Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Marekani, India zasaini mkataba wa kushirikishana taarifa muhimu
India na Marekani zimesaini mkataba wa kijeshi unaohusu ushirikishanaji wa taarifa za siri huku kukiwa na mzozo wa mpaka kati ya serikali za Delhi na Beijing.
Kuweza kuzipata data hizo kunachukuliwa kama muhimu kwa ajili ya kuyaqpiga makombora , ndege zisizokuwa na rubani na kuyalenga maeneo.
Mkataba huo ulitangazwa baada ya mkutano wa mwaka wa "2+2" wa mazungumzo ya viongozi wa ngazi ya juu mjini Delhi Jumanne.
Wataalamu wanasema kuimarika kwa ushirikiano kati ya India na Marekani kunalenga kukabiliana na ushawishi wa China katika ukanda huo.
Waziri wa ulinzi wa Marekani Mark Esper alifanya mazungumzo na mwenzake wa India Rajnath Singh. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Mike Pompeo pia alikutana na waziri wa mambo ya nje wa India S Jaishankar.
"Katika kipindi cha miongo miwili, ushirikiano wetu umekua imara kwa vitendo, na kwa kwa kiwango cha umuhimu," Bw Jaishankar alisema Jumanne. Aliongeza kuwa mazungumzo yatawezesha nchi mbili kushirikiana kwa pamoja kwa mapana zaidi katika masuala ya usalama wa taifa ".
Makubaliano ya Mabadilishano ya kimsingi na Ushirikiano au BECA, ni miongoni mwa mikataba michache ambayo Marekani husaini na washirika wake wa karibu.
Yanairuhusu India kupata data au taarifa kwa kiwango cha zile za siri za anga za mbali na zile zinazohusiana na sayansi ya kutengeneza na kuendesha ndege, ambazo ni muhimu kwa hatua za kijeshi
Pande mbili pia zimesaini mikataba mingine kadhaa inayohusiana na nishati ya nuklia, sayansi ya dunia na tiba mbadala. Lakini BECA ndio mkataba muhimu zaidi miongoni mwake.
Unairuhusu Marekani "kutoa misaada ya vifaa vya majini na ya safari za anga katika ndege za Marekani zilizotolewa kwa India ", chanzo cha kijeshi cha India kililiambia Shirika la habari la Reuters - kwamba pia inamaanisha Marekani inaweza kuweka vifaa vyake vya manuwari za kijeshi katika ndege ilizozitoa kwa India
Umuhimu wake unakuja wakati India ikiwa imefungwa katika moja ya mzozo mkubwa zaidi kati yake na China unaohusu jimbo la Himalaya.
Wanajeshi ishirini wa India walikufa katika makabilianoambayo yalizuka kati ya wanajeshi wa pande mbili mwezi Juni, na hivyo kusababisha kuanza kwa mazungumzo ya kidiplomasia ya miezi kadhaa ili kutuliza uhasama baina ya pande mbili. Lakini hilo halijasaidia kuonda uhasama huo hadi sasa.
Mahusiano kati ya Marekani na China pia yalizorota katika miezi ya hivi karibuni kuhfuatia ukosoaji wa mara kwa mara wa Rais Trump kuhusu jinsi China ilivyoshughulikia janga la virusi vya corona.
Marekani pia iliikemea China kwa kuweka sheria mpya katika Hong Kong, kufuatia maandamano makubwa ya kuipinga sheria hiyo.
Mkataba huo ni hatua nyingine ya kuimarisha urafiki wa kijeshi kati ya India na Marerkani. India ni mojawapo ya wanunuzi wakubwa wa vifaa vya kijeshi, lakini karibu 60-70% ya silaha zake huagizwa kutoka Urusi.
Marekani inataka kubadili hili na imekuwa moja ya wauzaji wakuu wa bidhaa za kijeshi kwa India katika miaka ya hivi karibuni. Hayo yamedhihirishwa katika kauli zilizotolewa na viongozi wa mataihfa hayo mawili.
Ziara itaimarisha nia ya India na Marekani ya "kujitolea kuimarisha ushirikiano wa jeshi kwa jeshi ," taarifa rasmi ilisema baada ya Bw Esper kukutana na Bw Singh Jumatatu.
"Mazungumzo yetu leo yalikuwa yenye kuzaa matunda, yalilenga kuimarisha ushirikiano wa karibu katika maeneo mapana zaidi ," Bw Singh alitweet baadae.
Hii ni awamu ya tatu ya mazungumzo ya "two-plus-two" ya mwaka kati ya India na Marekani.
Yakwanza yalifanyika mjini Delhi mwaka 2018. Mazungumzo ya hivi karibuni, awali yalipangwa kufanyika mapema mwaka huu, lakini yalicheleweshwa kutokana na janga la corona na yanafanyika wiki moja tu kabla ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Marekani . Wachambuzi wanasema kuwa muda ambao mazungumzo haya yamefanyika ni muhimu na yanaionesha India kuwa kipaumbele kwa Marekani.