukingo wa mashariki ni Urusi. Kwa mgeni wa mara ya kwanza anahisi kama mipaka ya Vita Baridi. Ngome mbili kubwa zinatazamana kwenye pande zinazopingana za mto, na mpaka wa kimataifa ukipita katikati.
Upande wa magharibi ni Ngome ya Narva, iliyojengwa na wavamizi wa Wadenmark Karne ya 13. Upande wa mashariki ni Ngome ya Ivangorod, iliyojengwa na mfalme wa Muscovite Grand mwaka 1492.
Kwa kuwa sehemu kubwa ya mpaka wa Estonia na Urusi huvuka ziwa, uvamizi wowote wa siku zijazo wa Moscow unafikiriwa kuwa unaweza kuja hapa au zaidi kusini, karibu na Latvia.

Kupitia mto huko Narva kuna barabara yenye daraja, lililozungukwa na uzio wa juu wa waya wenye miiba na nguzo za kutengenzwa mwishoni. Hapa napanga kukutana na Erik Liiva. Yeye ni msimamizi wa polisi wa mpakani au ili kumpa cheo chake cha Kiestonia, yeye ni kamishna. Mrefu, mwenye ndevu akiwa na silaha, ananisindikiza chini ya barabara ambapo mstari mmoja mwekundu umepakwa rangi kuvuka barabara.
"Sasa umefika mpaka," ananiambia. "Unagusa mpaka wa Urusi."
Kwa hivyo uhusiano upoje na wenzako wa upande wa Urusi tangu uvamizi wa Ukraine uanze?, nauliza.
"Hatuna mawasiliano mengi nao," Liiva anajibu, "lakini tuna nambari ya simu kwa sababu za kiutendaji. Tumeimarisha doria zetu za mpakani, tunafanya ukaguzi wa kina zaidi kwenye magari yanayopita."

Ni kupitia kituo hiki cha mpakani kilichojificha, wanasema polisi wa mpaka wa Estonia, ambapo maelfu ya Waukraine wamekuwa wakitiririka, wengi wamekimbia mambo ya kutisha yanayoendelea Mariupol na maeneo mengine ya vita. Hadi watu 300 kwa siku wamekuwa wakivuka kuingia Estonia, wengi wao wakihamia nchi nyingine au kurudi Ukraine.
Katika baa mjini nakutana na Katri Raik, meya Narva aliyeteuliwa hivi karibuni.
"Ukraine ni vita vyetu," anasema. "Tunapata hisia tukiwa hapa."
Wakati uvamizi ulipoanza, anasema, kulikuwa na ukimya wa wasiwasi katika jiji, hakuna mtu aliyezungumza kuhusu hilo. 47% tu ya watu hapa ni Waestonia, 36% ni Warusi na wengine wote wameorodheshwa kama "wageni" watu wasio na utaifa, wengi wao wakiwa wanazungumza Kirusi.
Kabla ya uvamizi huo, watu walitazama programu za Kirusi kwenye TV na walivuka mara kwa mara hadi Ivangorod na zaidi hadi St Petersburg, ambapo ni karibu na Narva kuliko Tallinn, mji mkuu wa Estonia.
Lakini sasa balozi husika huko Narva na St Petersburg zimefunga, visa ni vigumu kupatikana na Estonia imepiga marufuku programu za TV za Kirusi kwa kuwa zinachukuliwa kuwa propaganda za Kremlin.
Katri Raik, meya, amekutana na watu wengi wa Ukraini wanaopitia katika mji wake.
"Wamepitia kwenye giza," anasema. "Ni kama mwanga katika macho yao umezimika."
Katika sehemu nyingine ya mji, ninatembelea mojawapo ya vituo sita vya usaidizi wa kujitolea vilivyoanzishwa ili kuwasaidia Waukraine wanaoingia. Inawafanyakazi vijana zaidi wa Urusi na Waukraine wanaofanya kazi bila malipo yoyote kama vile Katya, kutoka Urusi.
"Mpaka huu ndio ufaao zaidi barani Ulaya kwa Waukraine kuvuka ," ananiambia. "Baadhi yao wamehamishwa kutoka maeneo ya vita na wanajeshi wa Urusi, wengine kwa hiari, wengine kwa lazima. Wanapofika mpakani wanakuwa wamechoka na wana kiwewe."

