Uchaguzi Tanzania 2020: Uchumi wa Tanzania unaimarika kwa kiasi gani?

Chanzo cha picha, EPA
- Author, Peter Mwai
- Nafasi, BBC Reality Check
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Rais wa Awamu ya Tano nchini Tanzania Dkt John Magufuli amekuwa akitaja ukuaji wa uchumi wa taifa hilo kama moja ya ufanisi wa utawala wake.
Ameahidi kuimarisha uchumi wa taifa hilo hata zaidi, ambapo Chama cha Mapinduzi kwenye ilani yake kimeahidi kukuza uchumi kwa wastani wa asilimia nane.
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe
Upinzani hata hivyo umekuwa ukiikosoa serikali na kusema kwamba ukuaji wa uchumi haujawafikia wananchi wa kawaida.
"Ukuaji wa uchumi wa Tanzania haujaambatana na kasi kubwa ya kupungua kwa watu masikini," kinasema Chama cha Wananchi (CUF) kwenye ilani yake.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo nacho kimekuwa kikisema uchumi haujakuwa sawa kwa miaka mitano iliyopita.
"Watu ambao wamefunga biashara katika hii miaka mitano ni wengi kuliko watu waliofungua biashara. Uwekezaji umepungua kwa nusu, zaidi ya asilimia 50 ya uwekezaji katika miaka mitano hii wameondoka," amesema mgombea urais wa Chadema Tundu Lissu.
"Watanzania wanajua kabisa kwamba hii miaka mitano imekuwa miaka ya njaa kweli kweli."
Je, hali halisi ya uchumi wa Tanzania ni gani?
Ukuaji wa uchumi umekuwaje?
Tanzania imeandikisha kiwango cha ukuaji wa uchumi cha juu kwa mwongo mmoja uliopita, ambapo kiwango cha ukuaji kimekuwa kwa wastani kati ya asilimia 6 hadi 7.
Kwa miaka mitano ya utawala wa Rais Magufuli, ukuaji wa uchumi kwa wastani umekuwa asilimia 6.5.
"Uchumi umekuwa unakwenda vizuri, na vilevile umekuwa jumuishi. Kumekuwa na uwekezaji katika sekta zinazowagusa watu wengi," anasema Prof Humphrey Moshi, mchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Kiwango cha ukuaji wa uchumi wa Tanzania kimekuwa cha juu ukilinganisha na baadhi ya mataifa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kipindi cha serikali ya Awamu ya Tano.
Ukuaji mwaka 2015 - mwaka wa mwisho wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete ulikuwa asilimia 6. Kasi ya ukuaji iliongezeka na kuwa asilimia 7 miaka miwili ya kwanza kamilifu chini ya Rais Magufuli.
Kasi ya ukuaji ilipungua na kuwa asilimia 5 mwaka 2018 lakini ikapanda tena mwaka 2019 na kuwa asilimia 6.
Mwaka 2019, kiwango cha ukuaji wa uchumi wa Tanzania kilikuwa cha tatu EAC baada ya Rwanda (9%) na Uganda (7%).
Ukilinganisha na awamu ya nne, mwaka wa ufanisi mkubwa katika miaka yote 14 ulikuwa ni mwaka 2011 uchumi ulipoimarika kwa asilimia 7.6.
Lakini mwaka uliofuata, mwaka 2012, ndio pia ulioshuhudia ukuaji wa chini zaidi wa uchumi katika kipindi hicho (4.5%).
Prof Moshi anasema ukuaji wa uchumi umetokana na uwekezaji uliofanywa na serikali kwenye sekta nyingi na kufaidi taifa kwa njia nyingi.
"Kwenye miundo mbinu kwa mfano, kumekuwa na uwekezaji kwenye uchukuzi wa majini, nchi kavu na angani," aliambia BBC.
"Uwekezaji huu unaisaidia serikali kufaidi zaidi kutokana na maliasili na rasilimali zake."
Anasema faida zaidi zitajidhihirisha baadhi ya miradi itakapokamilishwa.
Kwa mujibu wa Prof Moshi, uongozi pia umechangia akitaja mfano wa sekta ya madini na umeme ambapo anasema kurekebishwa kwa mikataba kumeongezea serikali mapato.
Taifa la uchumi wa kati?
Tanzania iliorodheshwa na Benki ya Dunia kuwa taifa lenye uchumi wa kati mnamo 1 Julai mwaka huu.
Rais Magufuli alisema hatua hiyo ilikuwa ni "ushindi mkubwa na kazi kubwa tumeifanya."
Lengo chini ya Dira ya Maendeleo ya Taifa (TDV) ya 2025 lilikuwa kufika katika kiwango hicho kufikia mwaka 2025, kwa hivyo hilo lilitokea miaka mitano mapema.

