Kifo cha Rais John Magufuli: Hadithi ya rais ambaye alikabiliana na corona tofauti na dunia

Iliyochapishwa

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli akizindua mradi mkubwa wa barabara Februari 24, jijini Dar es salaam alijigamba kwa mafanikio yaliyofikiwa na chama cha mapinduzi CCM.

"Mradi ulikamilika kwa wakati kwa sababu hakuna aliyetumia corona kama kisingizio cha kucheleweha'' alisema akiwapongeza wahandisi na kuwaagiza maafisa wa serikali kutovumilia yeyote atakayetumia janga la corona kama kigezo cha kuchelewesha mradi.

Hii haikuwa na tofauti na uzinduzi uliopita ambapo alimalizia hotuba yake kwa msisitizo wa kauli mbiu yake ya HAPA KAZI TU.

"Tanzania ni tajiri,tuutumie utajiri wetu kuleta maendeleo ''alisisitiza na kuhimiza Watanzania kulipa kodi.

Siku tatu baadae Magufuli aliweza kuonekana hadharani kwa mara ya mwisho.

Tangu kuchaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2015 Magufuli alijipambanua kama mtu wa vitendo, tofauti na watangulizi wake.

Namna yake ya kutekeleza majukumu ikiwemo kutumbua majipu ilimpatia mashabiki wengi ndani na nje ya mipaka ya Tanzania hususan katika ukanda wa Afrika Mashariki ambako kampeni ya #WhatWouldMagufuliDo iliibuka na kupata umaarufu kwa kusifia utendaji wake usiokuwa na simile katika mapambano dhidi ya ufisadi na kusimamia miradi ya ujenzi wa miundo mbinu bila kuchoka.

Watanzania walizingatia zaidi mtindo mashuhuri wa uongozi wa Magufuli ambao ulikuwa mfano wa kusifiwa na viongozi wengine Barani Afrika.

Kipenzi cha watu

Wafuasi wake watakosa mikutano yake ya mara kwa mara alipokuwa ziarani nchini Tanzania ambapo alisimama mara kadhaa vituoni kuzungumza na wananchi.

Ziara hizo ambazo mara nyingi ziliibua udhaifu wa watendaji wa serikali zilitangazwa mubashara katika runinga na kupata umaarufu kwa wananchi wengi kutumia fursa hiyo kuelezea matatizo yao.

Umati wa wananchi uliuzunguka msafara wa rais na kumtazama kwa karibu akiwa amezungukwa na walinzi wake waliojihami kwa silaha.

Akisimama kwenye gari yake na kutumia kipaza sauti mikononi mwake Magufuli aliwasikiliza na kuwahoji kwa kina.

Majibu yalikuwa mchanganyiko, sheria mpya ingetangazwa, au afisa angetimuliwa kibarua au kushushwa cheo au aliyeuliza swali angepuuzwa.

Wapinzani wake kisiasa mataifa jirani na makampuni ya uchimbaji madini, mataifa ya magharibi na yeyote aliyeonekana kugusa maslahi ya Tanzania alilengwa na serikali yake.

Wakosoaji wake wanasema alikuwa dikteta ambaye hakuweza kuvumilia kukosolewa, wala utani wa wasanii wa muziki ,wachekeshaji au watumiaji wa mitandao ya kijamii.

Alisababisha hofu nchini humo ambapo hata kutojulikana kwake alipo kwa zaidi ya majuma mawili sera zake tata ziliendelea kutekelezwa ikiwemo polisi kuwakamata watu waliozusha kuhusu wapi alipo rais au kuuliza yuko wapi raisi Magufuli?

Hali hii ya mambo imekuwa ikipingana na namna alivyojipambanua kama mtetezi wa utu wa Watanzania.

Soma zaidi John Magufuli:

Alivishughulikia vyombo vya habari kwa kufungia magazeti kadhaa vituo vya radio na runinga na majukwaa ya mitandao ya kijamii kwa kuripoti kinyume cha matakwa ya serikali.

Alikosolewa kwa kutekeleza sera iliyowazuia wasichana waliopata ujauzito wakiwa shuleni kurejea katika mfumo rasmi wa elimu baada ya kujifungua.

Lakini amekosolewa Zaidi kwa namna alivyoshughulikia janga la Corona.

Hivi karibuni alibadili msimamo wake wa awali kuhusu uwepo wa Corona nchini Tanzania hatua iliyoshangaza akiunga mkono ushauri wa kisayansi uliotolewa mapema wakati wa mlipuko wa janga hilo.

Magufuli, aliyewahi kuwa mwalimu wa somo la Kemia baadae alieleza wasiwasi wa kuwepo njama za kuidhuru Tanzania alipotilia shaka usalama wa barakoa na chanjo.

Wakati mmoja alituma sampuli za papai na nyama ya mbuzi kufanyiwa vipimo vya Corona na kutumia matokeo ya uchunguzi huo kupinga uwepo wa virusi vya Corona.

Gharama ya kupuuzwa kwa janga hilo inaweza kubainika katika idadi ya watu waliopoteza maisha.

Viongozi Imara au Taasisi Imara

Kutakuwa na mjadala mkali nchini Tanzania kuhusu urithi aliouacha Magufuli na ikiwa mrithi wake ataweza kumuenzi au atabadilika.

Suala la mjadala haliepukiki ikiwa Bara la Afrika linahitaji viongozi imara au taasisi imara.

Magufuli anatazamwa na wengi kutokana na kutokuzuiwa na sharia za kitaasisi.

Alitoa amri na mambo yalitokea na kwa raia wengi ambao walikuwa wamefadhaika na kutokuwa na Imani na serikali, walifurahishwa.

Lakini sawa na Waafrika wengi wanaotaka kuishi katika nchi zinazotegemea sheria, kufurahiya maisha ya utu yasiyo na ukatili, kuwa na viongozi wanaosimamia uaminifu na ukweli, na serikali inayowaheshimu na isiyoficha habari kuhusu afya ya rais wao.