Afghanistan: Wakimbizi wataenda wapi baada ya Taliban kuchukua udhibiti?

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelfu ya watu wanahangaika kukimbia Afghanistan baada ya Taliban kuchukua udhibiti wa nchi hiyo, karibu miongo miwili baada ya kuong'olewa madarakani na vikosi vya muungano vikiongozwa na Marekani
Idadi ya watu wanaotaka kuondoka nchini humo inaongezea wakimbizi milioni 2.2 ambao tayari wamekimbilia nchi jirani na wengine milioni 3.5 ambao wameachwa bila makao ndani ya mipaka ya Afghanistan kutokana na mzozo unaoendelea na misukosuko ya kisiasa.
Ni Waafghanistan wangapi wanaondoka?
Kwa sasa idadi kamili haijabainika.
Taliban wanadhibiti maeneo yote muhimu yanayokaribiana na majirani wa Afghanistan (kama inavyooneshwa katika ramani hapo chini) na wanamgambo wamesema hawataki Waafghanistan waondoke nchini.
Ripoti zinaashiria kuwa ni wafanyabiashara na wale walio na vibali sahihi vya usafiri wanaruhusiwa kuvuka.
"Raia wengi wa Afghanistan hawawezi kuondoka nchini kupitia njia za kawaida," msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kushughulikia Wakimbizi(UNHCR) alisema siku ya Ijumaa. "Kufikia leo, kuna wale ambao huenda wako hatarini na hawana njia ya kutoka."

Hata hivyo, baadhi ya wakimbizi wamefanikiwa kupata njia ya kuondoka nchini.
Maaelfu kadhaa ya raia wa Afghanistan wanasadikiwa kuvuka mpaka na kuingia Pakistan muda mfupi baada ya Taliban kuchukua udhibiti wa Kabul, huku wengine 1,500 wakiripotiwa kuingia Uzbekistan na wanaishi kwenye mahema karibu na mpaka.
Mjini Kabul, maelfu ya wangeine wamekuwa wakielekea uwanja wa kimataifa wa ndege ambao ndio uwanja pekee unaofanya kazi kwa sasa, wakijaribu kuodoka nchini.
Ijumaa iliyopita, afisa wa Shirika la Kujihami la Mataifa ya Magharibi (Nato), alisema zaidi ya watu18,000 awamesafirishwa kutoka uwanja wa ndege wa Kabulu tangu Taliban walipochukua udhibiti wa mji huo mkuu, lakini haijathibitishwa ni wangapi kati ya hao ni raia wa Afghanistan.
Ni watu wangapi wametoroka makwao?
Harakati za hivi karibuni ya Waafghanistan ni sehemu ya safari ya kihistoria kutoka nchi ambayo imekosa utulivu kutokana mizozo ya miaka mingi.
Hata kabLa ya Taliban kuchukua tena usukani, zaidi ya watu 550,000 walikuwa wamelazimika kutoroka makwao mwaka huu kutokana na mapigano, kulingana na UNHCR.
Hii inamaanisha karibu watu milioni 3.5 raia wa Afghanistan kwa sasa ni wakimbizi wa ndani.

Mbali na wale walio ndani ya mipaka ya Afghanistan, karibu wakimbizi milioni 2.2 walikuwa wanahtafuta hifadhi katika mataifa jirani kufikia mwisho wa mwaka jana.
Mwaka huu, raia wa Afghanistan pia walikabiliwa na ukame mbaya na uhaba wa chakula ulioshuhudiwa katika meneo mengi nchini.
Ripoti ya Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa WFP ya mwezi Juni ilisema kwamba watu milioni 14 - zaidi ya thuluthi moja ya watu wote nchini humo -walikuwa wanakabiliwa na njaa.
Wakimbizi wa Afghanistan wanaenda wapi?
Nchi jirani za Pakistan na Iran zilishuhudia idadi kubwa zaidi ya wakimbizi wa Afghanistan na waomba hifadi mwaka jana.
Karibu watu milioni 1.5 walikimbilia Pakistan mwaka 2020, huku Iran ikiwapokea wakimbizi 780,000, kwa mujibu wa takwimu za UNHCR.

