Waridi wa BBC: Mtanzania aliyetoka kwenye ufukara mpaka kuwa milionea kwa kutobagua kazi

Zahra Datani

Chanzo cha picha, Zahra Datani

Maelezo ya picha, Ilikuwaje hadi akafanikiwa?
    • Author, Anne Ngugi
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Iliyochapishwa

Zahra Datani ni mwanamke ambaye amefanikiwa kujinasua kutoka maisha ya ufukara hadi kupata utajiri kujitegemea na hata kuwasaidia wengine.

Ni jambo ambalo hakulitarajia wakati mmoja alipokuwa mdogo.

Ilikuwaje hadi akafanikiwa?

Familia yenye watoto wengi

Zahra alizaliwa kwenye maisha ya ufukara katika eneo la Itoma, Bukoba katika mkoa wa Kagera.

Anasema baba yake mzazi aliwaoa wake wengi na alijaliwa watoto wengi pia, kwa jumla wakiwa 21.

Hili lilifanya vigumu kwake kumudu mahitaji ya watoto wake.

Bi Zahara anasema kuwa mamake ndiye aliyechukua majukumu ya malezi kwa kulima shamba alilogawiwa na baba.

Bi Zahra anakumbuka kuwa kwenda shuleni ilikuwa kibarua kigumu sana - mama alihangaika kwa kiasi cha kutokuwa na uwezo wa kununua mafuta taa ya kutumiwa kwenye kibatari nyumbani.

Zahra Datani

Chanzo cha picha, Zahra Datani

Matumizi ya kila siku yalisumbua sana

"Ilifika wakati mama hangemudu hata taa ya kutoa mwanga usiku na ilibidi atushikie vigingi vya moto, anawasha anatusimamia tule haraka na kisha dada mkubwa anamshikia mama naye ili ale," anakumbuka Zahra.

Mama alihangaika sana hata kuwapeleka shuleni dada zake waliomtangulia kwani yeye ni mtoto wa tano.

Sehemu ya maisha ya mama ilikuwa kulima shamba ili kupata angalau fedha za kuwanunulia mahitaji ya shule kwa mfano sare na mikoba ya kubebea vitabu.

Wakati wake wa kwenda shule, anakumbuka, mama yake akihangaika sana hata kununua sare za shule.

Kwa kuwa mama hangemudu kila kitu ilibidi aende shuleni bila viatu jambo ambalo halikuwa kawaida shuleni mwao wakati huo.

Hisani kutoka kwa jamaa

Ndugu za mama walipoona mama anahangaika sana walimchukua Zahra kwenda kuishi nao.

Alipofika darasa la nne, dada wakubwa walikuwa wamefanikiwa kupata kazi, mmoja ya ualimu na mwingine muuguzi.

Walipata ahueni kwani dada zao walianza kuchangia matumizi ya nyumbani.

"Wakati huo dada waliungana pamoja na kunipeleka shule ya kibinafsi . Nikiwa kule shuleni nilikutana na watoto waliokuwa wametoka jamii za kitajiri," anakumbuka.

"Kilichoniumiza mno ni wakati mmoja wa wanafunzi aliyetambua jamii yangu aliwaeleza wanafunzi wenzangu kuwa nilikuwa nimetoka familia masikini sana.

"Ni jambo ambalo liliniumiza mno na pale kwenye bweni nikilia niliapa kuwa nitafanya kazi kwa bidii ili nisiishie kwenye maisha ya umasikini tuliyokuwa nao."

Zahara alimaliza shule na baadaye akafanikiwa kuajiriwa.

Alipoanza kazi alitamani maisha yake yabadilike sana. Alitamani watoto wake kupata elimu ya juu na kwa hivyo mmojawapo ya ndoto zake kuu ilikuwa watoto wake wasomee ng'ambo hususani Uingereza .

"Wakati ule nilipanga malengo ya kuniweka karibu na kusafiri Uingereza ili kufanikisha ndoto ya watoto wangu kupata elimu ya kiwango cha juu,"anakumbuka Zahra.

Alipofika darasa la nne, dada wakubwa walikuwa wamefanikiwa kupata kazi, mmoja ya ualimu na mwingine muuguzi.

Chanzo cha picha, Zahra Datani

Maelezo ya picha, Alipofika darasa la nne, dada wakubwa walikuwa wamefanikiwa kupata kazi, mmoja ya ualimu na mwingine muuguzi.

Safari ya kwenda Ulaya

Ndoto yake ya kusafiri Uingereza iliwadia na alisafiri Uingereza.

Zahra alidhania kuwa kusafiri ulaya maisha yangekuwa rahisi na ambayo hayana kuhangaika kwingi kama hali ilivyokuwa nyumbani kwao Tanzania.

Licha ya kuwa alikuwa ameajiriwa kazi za ofisini, pia alidhani kuwa akisafiri ng'ambo angepata kazi kwa haraka.

Ila alipowasili huko, alipata hali ilikuwa tofauti kabisa na matarajio yake.

"Nilipowadia UIaya ilikuwa kinyume na matarajio yangu. Wale watu waliokuwa wananisaidia kuanza maisha walikuwa ni watu tofauti na nilivyotarajia. Nilianza kusumbuka mno , kwani hata mahitaji ya msingi ilikuwa ngumu kuyatosheleza," anasema.

"Ule undugu niliokuwa natarajia na kutegemea kutoka kwa wenyeji sikupata. Walikuwa watu wenye roho ngumu kinyume na nyumbani nilikozoea watu wakarimu na wenye ushirikiano."

