Rais Samia: 'Wanamichezo kama hamjachanja naomba sana mkachanje'

Iliyochapishwa

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametangaza kwamba atadhamaini mashindano ya kila mwaka ya ubingwa wa Cecafa kwa wanawake .

Rais Samia amesema amelichukua jukumu hilo baada ya ombi la rais wa TFF nchini humo ili kuwa na mashindano ya wanawake ya Cecafa kama yale ya wanaume ambayo hudhaminiwa na rais wa Rwanda Paul Kagame .

Rais Samia ameyasema hayo jumapili akipokea Kombe la Ushindi la Michuano ya Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati kwa vijana wenye umri chini ya miaka 23 (CECAFA CHALLENGE CUP 2021) katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Rais pia aliwashukuru wanamichezo wa Tanzania walioshiriki mashindano ya Olimpiki yaliyokamilika nchini Japan .Alisema kuna haja ya kuwekeza Zaidi katika mfuko wa kuwafadhili wanamchezo wan chi hiyo ili kuendeleza talanta zao na kuiwakilisha nchi .

Kuhusu hatua yake ya kudhamini mashindano ya ubingwa wa Cecafa kwa wanawake ,rais Samia alisema kiasi cha fedha kinachohitajika ni kikubwa lakini anajua atakapozipata fedha hizo .

'Lakini nimepima misuli yangu nikaona mwenyewe sitaweza lakini najua nitakapozipata…kwa hivyo niwatangazie kwamba nitadhamini hayo mashindano' amesema rais Samia

Wanamichezo kuchanjwa dhidi ya COVID 19

Wakati huo huo Rais wa Tanzania Samia Suluhu amewahimiza wanamichezo nchini humo kuchanjwa dhidi ya Covid 19 .

Rais Samia amesema ni muhimu kwa wanamichezo kuchanja kwa sababu kando na kusafiri katika maeneo mbali mbali ya ulimwengu ,watakuwa pia wamejipa kinga dhii ya makali ya ugonjwa huo .

' Lakini wanamichezo mnasafiri hapa na kule na kila mnapopita testing za covid zinawasubiri ukichanja kwanza utakuwa na ushahidi kwamba umechanja lakini pili hata kama maradhi yatakupatahayaji kwa nguvu kama utakavyokuwa hujachanjwa.' Alisema Rais Samia .

Rais Samia alitoa mfano kwamba kuna watu ambao walikuwa amechanjwa lakini wakapatwa na maambukizo ya COVID 19 ,ambao hawakuathirika sana kwa sababu ya kinga waliopata kutokana na chanjo dhidi ya ugonjwa huo .

' Wamekwenda tu vizuri na shughuli zao ..unampigia simu kumuuliza unaendeleaje? Anakuambia niko vizuri ..'

Alisisitiza kwamba chanjo huenda sio kinga kabisa dhidi ya ugonjwa huop lakini inapunguza kabisa hatari ya kufa kwa sababu ya maradhi mengine nyemelea .

Katika hatua ya kuendelea kuwahakikishia watu kuhusu usalama wa chanjo rais Samia alisema ;

'Mimi mama yenu ,mkuu wenu sitapeleka jamii yangu kwenye hatari ..hata siku moja'

Ili kuondoa uoga kuhusu madai ya baadhi ya watu ambao wamekuwa wakipinga chanjo ya Covid 19 nchini humo Rais Samia alisema ;

'Kuna mwanangu aliimba huwezi kushindana na mwanadamu mwenye kinywa ..mwenye kinywa atasema tu anayotaka kusema lakini ukweli utabaki pale pale kwamba chanjo hizo zinasaidia kupunguza maumivu na kupunguza hatari ya vifo kwa watu'.