Kwa nini gharama za Barabara kuu ya Nairobi Expressway zimeendelea kupanda?

Chanzo cha picha, KENHA
Gharama ya ujenzi wa Barabara ya Nairobi Expressway ya kilomita 27.1 iliyoanza mwishoni mwa 2020 imepanda hadi takriban $777.8 milioni, kutoka makadirio ya awali ya bajeti ya $576.9 milioni yaliyotolewa na Mamlaka ya Kitaifa ya Barabara Kuu ya Kenya (Kenha).
Kwa gharama ya $32.4 milioni kwa kilomita, mradi wa Nairobi Express way huneda ndio mradi wa gharama ya juu zaidi wa barabara Kenya na katika eneo hilo na gharama zinaendelea kupanda.
Zingatia hili, gharama ya ujenzi wa Barabara ya Expressway iliyoanza mwishoni mwa 2020 imepanda hadi Sh87.9 bilioni au takriban $777.8 milioni, kutoka kwa makadirio ya awali ya bajeti ya Sh65.2 au $576.9 milioni iliyotolewa na Mamlaka ya Kitaifa ya Barabara Kuu ya Kenya (Kenha).
Hii yenyewe ilikuwa juu kutoka kwa jumla ya gharama iliyopendekezwa ya shilingi bilioni 55 sawa na takriban dola milioni 550 wakati mradi ulipoanzishwa kwa mara ya kwanza.
Kwa hivyo kwa nini gharama hii inazidi kupanda kwa kasi?
Wataalamu wanahusisha kupanda kwa gharama, ambazo kwa sasa zimeongezeka kwa takriban 34% kwa mbali mbali .
Kwanza, ni kushuka kwa thamani ya shilingi ya Kenya dhidi ya dola. Mnamo mwaka wa 2020 wakati mradi huo ulipoanza, Dola ya Kimarekani ambayo ufadhili wa mradi huo ulitolewa ilinukuliwa kuwa shilingi 106.39 kabla ya kushuka hadi takriban 113.50 mapema 2022.

Chanzo cha picha, KENHA
David Nashon ni mchumi wa uchukuzi jijini Nairobi, anabainisha kuwa kushuka kwa kiwango chochote cha ubadilishaji wa dola huathiri gharama za mradi moja kwa moja.
'Vitu kama vile mafuta, saruji na chuma vyote vinaletwa sokoni kwa thamani ya dola, mabadiliko yoyote yatakuwa na athari ya moja kwa moja.' Anasema.
Gharama zingine zisizoonekana pia zinaweza kuchangia , huku bei za chuma na saruji zikipanda kwa kasi katika muda wa miezi 24 iliyopita kutokana na uhaba wa usambazaji na usafirishaji wa meli ulioletwa na janga la Covid 19.

Chanzo cha picha, KENHA
'Gharama za usafirishaji wa meli zimeongezeka kote ulimwenguni. Zimeongezeka kweli. Ukiangalia nyenzo nyingi zinazotumiwa, mara nyingi huagizwa kutoka nje. Huingia kupitia bandari ya Mombasa, na hivyo kuathiri gharama,' Nashon anaongeza.
Data kutoka Marketwatch inathibitisha madai yake, ikionyesha kuwa Tangu Machi 2020, bei za chuma zimepanda kwa 215% duniani kote. Katika hali nyingi gharama hizi hupitishwa kwa watumiaji kama inavyowezekana katika mfano wa Kenya.












