Elvira Nabiullina: Mwanamke mwenye uwezo mkubwa na mshauri wa Putin anayebashiri 'yajayo' kwa kutumia mavazi yake

Iliyochapishwa

Amekuwa mshirika wa Vladimir Putin kwa zaidi ya miaka 20.

Kutoka kwenye kabila la Tatar, kundi kubwa zaidi la jamii ya wachache nchini Urusi, Elvira Nabiullina sio tu anatambulika kwa uwezo wake wa kukariri mashairi ya kifaransa na kutokuwa na huruma wakati wa shida, lakini pia anatambulika kwa kuwa mwanamke wa kwanza kuongoza Benki Kuu ya Urusi.

Mshirika wa Putin tangu aingie madarakani mwaka wa 2000, kiongozi huyo wa Kremlin alimteua kuwa Waziri wake wa Maendeleo ya Uchumi na baadaye, aliposhinda muhula wake wa tatu, alimleta serikalini kama sehemu ya timu yake ya washauri.

Mabadiliko makubwa katika kazi yake yalikuja mnamo 2013 wakati Nabiullina alipokuwa rais wa Benki Kuu ya Urusi, moja ya taasisi muhimu zaidi nchini humo.

Katika miaka yote hii yote, Benki hiyo imekuwa ikikabiliana na majanga mengi, lakini kamwe sio makubwa kama hili la sasa: kuokoa uchumi kwenye vita.

Mwanamke mwenye maneno machache, mwenye ushawishi, Nabiullina anashikilia ufunguo wa sera ya fedha ya nchi hiyo.

Ndiyo sababu, ili kujaribu kupata mwelekeo wa uchumi, wawekezaji na wachambuzi wamekuwa wakitumia alama katika mavazi yake hasa bruki, skafu au pini ya urembo anazotumia katika mavazi yake.

Lugha ya ya vipini na skafu

"Ninaweka kitu katika kila ishara, lakini sitaki kuelezea," Nabiullina aliiambia televisheni ya Urusi miaka miwili iliyopita.

Wengine wanaamini kwamba wakati aanapovaa kipini cha urembo cha ndege, ilikuwa ni ishara kwamba ongezeko la kiwango cha riba lilikuwa linakuja; au alipovaa pini yenye rangi ya wingu la mvua, alidokeza kwamba alitaka kupunguza matarajio ya mfumuko wa bei.

Siku chache baada ya Urusi kuivamia Ukrainia mnamo Februari 24, "alionekana kwenye mikusanyiko ya watu akiwa amevalia nguo nyeusi, kana kwamba yuko katika maombolezo," anasema Olga Shamina, mhariri wa uchumi wa Idhaa ya BBC ya Urusi.

Pini hizo, anaeleza Shamina, ni moja ya vipengele vya mfumo mgumu wa mawasiliano ambao benki ya Urusi imeutengeneza ili wahusika wa soko la fedha waweze kuelewa "kinachotokea na nini cha kutarajia" kutoka Benki Kuu.

Kwa mfano, wakati masoko yalipoanguka Machi 2020 katikati ya janga la covid-19, "Nabiullina aliweka kipini cha urembo chenye umbo la glasi ya kuchezea: inaanguka, lakini inainuka kila wakati," mtaalam wa uchumi wa Urusi anasema.

Na mnamo Aprili mwaka huo, wakati kila mtu alikuwa kwenye karantini, alivaa kipini (brooch) chenye muonekano wa nyumba. Shida ni kwamba tangu wakati huo pini hizo zikawa na tafsiri ngumu zaidi akivaa pini zenye nembo ya: chui, upinde, mshale na alama zingine zisizoweza kuelezeka.

Tangu kuanza kwa vita ya Ukraine, Nabiullina hajaonekana hadharani akiwa amevaa pini zake zozote kama ilivyoeleka.

Baada ya takriban muongo mmoja katika uongozi wa benki kuu, "mwanamke mvaa vipini" hivi majuzi aliidhinishwa tena kuendelea kuongoza benki hiyo hadi 2027, kipindi ambacho kinaweza kumpa majaribu ya ujuzi wake wote katika kuinua uchumi unaotikiswa.

Anatambulika kama miongoni mwa wenye nguvu Urusi

Katika miaka yake ya uongozi wa Benki Kuu, Nabiullina alipata kutambuliwa kwa usimamizi wake na mashirika ya kimataifa kama vile Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), wafanyabiashara, wawekezaji, mabenki na wataalamu wa mikakati wa serikali ambao walimwona kama mtaalamu mwenye uwezo.

Kwa mfano, alisifiwa kati ya 2013 na 2017, alipoondoa leseni zaidi ya 300 za benki kutoka kwa mashirika ambayo yalionekana kuwa dhaifu au yaliyoendeshwa kwa njia isiyo ya kiungwana, ambayo yaliwakilisha theluthi moja ya taasisi za mikopo za Urusi.

Jukumu lake kubwa ni "kuilinda Kremlin"

Jambo muhimu zaidi ni kwamba mafanikio yake yanayotambulika kimataifa sivyo yanavyoonekana.

Kwa mfano wanaeleza kuwa baadhi ya benki zilizofungwa katika kampeni iliyoongozwa na Nabiullina (kama Bank Otkritie, B&N Bank na Promsvyazbank) ziliishia kufilisika na baadaye kuokolewa kwa fedha za umma.

Wanamkosoa pia kwa kukosekana kwa uwazi katika baadhi ya shughuli zinazoongozwa na benki na kupendelea kampuni kubwa ya mafuta ya Rosneft.

"Nabiullina aliokoa labda kampuni iliyokuwa karibu zaidi na Kremlin," Maximilian Hess, mtafiti katika Mpango wa Eurasia katika Taasisi ya Utafiti wa Sera za Kigeni, aliiambia Redio ya Kitaifa ya Umma ya Marekani (NPR).

Kwa mtazamo wake, ishara zinazoonekana kwamba Nabiullina amekuwa "mshiriki wa karibu wa Putin" tangu alipoingia madarakani.

Yeye sio tu aliharibu akiba ya Kirusi, lakini alifanya gharama ya uwekezaji kuwa juu zaidi. Benki Kuu ya Urusi inasema ina jukumu la kulinda uchumi na kudhibiti mfumuko wa bei kama ilivyo kwa benki kuu nyingi, lakini ukweli Nabiullina ana jukumu moja tu ambalo ni kuilinda Kremlin na serikali ya Kremlin," Hess alisema. .