Jinsi wakazi wa Mlima Elgon walivyobadili kilimo chao kutokana na mabadiliko ya tabia nchi

    • Author, Roncliffe Odit
    • Nafasi, BBC Swahili, Nairobi
  • Iliyochapishwa

Migomba mirefu, miti ya matunda na mimea maridadi ndiyo inayokukaribisha katika shamba la Bwana Muneria Joseph ambaye ni mkulima katika wilaya ya Kapchorwa, mashariki mwa Uganda.

Ni taswira maridadi, picha ya mkulima anayetarajia kuvuna mazao mengi ikiwa kila kitu kitasalia kama ilivyo sasa. Na hiyo ndiyo taswira unayokumbana nayo katika maeneo mengi wilayani Kapchorwa na eneo zima la Mlima Elgon, mashariki mwa Uganda.

Mashamba yaliyojaa mimea ambayo yanaonekana kuwa maridadi na yanayopendeza sana.

Lakini hali haikuwa hivi miaka kadhaa iliyopita. Eneo hili la Kapchorwa na Mlima Elgon kwa ujumla lilipitia hali mbaya ya mabadiliko ya tabia nchi.

Kwanza mvua ilibadili taratibu ya kunyesha, na kisha wakati iliponyesha kukawa na mafuriko makubwa na maporomoko ya ardhi.

Aidha wengi wa wale waliokuwa wakitegemea mvua kwa ajili ya kilimo wanasema mabadiliko ya tabia nchi yaliwaathiri pakubwa.

'Zamani mvua ilikuwa inanyesha vizuri, lakini mabadiliko ya hali ya anga yameathiri kabisa kilimo chetu,' anasema Bwana Muneria.

'Siku hizi hakuna mvua kama ilivyokuwa ikinyesha zamani, tunaweza kwenda hata mwaka bila kuona mvua.

Bwana Muneria sawia na wakulima wengi katika eneo hili la Kapchorwa amelazimika kubadili njia yake ya kilimo ili kupata mazao.

'Sasa inatulazimu kufanya kilimo cha kunyunyizia mashamba maji. Nimeanza kutumia mbinu hiyo takriban miaka mitano iliyopita. Nimeweka mabomba katika shamba langu ili angalau nifurahie kilimo.', anasema Muneria.

Wakulima wengi mashariki mwa Uganda sasa wamekumbatia mbinu za kisasa za kilimo ili kuweza kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kujiendeleza katika kilimo.

Bwana Joseph Kishare, afisa wa kilimo katika eneo la Kapchorwa anasema bila mabadiliko hayo, kilimo kilikuwa kimefifia kabisa.

'Wakulima wa kahawa walijipata wana magonjwa mengi kwa mazao yao yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya anga. Kahawa zikaanza kukauka na wakulima wakapata hasara kubwa,' anasimulia Bwana Kishare.

Aidha hali hii ya magonjwa kwa mimea ilisababisha bei ya kahawa katika eneo hili kupungua kabisa. Ni changamoto ambayo iliilazimu idadi ya kilimo katika eneo hili la Kapchorwa kuanza kutoa mafunzo kwa wakulima ili kutumia mbinu za kisasa za kilimo.

Na hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha hali ya kilimo mashariki mwa Uganda.

'Tumeanza kwa kuwaelimisha wakulima jinsi ya kulima kwa kunyunyiza maji mashambani, na pia jinsi ya kutumia madawa ya kisasa ili kuzuia wadudu wanaosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi,' anaeleza Bwana Joseph Kishare, afisa wa kilimo katika eneo la Kapchorwa.

Utafiti wa hivi majuzi uliopewa jina la Kustahimili Mabadiliko ya Tabia Nchi Mlima Elgon: Athari za Sera na Mapendekezo, uliofanywa na Daniel Olago, John P. Owino na Eric Odada unaonyesha baadhi ya mabadiliko yaliyofanywa ili kukuza kilimo katika eneo la Mlima Elgon.

Ni pamoja na kupanda mazao yenye mavuno mengi na yanayostahimili ukame, kufanya mzunguko wa mazao na pia uzalishaji wa vyakula vya mifugo ili kupunguza shinikizo kwenye malisho ya milimani. Kwa hivyo mifumo ya kitamaduni inakabiliwa na mbinu kali zaidi za kilimo.

Na hapa Kapchorwa hilo liko dhahiri kutokana na mashamba na mazao unayokutana nayo hapa. Sasa badala ya kuwa na shamba kubwa lililopandwa aina moja pekee ya mazao, unakuta mashamba ambayo yana mchanganyiko wa mazao ili kuendeleza kilimo stahimili kwa hali ya anga inayobadilika.

Pia wakulima wengi sasa wanatumia maji ya mabomba kunyunyizia mashamba yao, na dawa za kisasa ili kuzuia wadudu wanaoshambulia mimea.

Lakini wakulima hawa wanasema bado mengi yanahitaji kufanywa ili kukabiliana vyema na mabadiliko ya tabia nchi.

Unaweza pia kutazama: