Tshisekedi afanikiwa kuunda serikali mpya ya mseto, jee sasa yuko imara kuyadhibiti madaraka ?

- Author, Mohammed AbdulRahman
- Nafasi, Mchambuzi
- Iliyochapishwa
Miezi minne baada ya Rais Felix Antoine Tshisekedi Tshilomba wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, kuamua kuachana na ushirika na mtangulizi wake Joseph Kabila Kabange na hivyo kuivunja serikali ya mseto, amefanikiwa kuunda serikali mpya.
Serikali hiyo iliotangazwa mapema wiki hii, inaundwa na washirika wapya chini ya muungano anaouita "Muungano Mtakatifu". Mbali na wafuasi wa Kabila waliompa kisogo, muungano huo unaungwa mkono na wapinzani wa kiongozi huyo wa zamani.
Hapana shaka kutangazwa kwa baraza jipya la mawaziri ni pigo jengine kubwa kwa mtangulizi wa Tshisekedi ambaye hadi Desemba 2020 alikuwa ni mshirika katika serikali ya awali ya mseto, kabla ya kuvunjika.
Chanzo cha kuvunjika serikali hiyo iliodumu miaka miwili, kilikuwa ni jaribio la Kabila ambaye tangu alipokabidhi madaraka Januari 2019 amekuwa akilazimisha kuwa na usemi mkubwa zaidi. Kabila pamoja na kwamba aliendelea kuzidhibiti wizara muhimu, sheria, mahakama na idara za usalama, hakuridhika. Alidai kuwa na usemi katika maamuzi ya Tshisekedi.
Serikali mpya ina mawaziri 56 na ni baraza dogo la mawaziri ikilinganishwa na la serikali iliopita. Muhimu mbali na kugawana nyadhifa za uwaziri ni uteuzi wa wanawake na vijana katika baraza hilo .
Kuna wanawake 15, akiwemo Eve Bazaiba, mpinzani wa muda mrefu wa Kabila kutoka chama cha Ukombozi wa Congo-MLC kinachoongozwa na Jean-Pierre Bemba. Bazaiba anakuwa Waziri wa mazingira na naibu waziri mkuu, miongoni mwa manaibu waziri mkuu wanne.

Chanzo cha picha, Eve Bazaiba /twitter
Kuundwa baraza la mawaziri, kulitokana na mazungumzo ya takriban miezi minne na Bemba pamoja na Gavana wa Mkoa wa Katanga Moise Katumbi baada ya ushirikiano na Kabila kuvunjika.
Mfuasi wa karibu wa Katumbi Christophe Lutunda anakuwa Waziri wa mambo ya nchi za nje. Wadadisi wanasema uteuzi huo utamsaidia Tshisekedi kupata uungaji mkono usiotetereka wa Katumbi na Bemba kumuwezesha kutawala bila ya msukosuko.
Katumbi Gavana wa zamani wa Katanga alifanyiwa mizengwe na Kabila na kumzuwia kugombea urais katika uchaguzi wa Desemba 2018. Ushindi mwengine wa kisiasa kwa Katumbi ni ile hatua ya Tshisekedi mwezi Februari, kumteuwa Jean-Michel Lukonde kuwa Waziri mkuu.
Lukonde ni mkuu wa zamani wa Kampuni kubwa ya madini katika mkoa wa Katanga ya Gecamines. Kwa matukio hayo Katumbi anahisi amefanikiwa pia kumpiga mwereka Kabila.
Inaelekea mikakati ya Tshisekedi kupata washirika wapya kwa kuunda Umoja alioupa jina " Muungano Mtakatifu" imefua dafu na amefanikiwa kumtenga Kabila ambaye wanasiasa kadhaa kutoka chama chake FCC wamempa mgongo na kujiunga na muungano huo.