Dhiki ugenini

Mwanamke huyu anasema kuwa alihangaika sana miaka ya kwanza akiwa Uingereza.

Kitu ambacho anasema aligundua ni kuwa wengi kutoka bara Afrika ambao walisafiri huko na kuishi miaka mingi malengo yao makuu na mienendo yao ilikuwa tu ni kutafuta pesa na mali.

Ilibidi ahangaike kufanya kazi za mkono yaani vibarua kwani kazi za ofisi ni nadra sana kuajiriwa kama mgeni.

Kwa mfano aliajiriwa kazi za jikoni, kazi za kufanya usafi, kusimama jikoni kwa masaa mengi akisubiria kuosha vyombo vigahawani baada ya wateja kumaliza kula.

Isitoshe mwanamke huyu anasema kuwa wenyeji wake nchini Uingereza walimtesa sana.

Mama alihangaika sana hata kuwapeleka shuleni dada zake waliomtangulia kwani yeye ni mtoto wa tano.

Chanzo cha picha, Zahra Datani

Maelezo ya picha, Mama alihangaika sana hata kuwapeleka shuleni dada zake waliomtangulia kwani yeye ni mtoto wa tano.

Kwa mfano hakuwa anapewa ufunguo wa nyumba walimokuwa wanaishi, na kwa hivyo wakati mwingine angerejea nyumbani kutoka kwa vibarua vyake na kusimama nje ya nyumba kuwasubiri.

"Jambo lililonikera mno ni kuwa nilikuwa napigwa na kibaridi kizito cha Ulaya, nikiwasubiri warejee nyumbani sikuwa na jambo la kufanya. Wakati mwengine nilikuwa nasubiri muda wa saa mbili au tatu nikiwa nahisi kana kwamba nakufa ganzi mikono na miguu," anasema.

"Nilianza kujiuliza haya maisha ya Ulaya ndiyo nilikuwa nayatafuta kweli? Ila kwa ile nia yangu ya kutaka kufanikiwa niliendelea kuvumilia tu."

Katika pilkapilka hizo alikutana na watu wengine waliomuonyesha njia ya kupata kazi za kuwahudumia wazee Wazungu.

Anasema kuwa sio kazi rahisi kwani ilibidi awaoshe na kuwahudumia.

Nyakati nyingi anasema ni zile ambazo ilibidi awahudumie na kuhakikisha pia kuwa hawajajiendea haja ndogo wala haja kubwa.

Anasema utu wake ulimpelekea yeye kuipenda kazi ile na kuifanya kwa bidii ya mchwa .

Akiwa kwenye pilka pilka za kazi ile alianza kupata wazo la jinsi ya kujiendeleza mbele na ndiposa akaingia kwenye taasisi ambayo hutoa mafunzo kuhusu kuwatunza wazee na wagonjwa.

Alipofuzu alipandishwa cheo na kuwa meneja msimamizi wa kampuni.

Kampuni yenyewe ilikuwa inahusika na kuwatuma wafanyakazi katika makazi ya Wazungu ambao walikuwa wazee au wagonjwa.

Kuanzisha kampuni yake

Zahra Datani

Chanzo cha picha, Zahra Datani

Maelezo ya picha, Akiwa kwenye pilka pilka za kazi ile alianza kupata wazo la jinsi ya kujiendeleza mbele na ndiposa akaingia kwenye taasisi ambayo hutoa mafunzo kuhusu kuwatunza wazee na wagonjwa.

Kwa muda wa miaka mitano alifanya kazi ile kwa umakinifu mkubwa mno. Mwenyewe alitamani kufungua kampuni kama ile na baada ya kampuni aliyokuwa ameajiriwa kazi kuuzwa kwa mtu mwengine aliamua kutimiza ndoto hiyo.

Hilo lilitokea kipindi ambapo alikuwa amewasafirisha watoto wake hadi Uingereza.

Walikubaliana kufanya kazi katika kampuni aliyoifungua ya kuwatunza wazee na wagonjwa. Walianza kwa kuifanya kazi hiyo wenyewe kabla ya kuwaajiri watu wengine.

"Kufikia sasa ni miaka 11 tangu nilipofungua kampuni yangu ya kuwatunza wagonjwa na wazee. Tukianza ilikuwa ni mimi na wanangu tuliokuwa wafanyakazi ila kwa sasa tumewaajiri wafanyakazi wapatao mia tatu," anasema Zahra.

Anasema sasa mahangaiko na mateso ya tangu utotoni yamefutwa yasionekane tena.

Kwa mfano amemudu kununua nyumba ya kifahari nchini Uingereza na vilevile kumudu kuendesha gari la thamani kubwa.

Ila anasema kuwa kutokana na mateso na mahangaiko mengi sana hata alipokuwa anasafiri Uingrereza, amekuwa na moyo wa kuwasaida watu wanaohangaikia maishani pindi wanapofika kule.

Nchini Tanzania pia ameanzisha miradi mbalimbali kwa mfano ya maji na pia bishara ndogo ndogo kwa watu kuwawezesha kimaisha.

"Nimekuwa nikisaidia sana watu. Ninamoyo wa kuwasaidia watu hasa watoto yatima, watu wanaohitaji ajira na pia ninawasaidia watu wanaopania kwenda shuleni na hawana karo," anasema.

"Mimi ni miongoni mwa waanzilishi wa taasisi inayoitwa Jambo Bukoba inayosaidia shule kwa ujenzi wa madarasa , kununua sare na kadhalika. Haya yote mimi hufanya kusudi likiwa ni kubadili yale niliyoyapitia nikiwa mtoto."