Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
‘’Ilinichukua miaka tisa kupata mimba sasa nimempoteza binti yangu’’: Uchungu wa wahanga wa mafuriko nchini Brazil
Mvua kubwa ilipoanza, Giselli Carvalho alirudi nyumbani haraka.
Alikuwa na wasiwasi kuhusu mama yake na binti yake mwenye umri wa mwaka 1, Helena.
Akiwa njiani, Giselli alikutana na jirani aliyempa habari zenye kuhuzunisha: nyumba ya familia yao ilikuwa imesambaratishwa na mojawapo ya maporomoko mengi ya ardhi yaliyokumba jiji la Brazili la Petrópolis mnamo Februari 15.
Siku hiyo ilinyesha katika jiji hilo milimita 259.8 katika muda wa saa 24, zaidi ya mvua ya kawaida kwa mwezi mzima, na kiasi kikubwa zaidi katika siku moja tangu rekodi zilipoanza mwaka wa 1932.
Gharika hiyo ilisababisha maporomoko ya ardhi yaliyoua zaidi ya watu 100, wakiwemo takriban watoto wanane, kulingana na Ulinzi wa Kitaifa wa Raia wa Brazili.
"Ilinichukua miaka tisa kupata ujauzito kwa sababu nilitaka kumlea binti yangu vyema," Giselli alikiambia kituo cha habari cha Brazil Globo TV.
"Niliweza kufurahia kuwa na mtoto wangu kwa zaidi ya mwaka mmoja tu," alilaumu.
"Naendelea kuwaza ni ndoto mbaya na nitaamka na kumuona Helena akiwa hapa kwangu," aliongeza huku akitokwa na machozi.
Wakati maporomoko ya ardhi yalipotokea, mpwa wa Giselli, María Carminante, pia alikuwa ndani ya nyumba hiyo, iliyoko Morro da Oficina favela, katika kitongoji cha Alto da Serra, mojawapo ya zilizoharibiwa zaidi na mvua.
Miili hiyo mitatu ilipatikana pamoja kwenye sofa.
Shughuli ya kutafuta miili iliendelea Alhamisi, kwa msaada wa majirani, timu kutoka Idara ya Zimamoto na Jeshi na Ulinzi wa Raia.
Kulingana na tovuti ya habari ya G1, pamoja na wafu ambao tayari wamepatikana hadi sasa, kumekuwa na rekodi ya watu 134 kutoweka katika eneo hilo.
Idadi ya vifo inatarajiwa kuongezeka huku mvua zaidi ikitabiriwa.
Giselli Carvalho sasa ni miongoni mwa mamia ya watu wasio na makazi ambao wapo kwenye makazi ya muda huko Petrópolis.
Mwanamke huyo alikuwa akitayarisha karamu kwa ajili ya siku ya kuzaliwa kwa binti yake yam waka wa pili yenye mada ya mhusika wa filamu ya Disney "Moana "
"Kila kitu kilikuwa tayari kwa sherehe. Sasa sijui nifanye nini," alisema huku akiwaonyesha waandishi wa habari video za siku ya kwanza ya Helena kwenye chumba cha watoto, siku chache kabla ya msiba.
- https://bbc.in/3p6p6zF
Kujirudia kwa msiba
"Sikupoteza mtu yeyote, lakini nilipoteza kila kitu."
Hivi ndivyo Carina Santiago, 41, anavyohitimisha maisha yake baada ya mvua kubwa kunyesha huko Petrópolis.
Carina ni mkazi mwingine wa Morro da Oficina.
Hadithi yake ni mfano wa kurejea kwa majanga yanayoweza kuzuilika.
Mnamo 1995, Carina alipoteza mama yake katika maporomoko ya ardhi katika eneo moja.
Zaidi ya miongo miwili baadaye, anaiambia BBC News Brazil kilichotokea Februari 15. "Ilikuwa siku ya kutisha, nilikuwa nimekwama kazini kwenye mtaa wa Teresa, ambao pia uliathirika."
"Mvua ilikuwa ikiongezeka, lakini hatukujua kungekuwa na huzuni nyingi, misiba mingi nanma hii."
Nyumba yake sasa haikaliki, lakini watoto wake watatu wenye umri wa miaka 19, 16 na 13 waliweza kujiokoa.
"Sehemu ya nyuma [ya nyumba] imeharibiwa, tumaini letu limetoweka. Watu wengi wanataka kurudi, bila kuelewa kuwa mtaa wetu umekwisha," anasema Natan Santiago Monteiro, mtoto wa kiume wa Carina.
