Gao Liu: Muigizaji wa China aonesha picha za pua yake baada ya upasuaji kwenda mrama

Chanzo cha picha, Sina Weibo/Gao Liu
Muigizaji wa China ameonya kuhusu hatari ya kufanya upasuaji wa mapambo kwa kusambaza picha za pua yake baada ya upasuaji kwenda mrama.
Gao Liu ni mwimbaji na muigizaji ambaye ameigiza katika filamu kadhaa na vipindi vya runinga na ameonekana kuwa nyota chipukizi. Lakini katika miezi ya hivi karibuni umaarufu wake umeshuka.
Akichapisha katika mtandao wa kijamii wa Weibo, alielezea kwamba kutokuwepo kwake kwa miezi kadhaa kulitokana na tukio moja la upasuaji wa mapambo ambao umewacha ncha ya pua yake kukatika.
Picha za kutisha zilifuata
Bi Gao alisambaza picha zake kwa wafuasi wake milioni 5 na kuzua mjadala kuhusu upasuaji wa mapambo ambao ni maarufu sana nchini China.
Alisema kwamba mwezi Oktoba , rafikiye mmoja alimpeleka kwa daktari mmoja wa upasuaji wa mapambo katika kliniki iliopo kusini mwa mji wa Guangzhou.
Muigizaji huyo alisema kwamba aliamua kufanya upasuaji huo katika pua yake kutokana na pendekezo kwamba ingepunguzwa kidogo na alidhani kwamba mpango huo ungemsaidia kuimarisha kazi yake.
''Upasuaji wote ulichukua saa nne. Nilifikiri katika saa hizi nne nitafanywa kuwa mrembo'' , aliwaambia wafuasi wake.

Chanzo cha picha, Sina Weibo/Gao Liu
"Sikutarajia kwamba saa hizo nne ndo zingekuwa mwanzo wa masaibu."
Alisema kwamba baada ya upasuaji huo, pua yake ilikuwa inawasha na baadaye kupata maambukizi, licha ya kuambiwa kwamba angeweza kurudi kazini kufikia mwezi Desemba au Januari.
''Ngozi iliopo juu ya pua yangu ilianza kuwa nyeusi na nyeusi na pua kuonekana kama iliojeruhiwa'', alisema, akiongezea kwamba alifikiria kujiua.
Bi Gao alisema kwamba alilazimika kulazwa hospitalini kwa miezi miwili na kukosa $61,800 za kikazi.
Amesema kwamba haiwezekani kwa yeye kufanya upasuaji mwengine ili kutengeza pua yake kwa takriban mwaka mzima kutokana na kiwango cha uharibifu wa upasuaji huo.

Chanzo cha picha, Sina Weibo/Gao Liu
Gazeti maarufu la habari, The Paper limesambaza data hadharani kutoka hopsitali ya Wilaya ya Tianhe mjini humo,likionesha kwamba kliniki ambayo Bi Gao alitibiwa ilikuwa tayari imepigwa faini kati ya mwezi Machi na Otoba 2020. Haijulikana ilikiuka sheria gani.
Baadhi ya malalamishi yamewasilishwa serikalini kuhusu kliniki hiyo tangu Bi Gao kuzungumzia masaibu yake kulingana na gazeti hilo. Uchunguzi unaendelea.
Katika mitandao ya kijamii , baadhi ya watu wametaka wale wanaohusika katika upasuaji huo wa Gao kuwajibishwa.
Wengine wametaka kuwepo kwa sheria bora katika sekta ya upasuaji wa mapambo nchini China.
Upasuaji wa aina hiyo umekuwa maarufu nchini China na kufikia kiwango kwamba mwaka 2004, taifa hilo liliwafanyia shindano malkia wa urembo waliokuwa wamepitia kisu hicho.
Shguhuli hiyo ni maarufu hususan miongoni mwa vijana wadogo.
Gazeti la South China Morning Post lilisema kwamba mwaka 2019, kwamba karibia thuluthi mbili za watu milioni 20 ambao walipitia upasuaji huo mwaka uliopita walikuwa chini ya umri wa miaka 30 na mmoja kati ya watano walikuwa chini ya umri wa miaka 21.
Gazeti hilo lilisema kwamba wanafunzi wengi wa shule ya upili walipendelea kufanyiwa upasuaji huo kabla ya kuingia vyuo vikuu, wakiamini kwamba zitaimarisha fursa zao kazini na kupata wapenzi.
Lakini ongezeko la mahitaji ya upasuaji huo yamefanya baadhi ya kliniki kutekeleza operesheni bila vibali ama hata kuwaajiri madaktari wa upasuaji ambao hawajahitimu.
Hatahivyo haijulikani hali ilikuwa vipi katika kliniki ambayo Bi Gao alifanyiwa upasuaji huo.












