Uchaguzi wa Uganda 2021: Je, ni kipimo cha mamlaka, nguvu na majukumu kwa Tume ya Uchaguzi?

Maafisa wa tume ya uchaguzi nchini Uganda

Chanzo cha picha, Uganda Electoral Commission/facebook

    • Author, Markus Mpangala
    • Nafasi, Mchambuzi Tanzania
  • Iliyochapishwa

Uchaguzi wa tano wa mfumo wa vyama vingi nchini Uganda unatarajiwa kufanyika tarehe 14 Januari 2021, ambapo Tume ya uchaguzi nchini humo inamulikwa kila kona na wananchi, taasisi za kiraia za ndani pamoja na waangalizi wa Jumuiya ya Kimataifa kuona nguvu, mamlaka na shughuli za kusimamia uchaguzi huru na haki zinavyofanya kazi bila upendeleo au utageuka na kuandika historia mpya yenye 'kitanzi' kwa taifa hilo la Afrika mashariki.

Maeneo yanayozingatiwa kuwa kipimo kwa Tume hiyo ni kusimamia taratibu na uendeshaji wa uchaguzi katika ngazi tofauti, uwazi wa shughuli za Tume katika uhesabuji wa kura na uwasilishaji na utangazaji wa matokeo, kusimamia kampeni zenye usawa, kuzingatia sheria na kanuni za uchaguzi bila upendeleo.

Duru za kisiasa zinaonesha matumaini uchaguzi huu huenda utafuta taswira hasi iliyojengwa chini ya aliyekuwa Mwenyekiti wake, Mhandisi Badru Kiggundu ambaye aliongoza Tume hiyo kwa kipindi cha miaka 14 tangu mwaka 2002.

Taswira ya Tume ya Uchaguzi imekuwa ikihusishwa na upendeleo kwa chama tawala NRM cha Yoweri Museveni ambaye anagombea muhula wa sita, huku wanasiasa wa vyama vya upinzani kuanzia zama za galacha Kizza Besigye hadi Bobi Wine wamejenga dhana kuwa Tume hiyo inafanya jitihada kukisaidia chama tawala na kudidimiza nguvu zao, hivyo uchaguzi huu ni muhimu kujenga taswira mpya ya Tume hiyo chini ya Mwenyekiti Jaji Simon Byabakama.

Je, Tume hiyo inaundwa vipi na wahusika ni akina nani?

Katiba ya Uganda ya mwaka 1995 inaipa mamlaka na nguvu kisheria Tume hiyo chini ya Ibara 16 ambayo imetaja majukumu, mipaka na nguvu zake katika shughuli za uchaguzi mkuu. Malengo makuu ya Tume hiyo ni kusimamia mchakato mzima wa demokrasia na utawala bora. Kwa mujibu wa sheria imekabidhiwa majukumu yafuatayo;

Mosi, kuendesha, kusimamia uchaguzi mkuu katika ngazi mbalimbali na kura za maoni.

Pili, kuhakikisha inasimamia taratibu za uchaguzi huru na haki kama inavyoelekezwa na katiba ya nchi hiyo, pamoja na kuunga mkono ustawi wa demokrasia nchini humo.

Tatu, kuandikisha na kutunza taarifa za wapigakura; kutenga nafasi za makundi maalumu na idara za uongozi. Kusajili, kuhifadhi na kuboresha taarifa katika daftari la wapigakura.

Nne, Tume imeagizwa na sheria kutoa elimu ya uraia na mipango inayohusu masuala ya uchaguzi mkuu kupitia wadau, taasisi za elimu za umma na binafsi, asasi za kiraia.

Tano, kutunga na kufundisha elimu kwa wapigakura na programu zinazohusu uchaguzi mkuu,kura za maoni pamoja na taratibu zake ili kuenzi demokrasia.

Sita, kufanya tathmini na kutoa mapendekezo ya kutunga na kubadilisha sheria, taratibu na kanuni za uchaguzi kadiri inavyohitajika kulingana na mazingira na wakati.

Saba, kusikiliza, kuendesha na kuamua mashauri yote yanayowasilishwa na wagombea kabla na wakati wa uchaguzi mkuu.

Nane, kukusanya, kuchapisha na kutangaza matokeo ya uchaguzi ya ngazi zote kuanzia urais na wawakilishi wa majimbo.

Tisa, kuajiri watumishi wa Tume na kutoa mafunzo kwa wasimamizi wote wa uchaguzi mkuu katika ngazi mbalimbali. Nafasi hizo hutangazwa kwa umma na kuwataka raia wenye sifa kuwasilisha maombi yao.

Tume ya uchaguzi ni huru na haipokei maelekezo kutoka taasisi yoyote wakati wa kutekeleza majukumu chini ya Ibara 62 ya Katiba ya Uganda. Bunge linahakikisha linapitisha bajeti ya Tume ya uchaguzi kwa mujibu wa Ibara ya 66 ya Katiba.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Uganda kwa sasa ni Jaji Simon Byabakama. Aliteuliwa kuongoza Tume hiyo Novemba 18, mwaka 2016. Mnamo Agosti 9 mwaka 2017 alikula kiapo cha kuwa Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Vitambulisho ya Taifa kwa mujibu wa sheria.