Tshiekedi ambaye alirithi uongozi wa chama chake cha UDPS baada ya kifo cha baba na mwanasiasa mkongwe Etienne Tshisekedi wa Mulumba Februari 2017, aliitwa kwa kejeli "Un Président sans pouvoir " (Rais asiye na madaraka), sasa ameyadhibiti kikamilifu.
Wachambuzi wanaamini wengi wa wanasiasa walioungana na Tshisekedi wanataka mabadiliko, kinyume na hapo awali ambapo kilichokuweko ni kinyanganyiro tu cha kuwania nafasi serikalini.
Hatua alizochukuwa kuzipangua safu za uongozi katika idara za usalama likiwemo jeshi la taifa pia zinampa ujasiri wa kuweza kudhibiti hatamu za uongozi na kuanza kuleta mageuzi anayoyakusudia ya kile wakongomani wanachokiita " Congo mpya".
Tshisekedi binafsi amesisitiza kwamba kuboresha hali za maisha ya wacongo na kujenga mazingira ya usalama kote nchini, ndio kipaumbele kwa serikali mpya. Walau kwa sasa Fatchi kama anavyoitwa na wafuasi wake, ana kila sababu ya kupumua baada ya kuungwa mkono na bunge na baraza la Seneti .
Wakati sura zinazoonekana ni zile zile, misimamo ya wengi wa wajumbe imebadilika Jukumu lao la kwanza kabisa litakuwa kushughulikia mageuzi ya masuala mbali mbali zikiwemo sheria mpya za uchaguzi na uteuzi wa wajumbe wapya wa tume ya uchaguzi.

Chanzo cha picha, MBELECHI MSOCHI
Kwa upande wa serikali italazimika sambamba na hayo kuanza kutatua matatizo ya kiuchumi.
Mchambuzi wa masuala ya maziwa makuu na mwandishi habari mkongwe wa kimataifa Bizokunda wa Bizo anasema, Wakongomani wanamtazama rais wao kwa hisia tafauti, mchanganyiko wa matumaini na tahadhari wakati mmoja.
Matumaini yao ni kwamba kwa kuwa na serikali imara na wingi alionao bungeni ataweza kushughulikia hali duni za maisha ya wengi wa raia , Wanaamini njia muafaka kufanikisha hayo ni kuwa na ujasiri wa kupambana kwa dhati na ufisadi uliokithiri.
Tshisekedi hana budi kuchukua hatua za kisheria kurejesha mali zilizoibiwa na wanasiasa na watendaji wakuu serikalini, baadhi wakihodhi utajiri usio na kifani.
Bila ya kuwa na ujasiri wa kufanya hivyo, raia watapoteza Imani sio tu kwake bali pia kwa serikali.
Kwa kuzingatia yalioisibu Congo kwa muda mrefu na ubadhirifu na wizi wa mali ya umma kugeuka jambo la kawaida haitokuwa kazi rahisi.
Pamoja na Tshisekedi kuliita baraza lake la mawaziri kuwa la wapambanaji, Wataalamu wa masuala ya uchumi nao wanasema licha ya kupanda kwa bei ya madini ya shaba na cobalt, hazina ya taifa karibu ni tupu.

Chanzo cha picha, Reuters
Kwa upande mwengine kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa watu milioni 27.3 katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, ikiwa ni karibu ya theluthi moja ya idadi jumla ya wakaazi wanakabiliwa na njaa, kutokana na athari za kiuchumi.
Taarifa ya Shirika la mpango wa chakula la Umoja huo (WFP) na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) Congo imeingia katrika orodha ya watu wanaohitaji msaada wa dharura wa chakula.
Miongoni mwa sababu kubwa za hali hiyo, ni vita ambapo maeneo yalioathirika zaidi ni pamoja na ile mikoa ya mashariki ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kusini, ambako serikali imekuwa ikipambana na makundi ya waasi kwa miongo kadhaa. Kwa kuzingatia yote hayo, changamaoto ni kubwa.
Katumbi na Bemba, vigogo wawili waliomunga mkono Tshisekedi kumdhibiti Kabila na kufanikisha kuundwa serikali mpya, wameamua kubakia nje ya serikali hiyo. Huenda lakini wakawa wanajiandaa kumkabili Tshisekedi atakaposimama tena kugombea muhula wa pili katika uchaguzi wa 2023.
Unaweza pia kusoma:
Mgombea urais aliyeshindwa , kiongozi wa muungano wa LAMUKA Martin Fayulu, amekataa kujiunga na serikali mpya akisisitiza kuwa hawezi kujiunga na mshindwa aliyewekwa madarakani na Kabila kwa masilahi yake binafsi.
Fayulu ambaye baadhi ya wanasiasa waliomuunga mkono nao wamebadili upande, huenda akajimwaga tena kwenye kinyanganyiro hicho, wakati utakapowadia.












