Kamala Harris: Mwanamke wa kwanza kupata mamlaka ya urais wa Marekani kwa muda mfupi

Chanzo cha picha, Getty Images
Makamu Rais wa Marekani Kamala Harris alikuwa mwanamke wa kwanza kupewa mamlaka ya muda mfupi ya urais, wakati Joe Biden alipokuwa akifanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara wa kiafya.
Bi Harris, mwenye umri wa miaka 57, alikuwa na mamlaka ya uongozi wa nchi kwa kipindi cha dakika 85 wakati Bw Biden alipopewa dawa ya usingizi (nusu kaputi) kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa utumbo Ijumaa.
Daktari wa Bw Biden alitoa taarifa baada ya uchunguzi huo, akisema kuwa ni mwenye afya na anaweza kutekeleza majukumu yake ya kikazi.
Uchunguzi huo wa kimatibabu ulifanyika siku moja kabla ya Rais Biden kuadhimisha miaka 79 ya kuzaliwa.
Bi Harris alitekeleza majukumu hayo katika ofisi yake ya kawaida iliyopo katika jengo la West Wing la Ikulu ya White House, maafisa walisema.
Ni mwanamke wa kwanza- Mmarekani mwenye asili ya rangi nyeusi na Kusini mwa Asia - kuchaguliwa kama Makamu rais wa Marekani.
Afisa wa habari wa White House Jen Psaki alisema kuwa kuhamishwa kwa muda wa mamlaka katika hali kama hiyo ni jambo ambalo halikuwa la ajabu, na kwamba ni sehemu ya mchakato ulliopangwa na katiba ya Marekani.
"Kama ilivyokuwa wakati Rais George W Bush alipofanyiwa uchunguzi sawa na huu katika miaka ya 2002 na 2007," alisema katika taarifa.
Rais Biden alionekana akitabasamu alipokuwa akirejea katika Ikulu ya White House. "Nahisi vizuri," alisema.
"Rais Biden ameendelea kuwa mwenye afya, mkamavu, mwanaume mwenye miaka 78, ambaye ana uwezo wa kufanikiwa kutekeleza majukumu yake ya urais ," alisema Kevin O'Connor, daktari wa rais.
Kevin O'Connor, ambaye ni daktari binafsi wa rais, alisema utumbo wa rais ulipatikana "umeanza kuonekana kuwa na uvimbe mdogo" ambao ulikuwa rahisi kuuondoa.

Chanzo cha picha, EPA
Bw O'Connor aliongeza kwamba mwendo wa rais ulionekana "wa kukakamaa na wa mtu asiye na maji maji ya mwili," kuliko siku zilizopita. Hii ilitokana na kuharibika na kupasuka kwa mgono.
Bw Biden, ambaye ni rais mwenye umri mkubwa zaidi kuwahi kuiongoza Marekani, alikuwa amefanyiwa uchunguzi wa mwisho wa kimatibabu mwezi Disemba 2019.
Wakati huo, daktarin wake alitoa ripoti ya matibabu yake akimuelezea kama "mwenye afya, mkakamavu'' na "anayeweza kutekeleza kwa mafanikio majukumu yake ya kikazi ya urais".












