Mbunge wa Kenya Moses Kuria amekiri kupokea hongo ya $1,000

Chanzo cha picha, AFP
Mbunge wa Kenya Moses Kuria ameiambia BBC alipokea rushwa ya $ 1,000 bungeni mwaka jana kuunga mkono uteuzi wa kiongozi wa wengi bungeni.
"Sio jambo la ajabu kwa wabunge kupata vishawishi vya aina hii," alisema, akiongeza kuwa atarudisha fedha hizo.
Bwana Kuria alisema hayo wakati yeye na wenzake wawili watashtakiwa kwa madai ya malipo yalifanywa ili kuunga mkono muswada wa marekebisho ya katiba.
Kiongozi wa wengi Amos Kimunya amekanusha madai kuwa hongo hulipwa bungeni.
BBC imemtaka Bw Kimunya kujibu madai ya Bw Kuria lakini bado hajazungumza chochote.
Wabunge wa Kenya ni baadhi ya wabunge wanaolipwa zaidi ulimwenguni - na maafisa wanakadiria kuwa Kenya hupoteza mabilioni ya dola kila mwaka kwa ufisadi.
Bw. Kuria amesema nini ?
Bw Kuria alisema ameshuhudia ufisadi mara nyingi bungeni.
"Na imetokea mara nyingi, kwa miaka minane ambayo nimekuwa bungeni," aliiambia kipindi cha Newsday cha BBC.
"Ni wazi kwamba mambo haya hayafanyiki kwenye kamera."
Alitoa mfano wa uteuzi wa Bw Kimunya. Alichukua nafasi ya Aden Duale kama kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa Juni mwaka jana.
Mbunge wa eneo bunge la Gatundu Kusini alikiri kwamba vitendo vya rushwa vilikuwa vibaya.
"Ni makosa. Na nadhani ndio ... nikipewa nafasi ningerejeshea angalau ile ninayoweza kukumbuka waziwazi," alisema.
"Labda nitafanya leo ... kurejesha $ 1,000 ambayo nilipokea kumpigia kura katika Amos Kimunya kama kiongozi wa wengi."
Bw Kuria alizungumza na BBC baada ya kuitwa mbele ya spika kwa kuwa alitoa madai ya kuwa wanasiasa walipokea karibu dola 1,000 kupiga kura ya muswada wa marekebisho ya katiba unaojulikana kama Building Bridges Initiative (BBI).

Chanzo cha picha, Getty Images
Bw Kuria aliambia BBC vishawishi vingine vilikuwa vimetumika kuwashawishi wanasiasa - kama vile mahitaji ya washiriki wa bunge la kaunti kwamba wangeunga mkono tu muswada wa BBI wa misaada ya gari, takriban yenye thamani ya dola 20,000 kila mmoja.
Tume ya Mishahara (SRC) iliidhinisha misaada hiyo mwezi Februari.
Hatahivyo, Mahakama Kuu ya Kenya Alhamisi iliamua kwamba muswada huo haukuwa wa kikatiba, ukiharibu mipango ya kura ya maoni kupigwa baadaye mwaka huu.













