Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Netanyahu aishutumu Iran kuhusika na mlipuko dhidi ya meli ya Israel katika Ghuba ya Oman
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ameilaumu Iran kwa mlipuko ulioharibu meli inayomilikiwa na Israeli katika Ghuba ya Oman wiki iliyopita.
MV Helios Ray, ilikuwa ikisafiri kutoka Saudi Arabia kwenda Singapore wakati mlipuko uliripotiwa kutoboa mashimo pande zote mbili za chombo hicho
"Kwa kweli hii ilikuwa operesheni iliyotekelezwa na Iran. Hiyo ni wazi," Bw Netanyahu aliiambia Redio ya Kan, bila kutoa ushahidi wowote.
Wizara ya mambo ya nje ya Iran ilisema inapinga vikali shutuma hizo.
Matamshi ya Bw Netanyahu yalitangazwa saa chache baada ya kundi la ufuatiliaji kuripoti kwamba mashambulio ya makombora ya Israeli yalikuwa yamelenga vikosi vya Iran huko Syria.
Bado haijulikani ni nini kilisababisha mlipuko ulioharibu Helios Ray Alhamisi usiku. Lakini mmiliki wa meli hiyo, Rami Ungar, alisema kuwa iliacha mashimo mawili yenye kipenyo cha 1.5m (4.9ft), juu tu ya njia ya maji.
Yoav Galant, waziri wa baraza la mawaziri la Israeli, aliiambia Ynet TV kwamba picha za bodi ya chombo hicho zilidokeza uharibifu huo kuwa ni matokeo ya "bomu, lililobandikwa kwa nje, katika operesheni ya makomandoo wa majini wa usiku ".
Alibainisha kuwa shambulio hilo lilitokea karibu na pwani ya Iran na kwamba wahusika walitambua kutoka hifadhi data inayopatikana hadharani kuwa chombo hicho kilikuwa cha Israel.
Mnamo 2019, Iran ilishutumiwa kuhusika na milipuko ambayo iliharibu meli kadhaa za mafuta katika Ghuba ya Oman. Wanajeshi wa Marekani walisema milipuko hiyo ilisababishwa na mabomu yaliyounganishwa kwa sumaku na kunasishwa kwenye bodi ya meli.
Iran ilikana kuhusika kwenye shambulio hilo na kukataa mashtaka ya Bw Netanyahu Jumatatu.
"Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman ni maeneo ya usalama wa haraka wa Iran. Hatutawaruhusu kueneza hofu," msemaji wa wizara ya mambo ya nje Saeed Khatibzadeh aliuambia mkutano wa waandishi wa habari.
"Netanyahu ana hofu na Iran na anafikiria njia ya kusuluhisha shida zake za nyumbani ni kueneza shutuma kama hizo. Israel inajua vizuri kwamba jibu la Iran litakuwa la kiufundi na sahihi kuhusu usalama wa kitaifa."
Alipoulizwa ikiwa Israel italipiza kisasi, Bwana Netanyahu alijibu: "Unajua sera yangu. Irani ni adui mkubwa wa Israeli. Nimeazimia kuizuia. Tunashambulia eneo lote."
Mahojiano ya Kan na Waziri Mkuu yalirekodiwa Jumapili usiku, saa chache kabla ya nchi jirani ya Syria kusema ilikuwa imekataa shambulio la kombora la Israeli.
Shirika la habari la serikali ya Syria, Sana, limetaja chanzo cha kijeshi likisema ndege za Israel zilirusha makombora kutoka Milima ya Golan kuelekea "baadhi ya maeneo karibu na Damascus". vyombo vya ulinzi wa anga vilizuia makombora mengi na kuyapiga risasi , chanzo kiliongeza.