Shambulio la meli ya mafuta: Marekani na Uingereza zailaumu Iran na kuapa kujibu shambulio la meli ya mafuta ya Israeli

Chanzo cha picha, Johan Victor via Reuters
Uingereza na Marekani zinaamini kuwa Iran ilifanya shambulio la meli ya mafuta ambalo liliwauwa watu wawili, na zimeapa kujibu shambulio hilo, zikilitaja kuwa ni ukiukaji wa sheria ya kimataifa.
Meli hiyo MV Mercer Street, ya kampuni inayomilikiwa na Israel , ilishambuliwa ilipokuwa kwenye mwambao wa Oman siku ya Alhamisi.
Raia wa Uingereza na mwingine wa Romania waliokuwemo ndani yake waliuawa.
Taarifa hii inakuja baada ya Waziri Mkuu wa Israeli Naftali Bennett kusema kuwa kulikuwa na "ushahidi" kwamba adui wa muda mrefu Iran alihusika.
Bw Bennett alionya kwamba " tunajua jinsi ya kutuma ujumbe kwa Iran kwa njia yetu wenyewe", huku Iran ikikana kile ilichokiita "shutuma zisizo na msingi".
Shambulio dhidi ya MV Mercer Street linaonekana kuwa ni la hivi karibuni katika ''vita vya kimkakati'' vinavyoendelea ambavyo havijatangazwa baina ya Israeli na Iran.
Tangu mwezi Machi kumekuwa na mashambulio kadhaa dhidi ya meli za nchi zote mbili mbili Israeli na Iran. Waathiriwa katika matukio hayo huwa ni nadra.
Iran pia imeishutumu Israeli kwa kulenga viwanda vyake vya nyuklia na wanasayansi wake.
Katika taarifa iliyotolewa Jumapili, Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Dominic Raab alisema kuwa Uingereza inaamini kuwa Iran ilitumia moja ya ndege zake zisizo na rubani katika shambulio hilo dhidi ya meli ya MV Mercer Street, ikilitaja kuwa la "makusudi'', na kwamba ni ukiukaji wa wazi wa sheria ya kimataifa ".
"Iran lazima iache mashambulio ya aina hii, na meli lazima ziruhusiwe kusafiri kwa uhuru ,"aliongeza.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken alisema kuwa Washington pia "inaamini kwamba Iran ilifanya hili ",na kwamba "jibu linalofaa" litafuatia.
Waziri mkuu wa Israeli alisema kuwa anatarajia jamii ya kimataifa kuwa wazi na kuiambia Iran imefanya kosa baya.

Chanzo cha picha, EPA
Iran haikuficha lolote katika jibu lake. Msemaji wa Wizara yake ya mambo ya ndani Saeed Khatibzadeh, aliwaambia wandishi wa habari kwamba "utawala wa Wazayuni (Israel) umesababisha ukosefu wa usalama, ugaidi na ghasia ".
Alisema kuwa Israeli "lazima iache shutuma zisizokuwa na msingi ", akionya : "Yeyote anayepanda mbegu ya upepo huvuna kimbunga."
Kuongezeka kwa uhasama huu kunakuja huku yakifanyika mazungumzo muhimu ya nyuklia mjini Vienna.
Maafisa wanasema wanataka kufufua mkataba wa kimataifa wa mwaka 2015, ambao kwa mujibu wake vikwazo dhidi ya Iran vinaondolewa ili Iran iwajibike katika kukabiliana na mpango wake wa nyuklia.
Nchi za magharibi zimeishutumu Iran kwa kujaribu kutengeneza bomu la nyuklia . Iran inakanusha shutuma hizi, ikisisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia ni kwa ajili ya utafiti na utengenezaji wa nishati.













