'Jinsi vidonge vya mpango wa uzazi vilivyotaka kuniua‘

A photo of Vanessa Centeno

Chanzo cha picha, VANESSSA CENTENO

Maelezo ya picha, Vanessa Centeno: 'Nilifikiri kuwa nimepata mshutuko wa moyo'.
Iliyochapishwa

Vanessa Centeno alipobaini kuwa ana damu iliyoganda inayoziba mapafu yake ilikuwa kitu kigumu sana kwake kukikubali.

Lakini alipobaini chanzo chake hicho ndicho kilichomkanganya zaidi.

Mwaka 2019, mwanamke huyo aliyekuwa anaishi Boston, kama mamilioni ya wanawake wengine duniani alikuwa akitumia dawa za kupanga uzazi.

Lakini tofauti na wanawake wengine, Venessa alianza kudhurika kwa kutumia vidonge kama njia ya mpango wa uzazi - damu ikaanza kuganda anachosema kuwa kilibadilisha kabisa maisha yake.

A woman holding on to her chest in pain

Chanzo cha picha, Getty Images

'Nilianza kufikiria kuwa nimepata mshutuko wa moyo'

"Nilikuwa ninatembea kwenye ngazi na ghafla pumzi zikaanza kubana hadi nikaanza kushika kijisanduku cha kuweka barua kwa sababu sikuweza kupumua," Vanessa anakumbuka.

"Sijawahi kuhisi kupoteza pumzi namna hiyo na nilikuwa ninajitahidi kwa kila namna niweze kupata hewa safi."

Licha ya kushuhudia tatizo hilo, Venessa aliamua kwenda kazini lakini akatoka mapema ili akamuone daktari.

"Walinipatia dawa ambayo inatakiwa kufungua njia ya kuingiza hewa. Nikaanza kupata nafuu na kuanza kupumua kiasi. Walinipiga picha na kusema kuwa wameona kitu kama kivuli kwenye mapafu yangu uwezekano wa kwamba lilikuwa tatizo la uvimbe kwenye mapafu au nimonia,"

Lakini kilichofuata, kliniki hiyo ikamuarifu Vanessa kwamba haukuwa ugonjwa wa mapafu na alihitaji kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu zaidi.

Hata hivyo, Vanessa hakuweza kuonana na daktari kwa karibu mwezi mzima, hali yake ikaanza kudorora na kliniki hiyo ikamshauri aanze kutumia bomba la dawa ya kupitisha oksijeni dawa inayotumika na wagonjwa wa pumu.

"Lakini hali hiyo ikatokea tena," anasema.

"Nilikuwa ninapanda ngazi na kushuka nikiendelea na kazi zangu za nyumbani kama kawaida lakini ghafla nikaanza tena kupata matatizo ya kupumua na nikaamua kufungua upande mmoja wa nguo ili nipate hewa safi lakini kilichofuata nilianguka sakafuni."

"Mwili wangu ulikuwa unauma; tumbo langu, kifua changu, mikono yangu, vyote vilikuwa vinauma na hapo nikaanza kufikiria kuwa nimepata mshutuko wa moyo."

Vanessa hakwenda hospitali lakini akampigia daktari wake na hapo muuguzi akamuagiza kufika hospitalini haraka iwezekanavyo.

"Siku iliyofuata, nilikwenda kumuona daktari na kumueleza dalili zangu zote na baada ya kunikagua akataka nipigwe picha ya CT Scan, na hapo ndipo nilipoelekezwa kufika katika hospitali kubwa.

"Huko nikawekwa katika vifaa chungu nzima kufuatilia hali yangu, nikaanza kupewa matibabu kwa njia ya mishipa, yaani kila kitu kilitokea haraka sana kiasi cha kuanza kuchaganyikiwa."

"Ikabainika kuwa damu yangu imeganda kifuani na mgando huo umeanza kupasuka pasuka na kuziba mapafu yangu."

Vanessa alikuwa hospitali kwa siku mbili ndio akaruhusiwa kurejea nyumbani lakini akahitajika kupumzika nyumbani kwa wiki mbili.

Madaktari walisema kuwa sababu kubwa iliyochangia hali hiyo ni kubadilisha njia ya mpango wa uzazi na hicho ndicho kilichoonekana kama kitu kigeni mwilini mwake.

"Madaktari walimuarifu kuwa ikiwa angemaliza siku moja zaidi kuna uwezekano mkubwa angepoteza maisha kwa sababu hali yake ilikuwa mbaya," anasema.

Migando ya damu inaathiri wanawake kwa kiwango gani kwasababu ya mpango wa uzazi?

A photo of conceptive pills on a pink background

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Vidonge ni moja ya njia maarufu za mpango wa uzazi Ulaya, Australia na New Zealand

Ni nadra sana.

Kulingana na huduma ya afya ya taifa Uingereza, kuna visa kati ya 5 na 12 kati ya wanawake 10,000 ambao hupata tatizo la kuganda damu kwa mwaka.

Duniani, zaidi ya wanawake milioni 150 wanatumia vidonge kama njia ya mpango wa uzazi na ndio njia inayotumika sana Ulaya, Australia na New Zealand.

A photo of a woman lying on a sofa

Chanzo cha picha, Getty Images

Pia njia hiyo ni ya pili kwa umaarufu barani Afrika, Amerika Kusini na Amerika Kaskazini huku barani Asia ikiwa ya tatu.

Vidonge kama njia ya mpango wa uzazi kama nyingine yoyote ile ina athari zake zinazofahamika sana ambazo ni pamoja na hisia za kubadilika-badilika na ama kuongeza uzito au kukonda.

Kwa upande mwingine miongoni mwa athari zisizofahamika sana za utumiaji wa vidonge kama njia ya upangaji uzazi ni kuganda kwa damu ambako kunaweza kuhatarisha maisha.

Hatari ya wanawake kuanza kuganda damu kunasababishwa na homoni, umri, historia ya familia ya tatizo hilo na mtindo wa maisha kama vile uzito wa mwili na kuvuta sigara.

A photo of different forms of contraception on a pink background.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Vanessa aliwahi kutumia njia kadhaa za mpango wa uzazi ikiwemo upandikizaji

'Mfumo dume unatatiza wanawake'

Zaidi ya mwaka mmoja baadaye, Venessa bado hajaweza kurejelea maisha yake ya kawaida.

"Ghafla, nikawa na uvimbe wa damu kwenye mishipa ya mapafu na nikalazimika kuanza kutumia dawa kwa miezi sita pia nikalazimika kuwa makini nisianguke au kujikata kwa sababu chochote kile kinaweza kusababisha kuvuja damu kwa ndani."

"Kila wakati nalazimika kujikumbusha kwamba niko sawa na sasa siko katika hatari yoyote tena."

"Sijui kwanini ilitokea kwasababu nimekuwa nikitumia njia za mpango wa uzazi kwa kipindi kirefu."

"Niliwahi kutumia ile ya upandikizaji lakini ikawa inanifanya niongeze uzito sana."

Vanessa anasema kuishi katika dunia yenye mfumo dume kunafanya wanawake kubeba mzigo mzito ikiwemo kuhakikisha mwanamke unatumia njia angalau moja ya mpango wa uzazi.