Ni uchaguzi mpya, Mwenyekiti mpya

Wakati Kizza Besigye akipambana na Yoweri Museveni katika chaguzi za mwaka 2001, 2006, 2011 na 2016 Tume ya Uchaguzi iliongozwa na Badru Kiggundu. Mwenyekiti huyo alikabidhiwa jukumu la kuongoza Tume hiyo mwaka 2002 na tangu hapo amesimamia chaguzi tatu ambazo chama cha NRM kilitangazwa kushinda dhidi ya Besigye.

Uchaguzi wa mwaka 2021 utashuhudia mwenyekiti mpya wa Tume Jaji Simon Byabakama akijenga taswira mpya au kubomoa zaidi mbele ya umma na jumuiya ya Kimataifa.

Mwenyekiti huyo anasimamia uchaguzi wa mwaka 2021 ukiwa wa kwanza kwake tangu alipochukua cheo hicho kutoka kwa Badru Kiggundu ambaye aliongoza kwa kipindi cha miaka 14, ikiwa ni mihula miwili kwa mujibu wa sheria.

Mwenyekiti wa Tume huongoza kwa miaka 7 na endapo akiongeza muhula mwingine ndipo hufikisha miaka 14 madarakani, lakini mamlaka za uteuzi zinaweza kubadili mwenyekiti iwapo itaidhinishwa na Bunge.

Je, ni upi udhaifu wa Tume ya Uchaguzi?

Kama zilivyo nchi zingine barani Afrika linapofika suala la uchaguzi mkuu, Uganda nayo imekuwa ikishuhudia malumbano makali juu ya mamlaka, nguvu na uaminifu wa Tume katika mchakato mzima wa demokrasia.

Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa kumekuwa na uhaba wa uhuru katika Tume yenyewe na miongoni mwa viongozi wanaotajwa kukipendelea chama tawala NRM.

Taswira waliyonayo baadhi ya wapigakura na wanasiasa wa upinzani kwa ujumla ni kutokuwa na imani juu ya mwenendo wa Tume kusimamia uchaguzi ulio huru na haki.

Kuelekea uchaguzi wa mwaka 2016 asilimia 89 za kura za maoni zilitaka mabadiliko katika Tume na michakato ya uchaguzi mkuu. Badala ya kufanyika mabadiliko hayo mamlaka zinazohusika zilibadilisha nafasi ya mwenyekiti kutoka Badru Kiggundu hadi Jaji Simon Byabakama.

Udanganyifu wa majina ya wapigakura na vituo vya kupigia kura na uhesabuji wake. Hali hiyo imetajwa kuwa ni udhaifu mkubwa kwa sababu unaruhusu mianya ya kuingizwa kura kutoka maeneo yasiyojulikana.

Kuvunja taratibu na sheria za uchaguzi. Mwaka 2001, Kizza Besigye alishindwa kufurukuta katika Mahakama ya Rufani baada ya jaribio la kupinga ushindi wa Yoweri Museveni kukwama. Katika kesi hiyo ilielezwa Mahakamani hapo juu ya ukiukwaji wa sheria,taratibu na kanuni hali ambayo iliiweka Tume katika taswira hasi.

Mwaka 2006 na 2011 kesi nyingine ya kupinga ushindi wa Museveni ilifunguliwa, licha ya Mahakama kukiri dosari za taratibu za uchaguzi, lakini haikufuta matokeo. Huo ulikuwa ushahidi wa udhaifu wa Tume kwa kuvunja Katiba ya nchi hiyo.

Msuguano wa mwaka 2016 ndani ya mhimili wa Mahakama unatajwa kuwa huenda ukawa chachu ya kufanya uamuzi wa kupingwa matokeo ya uchaguzi mwaka huu ikiwa utatokea na kuwataka Majaji kusimamia sheria kwani katika chaguzi zote kesi zinapofunguliwa kumeibuliwa hoja nzito juu ya udhaifu wa Tume ya Uchaguzi.

Tume hiyo imekuwa ikisisitiza kuwa uchaguzi huu utafanyika kisayansi na kwamba wagombea wanatakiwa kutumia vyombo vya habari kuwasiliana na wapigakura wao.

Hoja hiyo imetajwa kuwa dhaifu na Tume haikuzingatia ukweli kwamba wagombea wa vyama vya upinzani na wale wa kujitegemea wamekumbana na wakati mgumu kutumia vyombo vya habari hivyo kuwakosa wapigakura wao wanaoishi maeneo ya vijijini.

Duru za kisiasa zimetaja uamuzi huo kuwa ni chanzo cha kuwabana wagombea upinzani na kuonesha udhaifu wa Tume hiyo katika kusimamia haki zao.

