Mzozo wa Ukraine: Video potofu za TikTok kuhusu vita ya Ukraine zinavyotazamwa na mamilioni ya watu

    • Author, Shayan Sardarizadeh
    • Nafasi, BBC Monitoring
  • Iliyochapishwa

TikTok imeibuka na kuwa moja ya mitandao ya video inayoongoza kwa usambazaji wa haraka wa video za upotoshaji kuhusu vita vya Ukraine ambazo zinafikia mamilioni ya watu.

Ukiwa na watumiaji zaidi ya watu bilioni moja - zaidi ya nusu yao wakiwa na umri wa chini ya miaka 30 - TikTok ndipo ambapo vijana wengi wamekuwa wakipata taarifa mpya kuhusu mzozo huo, huku jukwaa hilo likijitahidi kuzuia kusambaa kwa taarifa za kupotosha.

Hauhitaji kuzama sana ili kupata maudhui yenye shaka. Kulingana na uchunguzi wa NewsGuard, tovuti inayofuatilia taarifa potofu mtandaoni, watumiaji wapya wanaweza kupendekezewa maudhui ya upotoshaji kuhusu Ukraine ndani ya dakika 40 baada ya kujiunga na mtandao huo.

Wakati mitandao mengine kama vile Facebook, Instagram na Twitter imekuwa ikizianika video za uwongo au za kupotosha kuhusu vita, TikTok inaonekana kujaribu kufuata mkondo huo. Kampuni hiyo inasisitiza kuwa imeongeza juhudi zake za kukabiliana na habari potofu.

Hizi ni baadhi ya njia za kawaida za maudhui ya kupotosha ambazo BBC imezibaini kwenye jukwaa.

Urushaji wa taariza za mubashara

Tangu siku za mwanzo za vita, taarifa feki zinazorushwa mubashara zimepata idadi kubwa ya maoni kwenye TikTok.

Mtumiaji wa mtandao anakutana na video ya kusisimua ya mzozo ama tukio la zamani au mazoezi fulani ya kijeshi, inawekwa sauti ya kughushi ya mlipuko mkubwa au kurushiana risasi, na kuanza kuirusha moja kwa moja mubashara, na mara hadhira kubwa inapojinga na akaunti zao za mtandao huo, wataombwa kuchangia.

Akaunti moja kama hiyo ilikuwa imevutia maoni karibu milioni 30 kufikia katikati ya Machi. Urushaji wa moja kwa moja wa video ya akaunti hiyo hadi wakati huo isipokuwa tatu zilikuwa kvideo fupi zilizochukuliwa kutoka kwa video ya YouTube ya mafunzo ya zamani ya kijeshi ya Ukraine, ya kuanzia mwaka 2017.

Wakati fulani, sauti ghushi ya milio ya risasi ulipata umaarufu sana kiasi cha kutumika na kuonekana katika zaidi ya video 13,000.

"Inaonekana urushaji wa video za moja kwa moja za kutisha zinaonekana kufanyika kwa matumaini ya kupata pesa kupitia mfumo wa zawadi wa TikTok," anasema Abbie Richards, mtafiti huru ambaye hutengeneza video kuhusu athari za habari potofu.

Michezo ya Video

Vipande vya kusisimua vya michezo ya video ya kijeshi au picha zinazozalishwa na kompyuta (CGI) zimetumika mara kwa mara badala ya video halisi za vita.

Matukio kutoka kwa michezo ya video kama vile Arma 3 na Call of Duty zimezagaa TikTok. Mapigano bandia ya angani, ikiwa ni pamoja na picha zinazoonyesha ndege za kivita zikidunguliwa, zimeonekana kuwa maarufu sana.

Baadhi ya akaunti hujaribu kufanya kitendo hicho kionekane cha kweli zaidi na kutumia video fupi za filamu za vita au tamthilia.

Video moja, ambayo ilitazamwa zaidi ya mara milioni 24, inaonyesha mwanamume mmoja anaonekana kuangusha kitu kilicholipuka kwenye tanki. Ilichukuliwa kutoka kwa video ya mmcheso wa Airsoft - na kupakiwa kwenye mtadao wa YouTube mnamo Januari.

Urushaji wa moja kwa moja wa matukio ghushi, unaotazamwa na watumiaji milioni 2.3, unajumuisha picha za CGI za mashambulio ya makombora na imekuwa ikisambazwa kwenye mtandao huu tangu mwaka jana.

Video za zamani

Video za mizozo ya zamani hutumiwa katika mzozo mpya unaoendelea. BBC imeona video za vita vya Libya, Syria na Chechnya zikitumika kana kwamba zinaonyesha mzozo uliopo.

Video inayodaiwa kuonyesha mapigano makali kati ya vikosi vya Urusi na Ukraine nje ya jengo la ghorofa imesababisha kutazamwa na watu milioni 7.7.

Lakini picha hizo zilirekodiwa mwaka 2014 katika mji mkuu wa Chechnya, Grozny, wakati wa shambulio baya la kundi la wanajihadi wenye silaha. Habari za punde nukuu za moja kwa moja ziliiwekwa kwenye picha asili ili kuficha chanzo halisi.

Baadhi wamechapisha video za mzozo kati ya Urusi na Ukraine wa mwaka wa 2014, ambao unaweza kuchukuliwa kimakosa kwa kuhusisha mzozo wa sasa, au picha za mazoezi ya kijeshi au gwaride katika nchi zote hizi bili.

Na video ya kifaru chenye bendera ya Ukraine, kikipita kwa kwa kasi kwenye makazi ya watu- iliyotazamwa mara milioni nne - pia ni ya mzozo wa Urusi na Ukraine wa mwaka 2014.

Uwazi finyu

Kama ilivyo kwa Facebook na Instagram kupitia kampuni Meta, TikTok inashirikiana na wakaguzi wanaotazama taarifa za kweli, ingawa kwa kiwango kidogo. Lakini ingawa Facebook na Instagram zimekuwa zikiainisha maudhui ya uwongo na ya kupotosha kuhusu Ukraine kwenye majukwaa yao, kwenye TikTok hilo ni nadra.

Tofauti na baadhi ya wapinzani wake, TikTok haitoi uwazi au zana za uchanganuzi kwa wasomi, watafiti na waandishi wa habari, ambayo Bi Richards anasema wataalam wa habari potofu kama yeye wamekuwa "wakidai" kwa muda mrefu.

Msemaji wa TikTok aliiambia BBC: "Tunaendelea kukabiliana na vita vinavyoharibu Ukraine kwa kuongeza rasilimali za usalamaili kugundua vitisho vinavyoibuka na kuondoa habari potofu.

"Ili kuunga mkono juhudi zetu za kusaidia kuweka TikTok kuwa mtandao salama na halisi, tumeongeza nyenzo zaidi kwenye udhibiti wetu na ukaguzi wa ukweli wa maudhui katika mzozo wa Urusi na Ukraine, ikiwa ni pamoja na wataalamu wa lugha za ndani na ushirikiano na mashirika huru ya kuangalia ukweli."

Unaweza pia kutazama: