Bintimfalme Latifa: UN yasema haina ushahidi kwamba mwana wa mtawala wa Dubai Sheikh Maktoum yuko hai

Bintimfalme wa Dubai Sheikha Latifa kabla ya jaribio lake la kutaka kutoroka
Maelezo ya picha, Bintimfalme wa Dubai Sheikha Latifa kabla ya jaribio lake la kutaka kutoroka
Iliyochapishwa

Umoja wa mataifa unasema kwamba haujaona ushahidi kwamba mwana wa mtawala wa Dubai yuko hai, wiki mbili baada ya kuomba ushahidi kutoka kwa UAE.

Bintimfalme Latifa Al Maktoum alijaribu kulitoroka taifa hilo 2018.

Katika kanda iliosambazwa na BBC Panorama, anadai kwamba makamanda walimpatia dawa ya kulevya alipokuwa akitoroka kwa kutumia boti kabla ya kumrudisha kizuizini. Mawasiliano yake tangu wakati huo yamepotea.

Kanda hiyo ya bintimfalme Latifa ilisababisha uchunguzi wa Umoja wa mataifa.

Mwezi uliopita , Umoja wa mataifa ulithibitisha kwamba uliiomba UAE kutoa ushahidi kwamba bi Latifa yu hai.

Lakini siku ya Ijumaa, ulisema kwamba hakuna hatua iliopigwa kufikia sasa.

Msemaji Robert Colville alisema kumekuwa na mikutano mingi na ujumbe wa UAE mjini Geneva, Switrzeland, lakini alipoulizwa iwapo thibitisho la kuwa hai limepokewa alijibu : bado.

Babake Latifa, Sheikh Mohammed Bin Rashid Al Maktoum, ni mmoja wa viongozi matajiri zaidi duniani.

Dubai

Chanzo cha picha, Getty Images

Je tunajua nini kuhusu Latifa?

Kupitia usaidizi wa marafiki, Princess Latifa anasema kwamba alijaribu kutoroka Dubai ili kuanza maisha mapya mnamo mwezi februari 2018.

''Siruhusiwi kuendesha gari, kabisa'', alisema katika kanda ya video iliorekodiwa muda mfupi kabla ya kutoroka.

Lakini siku chache baadaye, mwanamfalme huyo anasema alikamatwa na makomando katika boti moja katika bahari Hindi. Alisafirishwa hadi Dubai ambapo amekuwa tangu wakati huo.

Babake alisema kwamba alichukua hatua hiyo kumlinda.

Taarifa kutoka kwa ufalme wa Dubai mwezi uliopita ilisisitiza Kwamba alikuwa anaangaliwa nyumbani.

"Sheikha Latifa anaendelea kupona na tunataraji atarudi katika maisha ya kawaida wakati ufaao'', ilisema.

Kwa kutumia simu ambayo alipatiwa mwaka mmoja baada ya kukamatwa , bi Latifa alirekodi baadhi ya video kwa miezi kadhaa.

Alirekodi kanda hizo za video akiwa msalani kwa kuwa ndio eneo ambalo lilikuwa mlango pekee ambao angeweza kuufunga.

Bintimfalme Latifa na babake Sheikh Makhtoum kulia

Chanzo cha picha, Getty Images/PRINCESS LATIFA

Maelezo ya picha, Bintimfalme Latifa na babake Sheikh Makhtoum kulia

Katika kanda hizo aliandika alipigana na wanajeshi waliojaribu kumchukua katika boti hiyo akiwapiga mateke na ngumi na kumngata mkononi komando mmoja hadi akapiga kelele.

Baada ya kudungwa sindano ya kutulizwa , alipoteza fahamu alipokuwa akipelekwa katika ndege ya kibinafsi na hakuamka hadi ilipowasili Dubai.

Alikuwa akizuiliwa pekee bila ya kuweza kupata matibabu ama usaidizi wa kisheria katika nyumba moja ya kifahari ambayo milango na madirisha yake yalikuwa yamefungwa na kulindwa na polisi.