Mataifa yanafanya nini kuwasaidia?
Iran
Iran imeweka mahema katika mikoa mitatau ambayo inapakana na Afghanistan ili kuwasaidia wakimbizi. Lakini maafisa wa ngazi ya juu wa wizara ya mambo ya ndani wamesema raia wa Afghanistan waliovuka mpaka na kuingia Iran "wataregeshwa makwao hali itakapoimarika". Iran tayari inawahudumia wakimbizi karibu milioni 3.5 wa Afghanistan, kulingana na UN.
Pakistan
Waziri Mkuu Imran Khan alisema mwezi Juni kuwa nchi hiyo itafunga mipaka yake na Afghanistan ikiwa Taliban watachukua uongozi. Hata hivyo, ripoti zinasema maelfu kadhaa ya raia wa Afghanistan wamevuka mpaka na kuingia Pakistan na kwamba angalau mpAka mmoja uko wazi. Taliban wanasemekana kudhibiti njia ya kufika eneo hilo na kwamba wanaoweza kutoka ni wafanyabishara na wale walio na stakabadhi halisi ya usafiri.
Tajikistan
Idadi kamili haijathibitishwa lakini ripoti zinaashiria karibu mamia ya Waafghanistan wakiwemo maafisa wa jeshi la kitaifa la Afghanistan , wamevuka mpaka na kuingia nchini Tajikistan katika siku za hivi karibuni. Mnamo Julai, Tajikistan ilisema ilikuwa ikijiandaa kuchukua hadi wakimbizi 100,000 kutoka Afghanistan.
Uzbekistan
Karibu raia 1,500 Afghanistan wanasemekana kuvuka mpaka wa Afghanistan-Uzbekistan na kupiga kambi nchini humo. Ripoti zinaonyesha kuwa Taliban inaruhusu tu watu wenye visa halali kutumia njia rasmi za kuvuka mpaka.
Uingereza
Uingereza imetangaza mpango wa kuwapokea wakimbizi 20,000 wa katika kipindi cha muda mrefu Afghan. Mpango wa makazi ya raia wa Afghanistan wa serikali ya Uingereza utakusudia kuwaruhusu Waafghanistan 5,000 kukaa nchini Uingereza katika mwaka wa kwanza na itazingatia wanawake na watoto na pia watu wa dini ya wachache walio katika hatari kubwa ya kushambuliwa na Taliban.

Chanzo cha picha, Getty Images
Marekani
Rais Joe Biden ameidhinisha matumizi ya dola milioni 500 kwa ajili ya "wakimbizi wasiotarajiwa na mahitaji ya dharura uhamiaji kwa wakimbizi, wahanga wa mizozo na watu wengine walio hatarini kutokana na hali nchini Afghanistan.
Canada
Canada imesema kuwa itawapa makazi ya Waafghanistan elfu ishirini, ikilenga wale walio katika hatari ya kushambuliwa na Taliban, pamoja na wafanyikazi wa serikali na viongozi wanawake.
Ujerumani
Ujerumani imesema itawapokea baadhi ya raia wa Afghanistan, lakini haijabainisha idadi yao. Kansela Angela Merkel, ambaye alikabiliwa na ukosoaji mkubwa kutokana na sera yake ya mwaka 2015 ya kuwapokea wahamiaji, amesema kuwa serikali yake ililenga kuhakikisha kuwa wakimbizi "wanakaa salama katika nchi jirani za Afghanistan".

Chanzo cha picha, Getty Images
Ufaransa
Rais wa Emmanuel Macron amesema kwamba Ulaya lazima "ijilinde dhidi ya wimbi la kubwa la wahamiaji haramu" kutoka Afghanistan. Amesema Ufaransa "itawalinsa wale walio kwenye hatari zaidi", lakini akaongeza kuwa: "Ulaya haiwezi kuwajibikia matokeo ya hali ya sasa peke yake."
Uswizi
Uswizi imesema haitapokea idadi kubwa ya wakimbizi wanaowasili moja kwa moja kutoka Afghanistan.
Uturuki
Rais Recep Tayyip Erdogan amesema serikali yake itashirikiana na Pakistan kusaidia kuleta utulivu Afghanistan na kuzuia wimbi jipya la wakimbizi wanaoelekea Uturuki. Serikali pia imeongeza ujenzi wa ukuta wa mpaka na Iran kuwazuia wahamiaji kutoka nje.
Uganda
Uganda imekubali kuwapokea wakimbizi 2,000 wa Afghanistan.Nchi hiyo ya Afrika Mashariki ina idadi kubwa ya wakimbizi kuliko nchi nyingine yoyote ya Afrika - na ya tatu duniani.












