Kwa nini mwanasheria wa Kenya anataka Bibilia ifanyiwe marekebisho?

Wakili Joseph Hannington

Chanzo cha picha, Joseph Hannington

Maelezo ya picha, Wakili Joseph Hannington
Iliyochapishwa

Huenda ukajipata unasoma Biblia ukiwa na kalamu na kifutio baada ya kukutana na mwanasheria kutoka Kenya anayedai kuwa "ameagizwa" kutafsiri baadhi ya nambari ndani ya Biblia kwa njia ambayo hakuna mtu amefanya hapo awali.

Wakili Joseph Hannington, ambaye amekuwa mwanasheria kwa zaidi ya miaka 20, anahoji kwamba nambari za sura na aya za Biblia - ambazo ziliingizwa miaka kadhaa baada ya kuandikwa kwa Biblia - si tarakimu tu; lakini zina maana fulani.

Na kama ilivyokuwa na kitabu 'The Da Vinci Code' - kitabu ambacho kilichochea jumuiya ya Kikristo kwa tafsiri ya kubuniwa ya maisha na nyakati za Yesu - hoja ya Mkenya huyu bila shaka itazua mabishano si haba kwa sababu mwanasheria huyo anataka wamiliki wa Biblia kurekebisha baadhi ya mistari anayofikiri ilitafsiriwa vibaya na baadhi ya watafsiri wa Biblia.

'Nambari za Biblia hazipo kwa bahati mbaya lakini zimewekwa kimakusudi kama funguo za siri za Biblia. Hii ni sababu mojawapo kwa nini tunapaswa kuitazama tena Biblia kwa kuzingatia nafasi ya mistari hii, uhusiano wao na hivyo kupata muktadha mpya katika tafsiri yetu,' anahoji Bwana Hannington.

Wakili Joseph Hannington

Chanzo cha picha, Joseph Hannington

Maelezo ya picha, Mwanasheria huyo ametoa mifano ya mistari ya Bibilia iliyotafsiriwa kimakosa

Ni kutokana na mtazamo huo mpya, ambapo Hannington amedhamiria kuwaelekeza wamiliki wa Biblia kuhariri na kurekebisha baadhi ya aya kwa sababu zilitafsiriwa vibaya na baadhi ya watafsiri ambao walipuuza kanuni za kipekee anazozichambua.

Mifano ya mistari ya Bibilia iliyotafsiriwa kimakosa

Mwanasheria huyo ameandika kitabu chake 'The Cephas Code of Christ' ambapo ametoa mifano ya mistari ambayo anahisi imetafsiriwa kimakosa katika tafsiri za hivi karibuni za Biblia.

Hannington anasisitiza kuwa kitabu chake 'The Cephas Code of Christ' kina msingi wa Biblia na inachofanya kwa urahisi ni kuangalia tena aya na nambari za sura na kuonyesha kuwa sio za kimungu tu, bali zimeundwa kutoka mbinguni.

Wakili huyo anawataka wasomi wa dini, pamoja na viongozi wa kanisa kutumia tafrisi ya mwaka 1611 ya toleo la King James Version ambayo anadai ndiyo tafsiri pekee ya Biblia iliyo sahihi.

Hannington ambaye anajitambulisha kama mfuasi wa Kristo badala ya kuwa Mkristo, anasema mistari hiyo anayodai kuwa iliongezwa ni ya ishara na hivyo kutia mkazo maoni yake mapya katika kufasiri kanuni zinazoundwa na mistari hii.

'Kwa sasa kuna zaidi ya nakala tofauti tofauti 3,415 za Biblia. Lakini ukiangalia hizo zote utapata zina makosa katika kutafsiri na kuficha baadhi ya siri takatifu za neno la Mungu,' anadai Bwana Hannington.

Makasisi na viongozi wa dini ya Kikristo kwa upande mwingine wamepinga hoja ya Hannington kuwa ni ya kiholela wakisema sura na aya za Biblia zilipitishwa ili kufanya usomaji uwe wa mpangilio na rahisi ikizingatiwa kuwa kitabu hicho kiliandikwa kwa lugha tofauti.

Mchungaji Ron Swai

Chanzo cha picha, Ron Swai

Maelezo ya picha, Mchungaji Ron Swai, kiongozi wa Kanisa la Assemblies of God kutoka Tanzania.

'Wazo lake hilo halina msingi wowote wa kimaandiko. Ni kitu ambacho ameibua tu,' anaelezea Mchungaji Ron Swai, kiongozi wa Kanisa la Assemblies of God kutoka Tanzania.

Mchungaji Swai anasema Biblia iliandikwa na watu ambao waliongozwa na roho takatifu ya Mungu, na tafsiri mbali mbali zimedumisha mawazo yale yale, japo lugha inatofautiana.

'Viongozi wa dini tunaenda kwa madarasa ya Theolojia ili kujifunza na kuielewa Biblia. Na tunajua kwamba tafsiri zote tofauti za Biblia zinatafsiri lugha tu, lakini maana inasalia kuwa ile ile kwa sababu hayo ni mawazo ya Mungu si ya mwanadamu,' anasisitiza Mchungaji Swai.

Kiongozi huyo wa Kanisa la Assemblies of God nchini Tanzania amewataka waumini kutohadaiwa na watu, ambao anasema wanaweza kuipotosha imani.

Lakini mwanasheria huyo anatofautiana vikali na msimamo wa viongozi wa dini.

'Hakuna uzushi kuhusu hili. Haya yalikuwa mambo ambayo yaliahidiwa na Yesu mwenyewe. Yalisemwa na Yesu mwenyewe; yameandikwa na Yohana (mwanafunzi wake) mwenyewe. Kwa kweli, Biblia inatuambia kwamba katika siku za mwisho, itatubidi kuitazama tena Biblia nzima ili kuielewa.'

Sasa kuhusu madai ya mwanasheria Joseph Hannington, je, kuna nuru gizani? Au je, hii ni kujaribu kuziba mwanya ukifikiri ni pengo? Jibu ni la mtu binafsi, kwani waSwahili wanasema jino la pembe si dawa ya pengo.