Matokeo ya uchaguzi Tanzania 2020: Nini maana ya ushindi wa CCM kwenye ngome za upinzani?

- Author, Ezekiel Kamwaga
- Nafasi, Mchambuzi
- Iliyochapishwa
Habari kubwa ya kwanza ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania ilikuwa inahusu jimbo la Hai, mkoani Kilimanjaro, ambapo mbunge wake, Freeman Mbowe, alitangazwa kuangushwa na mgombea wa CCM, Saasisha Mafue.
Mbowe si mwanasiasa wa kawaida. Kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita, alikuwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na kwa maana hiyo Waziri Mkuu Kivuli.
Mbowe ni Mwenyekiti wa Chadema kwa takribani muongo mmoja na nusu na ndiye aliyekiongoza chama hicho kutoka kuwa cha tatu hadi chama kikuu cha upinzani bungeni.
Yeye ndiye aliyekibadilisha chama hicho kutoka kuwa cha kada la wahafidhina wenye mrengo wa kulia na kukifanya chama pendwa cha wasomi, vijana na watu was daraja la kati.
Vijana wengi mashuhuri wanaotamba katika siasa za Tanzania sasa wamepita katika mikono yake; iwe Zitto Kabwe, John Mnyika, Halima Mdee, John Mrema na wengine wengi.
Siku chache kabla ya uchaguzi, alihojiwa na vyombo vya habari na akasema anataraji kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania baada ya uchaguzi wa mwaka huu.
Matokeo hayo yamewaacha kinywa wazi wachambuzi wengi wa Tanzania. Mmoja wa wachambuzi maarufu wa siasa za Tanzania, Absalom Kibanda, alizungumza katika kituo kimoja cha televisheni nchini Tanzania kwamba jambo hili linahitaji tafakuri nzito kulielewa vizuri. Uso wake ulioneshwa kushtushwa na habari hizo - kama ilivyokuwa kwa wengi wengine.
Katika mazungumzo yangu na baadhi ya viongozi wa juu wa vyama vya upinzani wiki chache kabla ya uchaguzi, wengi walionesha matumaini makubwa na uchaguzi wa mwaka huu.

Nini kimetokea?
Hili ni swali ambalo litaendelea kujadiliwa ndani ya vyama na katika jamii pana katika kipindi cha siku, wiki na hata miaka kutoka sasa.
Ukweli ni kwamba, hakuna aliyeona matokeo haya yakitokea. Aliyekuwa mgombea Urais kupitia Chadema katika uchaguzi huu, Tundu Lissu, alikuwa akipata washabiki wa kutosha kwenye mikutano yake na katika siku za mwisho za kampeni alidai kwamba utafiti wa ndani wa chama chake ulionyesha kwamba kitapata ushindi wa kati ya asilimia 65 hadi 75.
Kama matokeo yataendelea kutoka katika namna inayoendelea sasa, kuna uwezekano wa CCM kupata ushindi mkubwa zaidi ya ule wa kihistoria alioupata Rais Jakaya Kikwete mwaka 2005 ambako alipata zaidi ya asilimia 80 ya kura zote zilizopigwa.
Matokeo ya namna hii; yakifuata uchaguzi wa mwaka 2015 ambako Chadema ilipata karibu asilimia 40 ya kura zote, yanaweza kuwa na maana mbili tu; ukiukwaji mkubwa wa taratibu za uchaguzi au wananchi kupoteza imani na vyama vya upinzani.

Chadema imelalamikia uchaguzi huu na kusema kuwa kulikuwa na matukio ya 'kupenyeza masanduku ya kura feki', madai ambayo Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ,Semistocles Kaijage amesema hayajafika rasmi kwenye tume ya uchaguzi.

Tanzania haina tume huru ya uchaguzi. Tanzania, kama zilivyo nchi nyingi za Afrika, ina mfumo unaompa faida kubwa Rais aliye madarakani - kama ilivyokuwa kwa mgombea wa CCM, Rais John Magufuli.
Vyama vya upinzani havikuwa vikishinda kirahisi huko nyuma. Mara zote wagombea wake walikuwa wakishinda katika mazingira magumu kutokana na mifumo na taratibu za uchaguzi za Tanzania; hata katika miaka ya nyuma.
Inavyoonekana, na hili ni jambo ambalo pengine taarifa zake zitakuja kujulikana baadaye, kuna kitu ambacho kimefanyika katika uchaguzi ambacho vyama vya upinzani havikuwa kimejiandaa nacho.
Ingawa kuna maeneo kama Zanzibar ambapo watu wamedaiwa kupoteza maisha kwa sababu ya uchaguzi huu, maeneo mengi nchini hayakuwa na vurugu wala mauaji.
Kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) hiihii na kwa sheria zilizopo, vyama vya Chadema na ACT Wazalendo bado vilikuwa na imani kwamba vitafanya vizuri.
Kuna kitu kimefanyika mwaka huu ambacho vyama vya upinzani havikuwa vimejiandaa nacho. Tafakuri za wanazuoni wa siasa, wadadisi na wanasiasa zitakuja kuliweka jambo hili bayana.
Nini athari ya kupoteza majimbo hayo?

Jambo la kwanza ni pigo la kisaikolojia kwa wafuasi wa vyama vya upinzani. Kama ingekuwa vitani, kilichotokea ni sawa na adui kwenda kupiga ngome yenye silaha zote.
Jambo hilo linaweza kushusha morali na linaweza kufanya watu wapoteze imani na mfumo wa demokrasia ya kupiga kura.
Chadema na upinzani kwa ujumla wana kazi kubwa ya kunyanyua morali ya wanachama na wapenzi wake baada ya uchaguzi huu.
Jambo la pili linahusu suala zima la mapato ya ruzuku. Mikoa yenye wapiga kura wengi hapa nchini ni Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya na Arusha. Ushindi wa CCM katika mikoa hii unamaanisha kwamba Chadema inaweza kupata kura chache majimboni na kupata fedha chache za ruzuku.
Baada ya uchaguzi uliopita, Chadema ilikuwa inapata zaidi ya shilingi milioni 300 kama ruzuku. Kama kuna jambo la mwisho ambalo Chadema inalihitaji kwa sasa ni kupungua kwa fedha za ruzuku.
Chadema kimekua sana na kinahitaji fedha kujiendesha. Bila mamilioni haya ya ruzuku, kinaweza kujikuta katika wakati mgumu.
ACT Wazalendo ilikuwa na matarajio kuwa mafanikio katika uchaguzi huu yatakiwezesha kupata ruzuku ambayo ingekifanya kikue zaidi. Kwa uchaguzi huu, ndoto hizo huenda zisitimie.














