Samuel Paty: Mwanafunzi akiri kumsingizia mwalimu wa Ufaransa aliyeuawa kwa kuonyesha vibonzo vya Mtume Muhammad

A protester wearing a face mask holds a sign in French that reads: 'I am Samuel'

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, kifo cha Samuel Paty kilisababisha
Iliyochapishwa

Samuel Paty alikatwa kichwa mwezi Oktoba baada ya kuwaonesha wanafunzi vibonzo vya Mtume Muhammad.

Msichana huyo, ambaye malalamishi yake yaliibua kampeni ya mtandaoni dhidi ya Paty, sasa amekiri kuwa hakuwepo darasani.

Kifo cha Bw Paty kiliishangaza Ufaransa na watu wengi walijitolea kuunga mkono mazishi yake na kufanya maandamano kote nchini humo.

Msichana huyo mwenye umri wa miaka 13, ambaye hakutajwa jina lake rasmi, awali alimwambia baba yake kuwa mwalimu Paty aliwataka wanafunzi Waislamu kuondoka darasani wakati alipokuwa akionesha katuni wakati wa somo la uhuru wa kujieleza na kukufuru.

Kulingana na ushahidi uliotolewa na msichana huyo ulioangaliwa na vyombo vya habari vya Ufaransa alisema: "Sikuona vibonzo, alikuwa ni msichana mwingine darasani kwetu ambaye alinionesha mimi hivyo vibonzo."

"Alidanganya kwasababu alihisi amekwama kwani wanafunzi wenzake walimuomba awe msemaji wao ," wakili wake, Mbeko Tabula, tameliambia shirika la habari la AFP. Msichana wa shule nchini Ufaransa amekiri kusambazamadai ya uongo kuhusu mwalimu kabla ya kuuawa mwaka jana.

Baba yake msichana huyo aliwasilisha malalamishi ya kisheria dhidi ya mwalimu na kuanza kampeni ya mitandao ya kijamii juu ya tukio kwa misingi ya ushahidi aliopewa na binti yake. Alimtambua Paty na shule ya Conflans-Sainte-Honorine, magharibi mwa Paris.

Waendesha mashitaka walisema muda mfupi baada ya mauaji kulikuwa na kiunganishi ''baina ya uchochezi wa kimtandao dhidi ya Paty na mauaji yake.

Muhusika wa mauaji hayo Abdullakh Anzorov mwenye umri wa miaka 18, alipigwa risasi na kuuawa na polisi muda mfupi baada ya shambulio.

Imebainika kuwa kampeni dhidi ya mwalimu huyo wa Jiografia na historia ilitokana na ushahidi wa uongo wa kile kilichotokea darasani siku chache awali.

Kama alivyofanya katika masomo sawa na hayo kuhusu uhuru wa kujieleza katika maiaka ya nyuma, Paty aliwaonya wanafunzi kuwa alikuwa anakaribia kuwaonesha picha ya Muhammad.

Alisema kwa yeyote anayehisi kuwa inaweza kumkwaza anaweza kufunga macho yake.

Msichana huyo awali alikuwa amedai kuwa mwalimu aliwataka wanafunzi Waislamu kuondoka katika chuma cha darasa. Alipokataa alifukuzwa shule, alisema.

Sasa inaonekana kuwa msichana huyo alikuwa amefukuzwa shule siku moja kabla ya somo hilo kutolewa, kulingana na gazeti la Paris- Le Parisien ,kwasababu ya kukosa kuhudhuria masomo mara kwa mara.

Msichana huyo anaelezea katika ushahidi wake uliopatikana kimakosa kwamba alitunga hadithi hiyo ya uongo ili kutomsikitisha baba yake. Alituma video mbili kwenye mitandao ya kijamii kujibu madai hayo.

Akizungumza na Redio ya Ufaransa Jumanne, wakili wa familia ya Paty alisema kuwa familia ya msichana ilitambua kuwa hakuwa darasani siku ile inayotajwana kwanini alikuwa amefukuzwa shule.

"Kwahiyo kuja na kusema sasa, samahani, Ninaamili binti yangu alisema uongo, huo ni udahifu kusema ukweli ," Virginie Le Roy aliiambia redio RTL.

Katika tukio jingine tofauti, maprofesa wawili wa chuo kikuu wamepewa ulinzi wa polisi baada ya kushutumiwa kuwa na chuki dhidi ya Uislamu na wanafunzi waandamanaji.

Uchunguzi umeanza baada ya mabango kutundikwa katika Chuo kikuu cha Sciences Po kilichopo Grenoble yaliyoandikwa "Fashishi wako katika kumbi zetu za masomo, chuki dhidi ya Uislamu inaua ", yakiwataja maprofesa hao kwa majina.

Waziri mdokgo wa mambo ya ndani Marlène Schiappa amesema kuwa maisha yao yamo hatarini na kampeni hiyo inachochea mateso aliyopitia Samuel Paty.

"Hatuwezi kuvumilia kitu cha aina hii," alisema.

Baada ya mauaji ya Paty Rais Emmanuel Macron aliipatia familia ya mwalimu huyo tunu la heshima ya juu ya taifa, inayofahamika kama Légion d'honneur.

Michoro ya Mtume Muhhamad ni mwiko katika dini ya Uislamu, na inachukuliwa kama kosa kubwa kwa Waislamu.

Suala hilo ni guhu hususan nchini Ufaransa kwasababu ya uamuzi wa jarida la Charlie Hebdo kuchapisha vibonzo vya Mtume Muhammad.

Wat kumi na wawili waliuliwa na waislamu wenye itikadi kali katika ofisi za jarida hilo mwaka 2015 baada ya kuchapisha picha hizo.

Mauji ya Charlie Hebdo na kukatwa kichwa kwa Samuel Paty yalileta mshituko kwa taifa hilo ambalo halifuati misingi ya dini - au laïcité - katika misingi ya utambulisho wa taifa.

Chini ya msimamo huo, taifa haliwezi kuingilia katika masuala ya kidini, na hivyo basi haliwezi kukabiliana na kujieleza kwa mtu kwa minajili ya kulinda hisia za jamii.