Kushindwa kukemea unyanyasaji unaofanywa na vyombo vya dola dhidi ya wagombea wa upinzani. Unyanyasaji,kukamatwa na kuwekwa rumande ni miongoni mwa mambo yanayofanyika huku Tume ikiwa kimya.

Wapinzani kuzuiwa na vyombo vya dola kufanya mikutano ya kampeni kutokana na kuwekewa vizuizi vya polisi kwenye miji mbalimbali. Upande wa chama cha NRM hakijakumbana na mkono wa vyombo vya dola ambavyo vimekuwa vikiminya usawa katika kampeni za uchaguzi.

Tume imeshindwa kukemea vitendo vya Jeshi la Polisi kumsweka rumande mgombea wa chama cha National Unity Platform Robert Kyagulanyi 'Bobi Wine' na wafuasi wake.

Licha ya kutokea maafa hivi karibuni taarifa za vyombo vya habari viliripoti kuwa takribani watu 50 walifariki dunia wakati wa kukamatwa mwanasiasa huyo Tume imeendeleza ukimya.

Ni changamoto zipi zinazoikabili Tume hiyo?

Mlipuko wa ugonjwa wa corona umesababisha kubadilishwa kwa taratibu za mikutano ya kampeni za uchaguzi mkuu. Mathalani tarehe 26 Desemba mwaka 2020 Tume ya uchaguzi ililazimika kufuta ratiba za mikutano ya kampeni za uchaguzi kwa wagombea katika miji ya Mbarara, Kabarole, Luwero, Kasese, Masaka, Wakiso, Jinja, Kalungu, Kazo, Kampala na Tororo.

Hatua hiyo ilikuja baada ya Wizara ya Afya na Tume ya uchaguzi kukubaliana kuwa njia pekee ya kukabiliana na maambukizo ya corona ni kudhibiti mikusanyiko na kufuta maelekezo ya awali kuwa wafuasi wanaohudhuria mikutano wasizidi 200.

Tume hiyo imekuwa ikikabiliwa na ukata kutokana na bajeti hafifu. Bajeti ya Tume inapitishwa na Bunge, lakini kutokana na hali mbaya ya kifedha imekumbana na nakisi ambayo inaipa changamoto kutekeleza majukumu yake.

Huduma hafifu za intaneti. Tume inalaumiwa kuweka utaratibu wa kisayansi ambao unaingilia uteuzi wa ndani wa wanasiasa wa vyama.

Mpango wa 'uchaguzi wa kisayansi' wenye maana ya kutumia intaneti kupitia huduma ya Zoom kuchagua viongozi katika majimbo utakabiliwa na matatizo ya mawasiliano ya intaneti, miundombinu na umasikini hivyo ni dhahiri ni jambo lisilowezekana.

Tume imesema uchaguzi kupitia Zoom unalenga kupunguza maambukizi ya corona. Hata hivyo wagombea na wanasiasa wa upinzani wanasema Tume hiyo inaweza kujifunza kupitia uchaguzi wa Malawi ambako maambukizi ni makubwa kuliko Uganda lakini walifanya uchaguzi wa marudio kwa njia ya kawaida, pia chaguzi za Burundi, Mali, Korea, Tanzania, Marekani na Ghana.

Mpango huo umefikishwa Mahakama Kuu baada ya raia mmoja Joseph Kabuleta kufungua kesi kwa hoja kuwa unakiuka demokrasia. Mlalamikaji huyo anataka mpango wa Zoom ufutwe kwa vile haujashirikisha vyama vya siasa na kinyume cha sheria ya Bunge, Rais na inayounda Tume kwa vile unazuia haki na uhuru wa kujieleza wa wapigakura.

Je, uchaguzi huu una maana gani kwa Tume hiyo?

Miaka 14 na kusimamia chaguzi tatu ni kipindi kirefu kwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi. Muundo wao ni ule wa muhula wa miaka 7, ambapo kwa ujumla wa mihula yote amesimamia chaguzi tatu za mwaka 2006,2011 na 2016.

Matokeo aliyotangaza katika chaguzi zote tatu alizosimamia yalitajwa mbele ya Mahakama kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa sheria, taratibu na kanuni za uchaguzi.

Hii ina maana uenyekiti wake ulifuga taswira mbaya ambayo ilielezwa mahakamani lakini mara zote hakujiuzulu wala mamlaka za uteuzi hazikumwondoa. Hilo peke yake linaonesha taswira ya Tume hiyo kulinda maslahi ya chama tawala NRM.

Kwa mantiki hiyo Mwenyekiti mpya Jaji Byabakama anatakiwa kuonesha tofauti na aliyepita ili kuwapa imani wananchi wa Uganda na wanasiasa wa vyama vya upinzani.

Pia utaonesha uhuru wa Tume na kuthibitisha haipokei maelekezo kutoka taasisi yoyote.