Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Matokeo ya uchaguzi Tanzania 2020: Wafahamu wagombea waliopita bila kupingwa
- Author, Asha Juma
- Nafasi, BBC Swahili
- Iliyochapishwa
Matokeo ya uchaguzi yanapoendelea kutolewa nchini Tanzania katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 28, 2020 kuna baadhi ya wagombea waliopita bila kupigwa.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania, ilitoa taarifa siku za nyuma kwa umma kuhusu kuteuliwa kwa wagombea pekee wa ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Wagombea hao ni kutoka majimbo 18 kati ya majimbo 264 ambayo wagombea walikuwa wameingia kwenye kinyang'anyiro.
Job Ndugai
Job Ndugai kutoka jimbo la Kongwa. Bwana Ndugai alikuwa spika wa Bunge la 11 la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.
Bwana Ndugai alikuwa Spika wa 7 wa Bunge la Tanzania tangu uhuru.
Profesa Palamagamba
Profesa Palamagamba wa CCM katika jimbo a Kilosa alikuwa waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania katika serikali ya iliyopita.
Kabla ya uteuzi huo Profesa Kabudi alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria.
Dkt. Hamisi Kigwangalla
Dkt. Hamisi Kigwangalla amepita bila kupingwa kupitia chama cha Nzega mjini na mara ya kwanza anaingia Bunge alikuwa miongoni mwa wanasiasa vijana akiwakilisha Nzega eneo la Tabora.
Pia aliwahi kukamatwa na maafisa wa uhamiaji kwa mdai kwamba sio raia wa Tanzania na hilo likawa gumzo kwenye vyombo vya habari Tanzania. Dkt. Kigwangalla alichaguliwa tena mwaka 2015.
January Makamba
Mwingine ni January Makamba wa Bumbuli aliyekua Waziri ofisi ya makamu wa rais ambaye aligombea tena Ubunge katika jimbo la Bumbuli -Tanga katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Kuna wakati Januari Makamba alidaiwa kuwa miongoni mwa viongozi ambao sauti zao zilisikika mitandaoni zikimzungumzia vibaya rais Magufuli.
Lakini Rais Magufuli akakiri kumsamehe.
Kassim Majaliwa
Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa. Alikuwa mbunge wa jimbo la Ruangwa tangu mwaka 2010 akigombea kwa CCM.
Tarehe 19 Novemba 2015 Bwana Majaliwa aliteuliwa na rais John Magufuli kuwa waziri mkuu wa serikali ya awamu ya tano nchini Tanzania.
Aliwahi kushika vyeo vya naibu waziri wa utawala wa mikoa na serikali ya mitaa katika ofisi ya waziri mkuu tangu mwaka 2010 na mkuu wa mkoa wa Lindi kuanzia 2006 hadi 2010.
Bwana majaaliwa ni mpenzi wa michezo ya klabu za Tanzania na ni shabiki wa Simba S.C.
Wengine waliopita moja kwa moja ni pamoja na:
- Mhandisi Isaack Kamwelwe wa Mlele
- Elias Kwandikwa Jimbo la Ushetu,
- Philipo Augustino Mulugo wa Songwe
- Zedi Jumanne wa Bukene
- Ahmed Shabiby jimbo la Gairo
- Palamagamba Kabudi wa Kilosa
- Jonas Van Zeela wa Mvomero
- Nape Nnauye wa Mtama
- Kalogereris Innocent wa Morogoro Kusini
- Vita Rashid Mfaume Kawawa wa jimbo la Namtumbo
- Taletale Hamis Shabani wa Morogoro Mashariki
- Sagini Abdallah wa Butiama
- Alexander Mnyeti jimbo la Misungwi
- Geofrey Pinda wa Kavuu