Ajali ya ndege ya Sriwijaya: Wapiga mbizi wa Indonesia wakitafuta kisanduku cheusi cha ndege

Maelezo ya video, Wapiga mbizi wa Indonesia wakitafuta mabaki ya ndege iliyoanguka
Iliyochapishwa

Wanajeshi wa majini nchini Indonesia wametoa video ya wapiga mbizi wakianza tena shughuli ya utafutaji mabaki ya ndege ya abiria iliyotumbukia baharini wikendi pamoja na kisanduku cheusi.

Ndege ya shirika la Sriwijaya Air aina ya Boeing 737 iliondoka uwanja wa ndege wa Jakarta ikiwa na watu 62, lakini ikapotea kwenye rada ikiwa inaelekea kisiwa cha Borneo Jumamosi.

Timu za uokozi tayari zimepata mabaki ya ndege pamoja na ya binadamu.

Maafisa husika tayari wamebaini eneo kilipo kisanduku cheusi cha mawasiliano cha ndege hiyo lakini bado hawajakipata.

Afisa mmoja amesisitiza umuhimu wa shughuli ya utafutaji ambayo imeanza tena kazi hiyo Jumatatu asubuhi, na kuitaja kuwa ni operesheni ya saa 24.

"Itakuwa ni operesheni isiyokuwa na ukomo," Rasman MS, mkuu wa shughuli hiyo ya utafutaji na uokozi amezungumza na wanahabari.

"Sasa hakutakuwa na mapumziko. Itakuwa bora tukipata waathirika kwa haraka."

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, baadhi ya wafanyakazi 2,600 sasa wako kwenye operesheni inayohusisha boti kadhaa na helikopta ambazo zinatumika kubeba miili, mabaki ya ndege na nguo za abiria ndani ya bahari kina cha takriban mita 23.

Pia kuna zaidi ya meli 50 pamoja na ndege zingine 13 zenye kuhusika na operesheni hiyo ya kutafuta mabaki ya ndege yenye usajili SJ182.

Basarnas

Chanzo cha picha, Instagram/@Sar_Nasional

Maelezo ya picha, Shughuli ya utafutaji imeanza tena Jumatatu asubuhi

Inaonekana kana kwamba hakuna matumaini ya kupata manusura.

Mchunguzi wa Kamati ya Taifa ya usalama wa usafiri Indonesia amezungumza na shirika la habari la Reuters kwamba mamlaka ina matumaini ya kupata kisanduku cheusi cha mawasiliano Jumatatu.

Aliongeza kuwa kuna uwezekano ndege hiyo ilianguka na kukatika vipande vipande ilipogusa maji kwa kuzingatia mabaki yaliyopatikana.

"Kuna uwezekano ndege hiyo ilivunjika vipande vipande wakati inagusa maji kwasababu kama ingelipuka kwenye anga, vipande vyake vingekuwa vimesambaa sana," amesema urcahyo Utomo.

Wachunguzi tayari wanachunguza vifaa ambavyo vinaaminika kuwa gurudumu na sehemu ya kiwiliwili cha ndege.

Gurudumu kutoka moja ya injini pia ni miongoni mwa mabaki ambayo yamepatikana.

Ndege ya shirika la Sriwijaya Air aina ya Boeing 737 ilipoteza mawasiliano dakika nne baada ya kupaa

1px transparent line

Nini kilitokea katika ndege hiyo?

Ndege hiyo ya kampuni ya Sriwijaya Air aina ya Boeing 737 iliondoka uwanja wa ndege wa Jakarta saa 14:36 saa eneo Jumamosi.

Dakika kadhaa baadaye, karibu saa 14:40 mchana, mawasiliano ya mwisho ya ndege hiyo nambari ya usajili SJY182 yakarekodiwa, kulingana na wizara ya usafirishaji.

Kawaida, safari ya ndege kuelekea Pontianak, magharibi mwa eneo la Kalimantan, katika kisiwa cha Borneo ingechukua dakika 90.

Inasemekana kuwa ndege hiyo ilikuwa na abiria 50 wakiwemo watoto saba na watoto wachanga watatu - pamoja na wahudumu 12 wa ndege hiyo ingawa ilikuwa na uwezo wa kubeba watu 130.

Kila mmoja aliyekuwa kwenye ndege hiyo ni abiria wa Indonesia, maafisa wamesema.

Inadhaniwa kuwa ndege hiyo ilikuwa imepaa zaidi ya mita 3,000 chini ya dakika moja, kulingana na tovuti inayofuatilia safari za ndege Flightradar24.com

Walioshuhudia kisa hicho wanasema waliona na kusikia angalau mlipuko mmoja.

Kipi tunachokijua kuhusu ndege hiyo hadi kufikia sasa?

Ndege hiyo ambayo bado haijapatikana siyo 737 Max, aina ya Boeing ambayo ilikuwa imesitishwa kuendesha shughuli za usafirishaji kutoka Machi 2019 hadi Desemba baada ya kutokea kwa ajali mbili mbaya.

Kulingana na taarifa za usajili, ndege hiyo ya Boeing 737-500 ilikuwa imetumika kwa miaka 26.

Pia ndege hiyo ilikuwa katika ubora wake, Mkuu wa Shirika la Sriwijaya Irwin Jauwena amezungumza na wanahabari.

Na safari zilikuwa zimecheleweshwa kwa dakika 30 kwasababu ya mvua kubwa iliyokuwa inanyesha, amesema.

Indonesian Navy personnel carry debris believed to be from the Sriwijaya Air SJ-182 plane,

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Maafisa wa jeshi la majini wa Indonesia wakibeba mabaki yanayoaminiwa ni ya ndege ya shirika la Sriwijaya usaji SJ-182

Ndege hiyo ilianza kutojulikana ilipo takriban kilomita 20 kaskazini mwa mji mkuu wa Jakarta ikiwa sio mbali sana kutoka eneo ambapo ndege nyengine ilianguka Oktoba 2018.

Jumla ya watu 189 walifariki dunia wakati ndege ya Shirika la Indonesia Lion ilipotumbukia baharini takriban dakika 12 baada ya kuanza safari kutoka mji huo.

Sababu zilizosemekana kuchangia ajali hiyo ni pamoja na mapungufu kadhaa katika muundo wa ndege pamoja na kasoro zilizosababishwa na shirika la ndege na marubani.

Ilikuwa ni moja ya ajali mbili mbaya zaidi ambayo ilisababisha wadhibiti kusitisha Boeing 737 Max kuendesha shughuli zake za usafirishaji.