Watu 16 wauawa kwa shambulio linalodaiwa kutekelezwa na waasi DRC

Ramani ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo
    • Author, Mbelechi Msoshi
    • Nafasi, BBC, DRC
  • Iliyochapishwa

Raia kumi na sita wameuawa jimboni Ituri Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokraisia ya kongo baada ya shambulio yaliodaiwa na waasi toka Uganda wa ADF.

Akizunguza na BBC , mbunge mchaguliwa wa jimbo hilo Iracan Gratien, amesema waasi walishambulia kijiji cha Ndala wilayani Irumu jana na kuchoma moto kanisa moja.

Lakini mbunge huyu amesma, hadi sasa hawajaweza kuthibitisha kama ni waasi wa ADF ndio waliotekeleza mauaji hayo, kwani jimbo hilo lina vikundi vingi vya waasi ambavyo lengo lao ni kupora na kuuza madini kwa njia haramu wakiungwa mkono na viongozi wa jeshi hata wafanya biashara wakubwa wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Duru toka eneo la tukio zinasema, waasi hawa walianza kwanza kushambulia vizuizui vya jeshi la nchi hiyo .

"Tulipewa taarifa ya kwamba raia waliuawa tena tena, na watu waliofanya vitendo vingi vibaya ni wengi hata wazawa wa jimbo hilo, watu walishakuwa na tamaa ya kuwa na pesa , nawaambia hata wanajeshi wako na mipango hio ya kutekeleza mauaji , wanawafungulia waasi njia baada ya kupewa pesa". Alisema

Kwa miaka kadhaa sasa, majimbo yanayokuwa na madini yanakabiliwa na uasi huku wachambuzi wengi wakikosoa wafanyabiashara kuwa sehemu ya vurugu hizo ili wauze madini kwa njia isiyo halali.

Jana pia, mji mkuu wa jimbo la madini la haut-Katanga Lubumbashi, lilishambuliwa na waasi wengine ambao walijaribu kuchukuwa udhibiti wa mahali pa kuhifadhi silaha na kambi mbili za vikosi maalum vya ulinzi wa jimbo hilo.

Jeshi la taifa lilitangaza kuwa waasi 12 waliuawa huku wakipoteza wanajeshi wao watatu pamoja na mtoto mmoja wa askari.