Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Rolex kubwa zaidi duniani ina uzito wa kilo 204.6 na urefu wa mita 2.32
Ikiwa unatatizika kufikiria jinsi hiyo inaweza kutoshea kwenye mkono wako basi sahau saa na ufikirie chakula cha mitaa ya hapa Afrika Mashariki.
Kama Waganda wanavyojulikana kusema: "Hatuvai Rolex, tunakula." Rolex - vitafunio - ni "mayai yaliyoviringwa ".
Mlo huo maarufu, unaopatikana katika vibanda vya barabarani kote nchini Uganda, umetengenezwa kutoka kwa omeleti ya mboga na kuongezwa nyanya kisha kufungwa kwenye chapati.
Tayari umepata sifa zaidi nchini Uganda na hivi majuzi rekodi za Guinness World Records ziliidhinisha rolex kubwa zaidi duniani.
Viungo vilivyotumiwa kwenye rolex hiyo nzito ni pamoja na mayai 1,200, kilo 90 za mboga (vitunguu, nyanya, kabichi, karoti na pilipili), kilo 72kg za unga na kilo 40 za mafuta ya kupikia.
Iliwachukua timu ya watu 60 kuutayarisha mlo huu.
Raymond Kahuma ambaye ni mtumiaji wa YouTube nchini Uganda aliwakusanya wapishi na waokaji ambao walitumia saa 14 kuchanganya, kukanda, kukata na kukaanga viungo hivyo katika jiko la nje mashariki mwa mji mkuu Kampala.
"Raymond na timu yake walikuwa wakifanya kazi kwa miezi kadhaa katika utayarishaji wa rekodi hiyo ili kuhakikisha kila kitu kingekwenda sawa," Guinness World Records ilisema.
Jaribio kama hilo la kuweka rekodi mwaka 2020 liliporomoka baada ya gharama kukadiriwa kuwa dola 3,000.
Inaaminika kuwa chakuka hiki kitamu cha rolex kilienezwa kwa mara ya kwanza na mchuuzi wa chakula ambaye aliwauzia wanafunzi kwenye Chuo Kikuu cha Makerere mjini Kampala. Kisha umaarufu wake ukaenea katika miji mingine.
Vitafunio hivi sasa vinachukuliwa na Waganda kama chakula cha haraka kinachopendwa zaidi katika nchi ambayo nafasi za maegesho na kando ya barabara mara kwa mara hubadilishwa kuwa maduka ya chakula wakati wa jioni.
Kuonekana kwa watu waliojazana kuzunguka majiko ya mkaa wakiwa kwenye viti vya mbao, wakipiga soga huku wakisubiri oda zao za rolex kutayarishwa ni kawaida.
Aaron Odeke aliingia katika biashara ya rolex muongo mmoja uliopita akiwa na umri wa miaka 12 tu baada ya kukosa kupata kazi nyingine.
Duka lake ni miongoni mwa safu za wachuuzi walio nje ya Chuo Kikuu cha Kiislamu nchini Uganda katika mji wa mashariki wa Mbale. Anauza takriban rolex 100 kwa siku kwa shilingi 2,000 za Uganda au dola 0.57 kila moja, haswa kwa wanafunzi.
Yeye hufanya kazi kwa haraka akitumia vitunguu, nyanya, pilipili hoho na karoti, na nyakati fulani huongeza vipande vya nyama iliyopikwa ikiwa mteja anataka kitu cha ziada.
Mchakato mzima wa kupikia rolex ni wa haraka - chini ya dakika tatu wakati viungo vyote viko tayari
Lakini wapenda vyakula wanasema ladha ya rolex ya hoteli haifikii ladha ya rolex inayopikwa barabarani.
Ni jambo la kawaida kuona watu waliovalia suti nadhifu wakiwa wamesimama kando na wale ambao bado hawajafanikiwa huku kila mmoja akisubiri agizo lake.
Sasa utambuzi wa Guinness World Records kwa rolex kubwa zaidi duniani kunamaanisha wakati umefika kwa ulimwengu kukumbatia mlo huu kutoka Uganda.