Mlipuko wa volkano Congo: Makumi ya watoto hawajulikani walipo
- Author, Na Olivia Acland
- Nafasi, Goma, DR Congo
- Iliyochapishwa
Lava iliyotiririka kutoka Mlima Nyiragongo Jumamosi jioni imeleta uharibifu na maafa katika wilaya ya kaskazini ya mji wa Goma, mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Takriban nyumba 500 ziliteketea na zaidi ya watoto 100 hawajulikani walipo baada ya kutengana na wazazi wao wakati wakikimbia lava kutoka mlimani, kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto (Unicef).

Chanzo cha picha, Olivia Acland
Charles Kambale amekuwa akisaka kwenye vifusi vilivyosalia katika eneo ambalo nyumba yake ilikuwa kabla ya kuteketezwa na lava katika wilaya ya Buhene.
"Sijawaona watoto wangu wawili wadogo," alisema.
Alikuwa harusini na mke wake wakati mlipuko ulipoanza. Watoto wake wawili mmoja wa miaka sita, na mwingine wa miaka miwili walikuwa nyumbani na majirani. Anasema anapanga kutoa tangazo redioni ili watu wamsaidie kuwatafuta.

Chanzo cha picha, Olivia Acland
Watoto pia wamekuwa wakisaka kwenye vifusi vipande vya chuma au sufuria zilizoungua kwa ajili ya kuuza.

Chanzo cha picha, Olivia Acland
Anga la Goma lilibadilika na kuwa jekundu siku ya Jumamosi wakati volcano ilipolipuka na kutirirsha lava.
Kwa kuogopa kuwa lava ingefunika baadhi ya maeneo ya mji na kuwaua mamia ya watu, kama ilivyofanya mwaka 2002, mamia ya watu walikusanya mali zao na kukimbia kuelekea kwenye mpaka wa nchi jirani ya Rwanda.

Chanzo cha picha, Olivia Acland
Zaidi ya watu 3,500 walivuka mpaka katika usiku wa mlipuko pamoja na uwepo wa foleni kubwa ya magari. z
Wengi wa wakazi wa Goma wamezoea kukimbia. Makundi ya waasi yenye silaha yamekuwa tisho kwa eneo hilo kwa zaidi ya miaka 25 na wengi wanaoishi katika mji huu walihamia baada ya ghasia kuviathiri vijiji vyao vilivyo karibu.

Chanzo cha picha, Olivia Acland
Tofauti na mwaka 2002, watu wachache wameripotiwa kupoteza maisha hadi sasa

Chanzo cha picha, Olivia Acland
Baadhi ya watoto waliokimbia mtiririko wa lava na kutenganishwa na wazazi wao wanakaa katika kituo kinachoendeshwa na Shirika la Msalaba Mwekundu mjini Goma.
Wafanyakazi wa shirika hilo na baadhi ya maafisa wa serikali wanajaribu kuwaunganisha na familia zao.

Chanzo cha picha, Olivia Acland
Benisse mwenye umri wa miaka minne ametengana na familia yake tangu mlipuko ulipotokea.
Mama yake alienda kuuza samaki sokoni wakati mlipuko ulipotokea na akakimbilia kwa majirani na watoto wengine.
Alikuwa akizurura karibu usiku mzima katika mji mwingine wa Sake, uliopo kilomita 23 (maili 14) kutoka Goma, ambako alilala kando ya barabara.
"Nilitoroka na marafiki zangu, lakini hata sijui wako wapi sasa, niko peke yangu hapa," Benisse alimwambia Gilbert Ramazani, anayefanya kazi katika kitengo cha serikali cha masuala ya jamii.

Chanzo cha picha, Olivia Acland
Akina mama wenye wasiwasi wamekuwa wakiwasaka watoto wao kutoka kituo kimoja hadi kingine, kuona iwapo wanaweza kuwapata.
Na baadhi wamefanikiwa kuwapata watoto wao.

Chanzo cha picha, Olivia Acland
Sifa Ombene, mwenye miaka 32, alikuwa amekwenda kuuza chakula nje wakati mlipiko ulipotokea.
Alikimbia kwenda nyumbani lakini hawakuwakuta watoto wake wawili, walikuwa wameshakimbia. akakuta watoto wake wawili wametoroka.
"Nilienda kila mahali kuwatafuta watoto, nilienda hata mochwari, walinionesha miili ya watoto waliokufa," alisema huku akiwa amemkumbatia binti yake Elea mwenye miaka minne.
"Ninafuraha sana kuwapata hapa."
Picha zote na Olivia Acland.