Katika kituo cha mpaka cha Urusi huko Ivangorod, Waukraine wanahojiwa kwa muda mrefu haswa wanaume. Maafisa wa usalama kutoka idara ya usalama ya FSB inayoogopwa nchini Urusi huchunguza simu zao ili kuona picha, machapisho kwenye mitandao ya kijamii na nambari za mawasiliano, kuangalia tatoo za uzalendo au mashirika ya kijeshi.
Wanaanagalia hata michubuko ya bega inayosababishwa na kurusha silaha. Mahojiano hayo yanaweza kudumu kwa saa nyingi na yeyote anayeibua tuhuma anashikiliwa kwa uchunguzi zaidi.
Bado baadhi ya wale ambao wamefika upande wa Estonia wanakosoa Magharibi. Katika kituo cha kujitolea, wanawake wawili wazee wa Kiukreni kutoka kijiji karibu na Kharkiv hatimaye walikubali kuzungumza kwa Kirusi kama Katya anavyotafsiri. Wanasema wanashukuru kwa wanajeshi wa Urusi waliosaidia kuwahamisha hadi Belgorod upande wa mpaka wa Urusi.

Unamlaumu nani kwa vita hivi, nawauliza.
"Ni kama talaka," anajibu Viktoria, akimpandisha mbwa mdogo kwenye mapaja yake. "Kwa sababu pande zote mbili zina lawama. Marekani ina makosa kwani haikupaswa kutoa silaha kwa Ukraine."
Na vipi ikiwa Ukraine itaishia kugawanywa katika kanda zinazotawaliwa na Urusi kwa upande mmoja na serikali halali ya Kyiv kwa upande mwingine? Ungechagua kuishi wapi?
"Zelensky hapaswi kuwa rais, yeye ni mraibu wa dawa za kulevya," anajibu rafiki wa Viktoria, akirejea mstari wa chama uliowekwa na Kremlin.
"Tungeenda kuishi katika eneo la Urusi, bila shaka."
Nje ya kituo, mfanyakazi mwingine wa kujitolea, Dennis, ananipeleka kando ili kunieleza.
"Ni jambo la umri," anasema. "Hata hapa Narva wazee wengi wanalaumu Nato na Magharibi kwa mgogoro huu. Vijana wanafikiri tofauti. Hata wale wanaojiita Warusi wana hasira na Putin kwa kusababisha fujo hii."
Estonia pamoja na majirani zake wa Baltic Latvia, Lithuania na Poland ina wasiwasi mkubwa juu ya nia ya baadaye ya Urusi baada ya uvamizi wa Ukraine.
"Ulaya na Nato zinakabiliwa na ukweli mpya kabisa" anasema Tuli Duneton, mkurugenzi wa kisiasa katika wizara ya ulinzi ya Estonia. "Shambulio [kutoka Urusi] haliwezi kutengwa tena."
Ili kuzuia matamanio yoyote ya Urusi kuvamia mataifa haya manne ya Baltic, Nato imeharakisha katika uimarishaji wa pwani yake ya mashariki - sehemu ya kile inachoita "Uwepo Ulioimarishwa wa Mbele".
Uingereza, ambayo inaongoza katika mataifa mbalimbali vya Nato yaliyopo nchini Estonia, imeongeza maradufu ukubwa wa kikosi chake nchini humo. Sasa kuna vifaru 28 vya Challenger 2, magari ya kivita 95 na silaha 12 za mizinga ya AS90.