"Nilikuwa dukani tukaona kijito kinapita, magogo yanapita, watu wanapita, lakini hatukujua tutapoteza kila kitu, tuna nguo zetu tu, sasa inabidi twende kanisani tukaishi hapo," alisema kijana huyo.
Carina anasimulia kwamba alipofiwa na mamake katika maporomoko ya ardhi yaliyopita, yeye pekee ndiye aliyepoteza nyumba yake.
Sasa, adokeza, kilichotokea ni kibaya zaidi kwa kuwa familia nyingi zimeathiriwa.
Ni mshtuko kikubwa sana. Wakati huo [alipofiwa na mama yake], nilikuwa na umri wa miaka 15, leo nina miaka 41 na naangalia kila kitu nilichofanyia kazi, vitu nilivyokuwa navyo, nimepoteza kila kitu, sina chochote.
"Nataka kumpa mtoto wangu mazishi ya heshima. Yeye ndiye kipenzi cha maisha yangu"
Huku kukiwa na vifusi na matope yaliyosalia kutokana na kuporomoka, mwanamume mmoja amekuwa akiutafuta mwili wa mwanawe kwa siku tatu.
Mtoto huyo mwenye umri wa miaka 18 alikuwa na nyanyake, ambaye pia hayupo chini ya kifusi, katika nyumba iliyo chini ya kilima, ambayo iliporomoka kutokana na mvua kubwa iliyonyesha.
"Nitaondoka hapa tu nitakapoipata," Paulo Roberto de Oliveira, 40, mshauri wa bunge, anamwambia mwandishi wa habari Rafael Barifouse wa BBC News Brazil.
Katikati ya msako huo, Paulo anaishi kwa hofu ya hasara ya watu wengine.
Anasema kuwa alikuta mguu wa binadamu ukiwa katikati ya tope, ambao uliteremka chini ya kilima pamoja na mabaki ya samani na vifaa ambavyo hapo awali vilikuwa vya babu na bibi, wazazi na watoto.
"Alizaliwa na kukulia huko Petrópolis," hii si mara ya kwanza kwa maisha yake kuathiriwa na athari za hali mbaya ya hewa katika jiji hilo.
Mnamo 2011, alipoteza nyumba yake kutokana na mvua kubwa iliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 900 katika nyanda za juu za Rio mwaka huo.
Wakati huo, familia yake yote iliachwa bila makao, na ilimbidi kwenda kwenye makazi ya muda.
"Ni sisi pekee ambao hatukupoteza maisha," Paulo aliambia BBC News Brazil, akiongeza kuwa mwaka wa 2011 nyumba 110 zilifungwa katika mtaa wake.
Ripoti ya mwaka 2017 iliyotolewa na mamlaka ya jiji ilikadiria kuwa karibu 20% ya eneo la Petrópolis "liko katika hatari kubwa ya maporomoko ya ardhi na mafuriko."
"Halmashauri ya Jiji inasubiri watu zaidi wafe ili kuchukua hatua," analalamika Paulo.
Alipoulizwa anapata wapi nguvu za kuwa huko, anajibu "Mungu pekee."
"Ni matumaini yangu kwamba nitampata mwanangu na kumzika kwa heshima. Yeye ndiye kipenzi cha maisha yangu," anasema.
"Mamlaka ziko wapi? "
Sueli Alcantara alipoteza wapwa watano, akiwemo mpwa wake mjamzito.
"Nilipoteza majirani zangu wote, upande wa kulia hakukuwa na nyumba hata moja," anasema Sueli.
Alikuwa nyumbani wakati mvua inaanza kunyesha.
Ilimbidi apande dirishani na kutafuta makazi upande wa pili wa kilima.
Sasa, wanashutumu mamlaka.
"Mamlaka za mitaa ziko wapi, Meya yuko wapi? Hakuna mtu hapa aliye na jembe la kutusaidia. Hawa watu wote wanatuomba kura wako wapi?"
Ukosoaji wa wakazi dhidi ya mamlaka umeenea
Huku nyumba zaidi ya 80 zikiwa zimeathirika huko Morro da Oficina, majirani wanaripoti kuwa, siku ya Jumatano, kulikuwa na maiti nyingi mahali hapo na walilazimika kutumia shuka kulinda mabaki ya watu kutokana na ukosefu wa plastiki ya kutosha.