Waridi wa BBC: Kukatwa titi moja hakujaondoa thamani yangu ya kuitwa mwanamke

Chanzo cha picha, Mwende Mutiso
- Author, Anne Ngugi
- Nafasi, BBC Swahili
- Iliyochapishwa
Unapokutana na Mwende Mutiso, unaweza ukastaajabu tabasamu ambalo yuko nalo haswa utakaposikia simulizi ya kusikitisha ya maisha yake.
Alipokuwa na umri wa miaka 23, Musito aligundulika kuwa alikuwa na saratani katika titi lake mmoja.
"Nilipoelezwa kuwa nina saratani ya matiti, ilikuwa vigumu kuamini matokeo hayo. Mimi nilikuwa naona kuwa saratani ya matiti humpata wanawake walio na miaka 40 na kwenda juu, sasa itakuwaje msichana mdogo kupata ugonjwa wa namna hiyo? Ila hali hiyo ndio ilikuwa sababu ya kubadilisha mtazamo wa maisha yangu yote," anasema Mwende.
Alipata matokeo hayo mwaka 2016 , yeye na wazazi wake waliamua kupata maoni mengine kutoka hospitali nyingine ila vipimo vilionesha hivyohivyo kuwa ana saratani.
"Aina ya matibabu ambayo yalikuwa yanapendekezwa na wataalamu yailikuwa yanagharimu mamilioni ya fedha, kwa hivyo ilinilazimu nikatwe titi moja ili kupunguza kasi ya saratani kusambaa hadi maeneo mengine ya mwili," anasema Mwende.
Kubadilika kwa maisha ya Mwende

Chanzo cha picha, Mwende Mutiso
Anasema upasuaji huo ulibadilisha maisha yake lakini alipiga moyo konde na kuendelea na maisha yake, ingawa hatua ya kukatwa titi ilikuwa na changamoto zake hasa mtazamo wa jamii baada ya mwanamke kukatwa matiti kutokana na saratani.
"Bila shaka hatua ya kutolewa titi iliniathiri, ndio wakati nilikuwa naanza maisha, nilikuwa naona kama ni ndoto, na nilikuwa najiuliza nitawezaje kuishi na titi moja?
Je kama mwanamke, muonekano wangu utabadilika vipi! nguo zitanikaaje," Mwende anakumbuka miongoni ya maswali aliokuwa anajiuliza.
Na si hayo tu, mawazo ya kifo pia yalikuwa yakimuandama. Hii ni kutokana na dhana aliyokuwa nayo ya kwamba saratani ina maanisha kifo cha mapema.
Baada ya kugundulika kwa saratani, Mwende alisimamisha mipango aliyokuwa nayo ikiwemo masomo katika chuo kikuu, anasema kwamba ilibidi familia yake kuchagua matibabu kwanza kutokana na fedha nyingi zilizokuwa zinajihitajika kwa matibabu na dawa ili kukabiliana na saratani.
Aliishi bila titi moja na anasema kwamba alikuwa haoni changamoto kubwa kiasi cha kuwa tayari kuzungumzia hali yake hasa kwa wale waliokuwa wanashangaa muonekano wake baada ya upasuaji- amekuwa akivaa titi bandia hadi leo.
Mwaka 2019, miaka miwili baada ya saratani kugunduliwa alianza kuhisi maumivu kwenye kifua chake hasa kwenye kovu la titi lililokatwa.
Mwende anasema kuwa uvimbe mwingine ulianza katika eneo hilo. Alipotafuta matibabu tena, matokeo yalikuwa ya kusikitisha.
Yalionyesha kwamba ana saratani katika eneo hilo la titi lililokatwa na pia kusambaa hadi kwenye mapafu yake.

Chanzo cha picha, Mwende Mutiso
Mwanadada huyo anasema kwamba wakati anapewa matokeo hayo alikuwa ametimiza miaka 27.
"Nilipopewa matokeo ya kwamba nina saratani iliyoenea mno kifuani, daktari pia alinieleza kuwa huenda sitakuwa hai baada ya mwaka mmoja, ilikuwa ni siku moja kabla ya kusherehekea siku ya kuzaliwa kwangu, tarehe 8 Disemba, 2019. Miaka miwili baadaye bado niko hai," anasema Mwende.
Mwende anaonyesha ujasiri usiokuwa wa kawaida licha ya kutaarifiwa juu ya hatima ya uhai wake , taarifa ambazo zinaweza kumkatisha mtu tamaa ya kuishi, lakini kwake yeye anaona kila inayoitwa leo ni zawadi kwake kutoka kwa Mungu.
Japo kama binadamu alishtushwa na ujumbe wa daktari lakini haukumuathiri kwa muda mrefu.
"Nilipoelezwa kwamba saratani ilikuwa imerudi, nilishtuka ndio, lakini nilikubali hali yangu, mtazamo wangu wa maisha ulibadilika kabisa nikawa ninachukulia kuwa kila siku ni ya tabasamu kwangu. Nilianza kuthamini kila jambo ninalofanya," Mwende anakumbuka.
Sio ajabu kwamba mwanamke huyo alianza kufanya mambo ya kipekee, baada ya kujiunga na kikundi cha Kilele Health nchini Kenya kinacholeta pamoja walionusurika na saratani, na watu wanaochagua kuwa nguzo kwao.
Kupitia kikundi hiki mwanadada huyo ameweza kupanda Mt. Kenya na hivi karibuni Mlima Kilimanjaro nchini Tanzania.
Aidha, anaongezea kwamba kwa kupanda milima hiyo kunampa nguvu ya kukubali hali yake ya saratani na kutafuta mbinu za kuishi maisha yake anavyopenda yeye.
"Niliacha kujiuliza maswali mengi na kujihurumia wakati nilipokubali kwamba saratani ni sehemu ya maisha yangu. Nikakubali kuishi maisha tofauti kuanzia ni nani atakuwa karibu na mimi, nitazipa shughuli zipi kipaumbele na kadhalika. Hiyo imenirahisishia jinsi ya kuchuja majukumu muhimu maishani," anasema Mwende.
Akiwa na miaka 29 mwaka huu anatambua fika kwamba imekuwa ni safari yenye milima na mabonde.
Katika ulingo wa mapenzi, Mwende anasema kwamba wakati alipopatikana na saratani mara ya kwanza alikuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na mwanaume aliyemsaidia sana katika hali ya matibabu na pia kumpa moyo.
Ni uhusiano ambao ulikaa hadi mwaka 2020 ila kuachana kwao hakuhusiani na ugonjwa wa saratani. Mwende anaamini kwamba mwanamke ni zaidi ya matiti na hakuna kiungo cha mwili wake kimeshusha thamani ya yeye kujihisi kama mwanamke kamili.
Kuna ambao bado wakisikia sina titi moja, hushangaa na kunichukulia vingine, ila mimi huwa nachukua kila fursa kuelimisha jamii kuhusu saratani na jinsi inavyoweza kuwa wa msaada kwa wahanga kama mimi. Ndio sina titi moja ila naamini kwamba mimi ni mrembo sana," anasema Mwende.












