Virusi vya corona: Sababu za nywele kudondoka na tiba yake

Iliyochapishwa

Kudondoka kwa nywele kwasababu ya virusi vya corona kawaida huwa ni kwa muda tu.

Mwanafunzi wa chuo kikuu Janaina Corrêa, 24, alipata virusi vya corona Macapá kasakazini mwa Brazil, Aprili 2020, wakati tu ugonjwa huo ndio unaanza kuingia nchini humo.

Alikuwa na homa ya wiki mbili, kichefuchefu na kushindwa kupumua. Lakini dalili za ugonjwa huo hazikuishia hapo.

Pia alikuwa na uchovu na akaanza kubaini kwamba nywele zake zinadondoka. Hali yake ikaanza kuwa mbaya na tayari alikuwa amepoteza wajomba zake wawili waliofariki dunia kwa ugonjwa wa corona, mama yake alikuwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi pia kwasababu ya ugonjwa huo.

"Ulikuwa unahitajika kusubiri kwa saa 24 kujua vile mama yako anavyohisi. Ndani ya hospitali nikaanza kubaini kuwa nywele zangu zinadondoka. Nilikuwa na nywele nyingi lakini ni kawa naogopa, "anasema.

Mama yake akafanikiwa kupata nafuu lakini pia naye nywele zake zikaanza kudondoka baada ya kupata maambukizi.

Sababu zinazoweza kuchangia nywele kudondoka

Ugonjwa wa covid-19 kwa muda mrefu umehusishwa na sababu mbili mbaya zinazochangia nywele kudondoka.

Kulingana na Paulo Criado, mratibu wa idara ya magonjwa anayotibiwa bila kufanyiwa upasuaji nchini Brazil, matatizo ya hisia na magonjwa ya kuambukiza kunaweza kusababisha nywele kudondoka.

Pia kuna wagonjwa wenye matatizo ambayo ni urithi wa kijenetiki au magonjwa yanayotokea kwa sababu ya mfumo wake wa kinga kushambulia chembe fulani za mwili.

Kupitia BBC News Brazil, Criado ameelezea kuwa ni kawaida nywele kudondoka miezi kadhaa baada ya kupata ugonjwa mbaya wa kuambukiza kama vile dengue, chikungunya au Zika, pia baada ya kuwa na msongo wa mawazo, kupunguza uzito na kupata mtoto.

"Kile kinachoaminika sasa hivi ni kwamba virusi vya corona ni sehemu ya kundi hili la magonjwa ambalo linahusishwa na kudondoka kwa nywele," amesema.

Vile ugonjwa wa corona unavyoweza kuathiri kudondoka kwa nywele

Kazi ya nywele ni zaidi ya kile tunachoweza kufikiria: zaidi ya kushika, kuhisi na kulinda mashimo ya ngozi dhidi ya mionzi.

Inakadiriwa kuwa kila mwanadamu ana karibu mizizi milioni 5 ya nywele ambayo husambaa katika mwili mzima wa mwanadamu huku karibu 100,000 ikiwa kwenye ngozi ya kichwa.

Kwa ujumla mzunguko huo wa ukuaji wa nywele unadumu kutoka miaka miwili hadi saba na hugawanywa katika awamu tatu.

Kwanza, nywele hukua kwa karibu sentimita moja kwa miaka mitatu kwa wastani.

Kisha inachukua wiki mbili au tatu na inaaacha kukua na kujitayarisha nafasi yake ichukuliwe na nywele nyingine.

Awamu ya tatu na ya mwisho, nywele hutulia tu na inachukua karibu miezi mitatu au minne. Hapo ndipo nywele huanza kudondoka na kuondolewa na nywele mpya ambayo inakua katika shimo lile lile na nywele ya zamani.

Kila mmoja kawaida anapoteza nywele 30 hadi 150 kwa siku. Lakini ukiwa na magonjwa nywele zinaweza kudondoka karibu 300 kwa siku.

Inapotekea kudondoka kwa nywele kiasi kikubwa namna hiyo kunatokana na ugonjwa wa corona, muda wa kupata maambukizi hadi kuanza kudondoka kwa nywele umebainika.

Kudondoka kwa nywele mara nyingi kunatokea miezi mitatu baada ya kutokea kwa kisababishi na kunaweza kudumu kwa miezi mitatu hadi sita.

Dhana ya kudondoka kwa nywele

Katika utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Wyne na hospitali ya Henry Ford, kati ya wagonjwa 552 waliopata maambukizi ya virusi vya corona kati ya mwezi Februari na Septemba 2020, wagonjwa 10 walikuwa wanadondoka nywele kwasababu ya ugonjwa huo ambapo 9 kati yao walikuwa wanawake.

Utafiti huo ulionesha kwamba sababu za kudondoka kwa nywele kama vile za kisaikolojia na msongo wa mawazo.

Je tiba ya nywele kudondoka ni ipi?

Hadi kufikia sasa, hakuna dalili zozote kwamba kudondoka kwa nywele kutokana na ugonjwa wa corona kuna hitaji matibabu maalum.

Kwanza, ni muhimu kuweka wazi kuwa ni jukumu la mtaalamu wa ngozi kubaini tatizo na kutibu.

Hili litategemea na historia ya kila mgonjwa na kiwango ambacho nywele zimedondoka.

Chama cha tiba ya ngozi Brazil kimeonya dhidi ya hatari ya kujitibu mwenyewe kwasababu hatua hiyo inaweza kuathiri afya yako.

Kwa ujumla, iwapo nywele zitadondoka kwasababu ya ugonjwa fulani mfano corona, zitamea zenyewe tatizo litakapomalizika.