Kombe la Dunia 2022: 'Dabi ya Jollof' ,mahasimu wa Afrika Magharibi kusaka tiketi ya Qatar

Ghana ilimteua Otto Addo (kushoto) baada ya Kombe la Mataifa ya Afrika, huku Nigeria ikisalia na Augustine Eguavoen

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa

Ukitaja mchezo kati ya Nigeria v Ghana, kwa wengi yatakuja mambo mawili makubwa - ushindani wa wa hali ya juu kwenye soka na chakula kinachoitwa 'Jollof rice', ambacho ni chakula maarufu Afika. Kwa kifupi ni pilau la asili ama wali unaochanganwa na viungo mbalimbali ikiwemo nyanya, vitunguuu na pilipili ikipikwa pamoja na samaki ama nyama.

Wakati mjadala ukiendeleaa na kitendawili cha taifa gani ni bora kwenye kuandaa ''Jollof rice' nzuri kikiwa bado hakijateguliwa, hoja ya taifa gani kati ya hayo ni mbabe katika soka pengine inaweza kuamulia kwa sasa kupitia michezo miwili ya Machi 25 na 29.

Mataifa hayo mawili yatakutana mjini Kumasi tarehe 25 mwezi Machi kuwania nafasi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia, ikiwa ni tukio linaloadhimisha miaka 50 ya ushindani mkali wa soka Afrika Magharibi.

Timu hizo zinakutana kwa mara ya kwanza katika miaka 11 na kwa mara ya kwanza katika mechi ya kufuzu kuelekea Kombe la Dunia tangu 2001.

Siku nne baadaye, Nigeria itakuwa mwenyeji wa Black Stars mjini Abuja atakayeshinda katika mechi hizo kwa ujumla atafuzu fainali hizo za Qatar 2022.

Super Eagles wanajiandaa kufuzu kombe la dunia kwa mara ya nne mfululizo, na mara ya sita kwa ujumla, wakati Ghana ambayo imefuzu mara tatu wa kufuzu, wanataka kurejea katika fainali hizo baada ya kushindwa kufuzu fainali za mwaka 2018 nchini Urusi.

Ni ndugu wakubwa, wenye mafanikio kidogo

Kuna mechi chache sana ambazo zina athari za kitamaduni na kihisia ambazo zinaweza kuileza mechi hii kati ya Nigeria-Ghana.

Mataifa hayo mawili yalisimama bega kwa bega tena mstari wa mbele katika vita vya kupigania uhuru kutoka kwa utawala wa kikoloni katika miaka ya 1950, wakati Ghana ilikuwa na jamii kubwa ya wahamiaji nchini Nigeria hadi miaka ya 1980.

Kwa kigezo cha idadi kubwa ya watu iliyonayo, Nigeria - yenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika ya karibu milioni 200 - ni wazi kwamba ni nchi kubwa kuliko mpinzani wake.

Nigeria ilifungwa 1-0 na Tunisia katika mchezo wa mwisho wa Kombe la Mataifa ya Afrika 2021 nchini Cameroon.

Chanzo cha picha, Getty Images

Hata hivyo, kwa upande wa soka, Ghana imeipiku Nigeria kwa mafanikio: Ikitwaa kombe la mataifa ya Afrika mara 4, Nigeria mara 3, ikicheza robo fainali ya Kombe la Dunia (licha ya kushiriki mara chache ukilinganisha na Nigeria) na imeshinda michezo 21 dhidi ya 10 mataifa hayo yalipokutana katika mashindano mbalimbali.

Hata hivyo Ghana imeshinda zaidi katika kipindi cha miaka ya 70 na 80 ambapo Ghana ilikuwa inatawala soka la Afrika, lakini tangu ushindi wa 2-1 wa Black Stars mwaka 1992 dhidi ya Super Eagles katika nusu fainali ya Kombe la Mataifa, mambo yalianza kubadilika.

Tangu wakati huo, Nigeria ikapanda na kupata mafanikio katika soka la Afrika kati ya mwaka 1994 na 2013, na kuongeza taji lao la mwaka 1980 wakati Ghana - mabingwa mara nne wa Afrika - hawajashinda taji hilo tangu mwaka 1982, badala yake wamekuwa wakikaribia tu kufikia mafaniko ya kutwaa mataji katika kipindi cha miongo minne iliyopita.

Mchezo wa kuchezeana akili

Kabla ya mechi hiyo ya mchujo, Ghana ilichelewesha kutangazwa hadharani kwa kikosi chao hadi kufikia mwishoni mwa mwezi, ikitajwa kuwa "mkakati" uliobuniwa ili kuhujumu maandalizi ya kambi ya Nigeria.

"Na wamechanganyikiwa sana," mjumbe wa baraza kuu la Ghana FA (GFA) Sammy Anim Addo aliieleza BBC kabla ya kutangazwa kwa kikosi hicho mapema wiki hii.

"Hatuwezi kufanya kitu kile kile kila wakati na kwa mara ya kwanza huu ni mkakati na tunaamini. Tutaifunga Nigeria na kufuzu Qatar 2022."

Ghana ililazimika kuhamia uwanja wa Baba Yara huko Kumasi baada ya uwanja wa kuchezea katika uwanja wa Cape Coast kuharibika wakati wa sherehe za Siku ya Uhuru wa nchi hiyo tarehe 6 Machi.

Chanzo cha picha, Getty Images

Chini ya benchi jipya la ufundi, Otto Addo kama kocha na mchezaji wa zamani wa Tottenham, Chris Hughton akiwa mkurugenzi wa kiufundi, Ghana itaingia uwanjani mbele ya mashabiki wake wa Kumasi bila nahodha wake aliyesimamishwa kwa kadi Andre Ayew.

Nigeria pia itawakosa uwanjani nyota wake kadhaa, Alex Iwobi, kiungo wa kati wa Leicester City Wilfred Ndidi (majeruhi) huku ikitarajiwa kuwa na nyota wa Leicester, Ademola Lookman, aliyeukacha uraia wa England na kutua Nigeria.

Tangu kupangwa kwa droo ya michezo hii ya kufuzu kombe la dunia, kutoka ukanda wa Afrika, mashabiki wa Nigeria wameonekana kuwa na hamasa zaidi.

Inatokana na kufanya vibaya kwa Ghana katika fainali zilizopita za Afrika, Ghana akimaliza mkiani mwa kundi C, ikipoteza michezo miwili kati ya mitatu, ukiwemo dhidi ya 'vibonde' Caper Verde waliokuwa wanashiriki fainali hizo kwa mara ya kwanza.

Nigeria yenyewe ilishinda mechi zake zote 3 za makundi, kabla ya kutolewa kwenye hatua ya 16 bora kwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa Tunisia.

Mahasimu wa muda mrefu

Ushindani kati ya Ghana na Nigeria umekuwepo kwa muda mrefu.

Ghana ilikuwa taifa la kwanza la waafrika weusi kupata uhuru wake kutoka kwenye utawala wa kikoloni mwaka 1957 na Nigeria ilipata uhuru wake mwaka 1960. Wanigeria wengi wakihisi kwasababu taifa lao ni kubwa lilipaswa kupata uhuru wake kabla ya Ghana.

Ushindani ama uhasama kwenye soka ulianza tangu wakati huo nchi hizo zikipigania uhuru, huku Ghana ikishinda mechi za kwanza kwanza za kirafiki katika miaka ya 1950, ikiwa ni pamoja na ushindi wa 7-0 mwezi Juni 1955 dhidi ya Nigeria ambayo wakati huo ilikuwa ikiitwa 'Red Devils'.

Mvutano wa kisiasa ulianza baina ya mataifa hayo ya Afrika Magharibi baada ya agizo la serikali ya Ghana la mwaka 1969, kuamuru wageni wote wasio na vibali vya kuishi Ghana kuondoka.

Nigeria ilishinda taji lao la tatu la Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2013 kwa ushindi dhidi ya Burkina Faso

Chanzo cha picha, Getty Images

Ingawa kulikuwa na raia wengi kutoka Togo, Burkinafaso, Ivory Coast, Niger na mataifa mengine ya Magharibi waliokuwa wanaishi nchini humo, lakini idadi kuwa ya raia wa kigeni waliokuwa wanaishi Ghana wakati huo walikua ni Wanigeria - hasa wa kabila la Yoruba.

Baadhi yao walikuwa nchini humo kwa miaka mingi na walikuwa katika vizazi vyao vya pili na vya tatu, hivyo tangazo hilo halikuwapendeza Wanigeria - walihisi kana kwamba zoezi hilo ama tangazo hilo liliwalenga wao.

Mambo yalibadilika wakati mafuta yalipogundulika Nigeria na uchumi wa Ghana uliporomoka, ikimaanisha kuwa kuanzia mwaka 1974, kukawa na msururu wa raia wa Ghana waliokimbilia kwenda Nigeria kutafuta ajira.

Karibu muongo mmoja baadaye, biashara ya uchimbaji mafuta ulishuka kwa sababu ya soko la dunia na uchumi wa Nigeria ulishuka, hilo likasababisha serikali kuagiza zaidi ya wahamiaji milioni moja wa Afrika Magharibi, wengi wao wakiwa ni raia wa Ghana, kuondoka Nigeria haraka mwaka 1983.

Sababu kubwa ya kuwatimua wageni kwa mujibu wa Serikali ni kwamba wahamiaji wasio na vibali wa Afrika Magharibi walikuwa wakidaiwa kuchukua kazi kutoka kwa Wazawa wa Nigeria na kusababisha viwango vya juu vya uhalifu.

Matukio ya mwaka 1983 mara nyingi huongeza na hutawala mjadala wa mashabiki kutoka pande zote kabla ya nchi hizo kukutana uwanjani, na michezo ya wiki hii ijayo inaweza kusiwe na tofauti kubwa.