Chanzo cha picha, Reuters
Lakini nini kilitokea hasa na maana yake ni nini?
Benki ya Dunia huyaorodhesha mataifa katika viwango vinne kwa kuzingatia mapato ya taifa - pato la chini, la kati la chini, la kati la juu na mataifa ya pato la juu.
Hili hufanyika kila mwaka 1 Julai kwa kuzingatia pato ghafi la taifa (GNI) kwa kutumia thamani ya dola ya Marekani ya mwaka uliotangulia na pia kwa kuzingatia mfumko wa bei.
Kipimo cha GNI cha Tanzania kwa kila mtu kiliongezeka kutoka $1,020 mwaka 2018 hadi $1,080 mwaka 2019 uliokuwa unatumiwa kuorodhesha mataifa.
Kiwango cha mataifa ya pato la kati la chini kilianzia $1,036, hivyo Tanzania ikawa kwenye kundi hilo.
Bw William Battaile, mchumi mkuu katika Benki ya Dunia anayeangazia Tanzania, Malawi, Zambia na Zimbabwe, anasema ni sahihi kutazama kuorodheshwa kwa taifa hilo kama taifa la uchumi wa kati.
Hata hivyo, anasema yapo mambo mengine yanayofaa kufanyika kutimiza malengo yaliyopo kwenye TDV ya 2020. Anasema dira hiyo ni pana.
"Inaitazamia Tanzania kama nchi ya pato la chini yenye viwango vya juu vya maisha; amani, uthabiti, na umoja; utawala bora; jamii iliyoelimika vyema na inayosoma; na uchumi wenye ushindani unaowezesha maendeleo endelevu na faida jumuishi," anasema.
"Kwa hivyo ongezeko la GNI halitoshi. Kuwekeza katika ustawi wa watu na miundo mbinu ni muhimu katika kutimiza malengo haya pana na kuboresha maisha kwa Watanzania wote."
Prof Moshi anakubali kwamba kutimizwa kwa lengo hilo ni hatua moja tu, na anailinganisha na safari.
"Ni kama kuvuka mpaka, na kazi kubwa lazima ifanyike. Ni lazima tuendelee kuimarisha uchumi na kuhakikisha kilimo kinakuwa na tija na uchumi uwe jumuishi," anasema.
Je, umaskini umepungua?
Benki ya Dunia inasema ingawa kiwango cha umaskini nchini humo kimepungua, idadi ya watu ambao ni maskini haijapungua.
Hili kwa kiwango fulani limechangiwa na ongezeko la idadi ya watu nchini humo. Lakini pia kasi ya ukuaji wa uchumi haijaambatana na kasi ya kupungua kwa umaskini.
Katika miaka ya karibuni, ukuaji wa uchumi pia haujakuwa na matokeo makubwa sana katika kupunguza idadi ya watu maskini.
Kati ya 2007-12 ukuaji wa 10% katika Pato Ghafi la Taifa kwa mtu binafsi ulichangia kupungua kwa 10% kwa kiwango cha watu maskini. Lakini 2012-18, kiwango sawa na hicho kilichangia kupungua kwa umaskini kwa 4.5%.
Kwa mujibu wa benki hiyo, karibu nusu ya watanzania huishi chini ya kipimo cha umaskini cha kimataifa cha dola za Marekani 1.90 kwa siku.
Kiwango hicho hakijabadilika sana kati ya 2012 na 2018.

Kwa kutumia kipimo cha umaskini cha taifa (dola 1.35 kwa siku), maskini walipungua kutoka asilimia 28.2 mwaka 2012 hadi asilimia 26.4 mwaka 2018, tofauti ya asilimia 1.8.
Lakini kiwango hicho kilipungua kwa kiwango kidogo ukilinganisha na kushuka kwa asilimia 6.7 kati ya 2007 na 2012.
"Kupungua kwa kasi ya kupungua kwa watu maskini, ukiongeza na ukuaji wa idadi ya watu, vilisababisha ongezeko la watu maskini 1.7 milioni kati ya mwaka 2012 na 2018," Benki ya Dunia inasema.
"Hii inaashiria kuwa ukuaji wa uchumi umekuwa hauwajumuishi watu wengi na hauwafai maskini. Ukuaji umekuwa kwenye sekta ambazo maskini wengi hawafanyi kazi. Sana imekuwa ni Watanzania tajiri, wenye elimu na mali, ambao wamenufaika kutokana na ukuaji."
Bi Bella Bird, mkurugenzi wa Benki ya Dunia aliyesimamia Tanzania, Malawi, Zambia na Zimbabwe, anasema juhudi za serikali za kuboresha hali ya maisha zimechangia kuongeza upatikanaji wa huduma za msingi na kuimarika kwa Watanzania kielimu na katika ujuzi.
Hilo limesaidia kupunguza umaskini.
"Kuendelea kupunguzwa kwa umaskini ni habari jema lakini ni muhimu kwa Tanzania kuongeza kasi ya kupunguza kwa umaskini kwani idadi ya maskini bado ingali juu," alisema, baada ya kutolewa kwa ripoti kuhusu umaskini Tanzania Desemba mwaka jana.
Benki ya Dunia wakati huo ilikadiria kwamba walikuwepo watu maskini 14 milioni nchini Tanzania. Idadi hiyo ilikuwa imeongezeka kutoka watu 13 milioni mwaka 2007.
Wapo pia watu wengi walio kwenye hatari ya kutumbukia kwenye umaskini kwani kwa kuzingatia vigezo vya kimataifa, ambapo maskini hutazamwa kuwa mtu anayeishi kwa chini ya $1.90 kwa siku, karibu nusu ya Watanzania wamo kwenye kiwango hicho.
Prof Moshi anasema ndipo Tanzania ifanikiwe kupunguza tatizo la umaskini, ni lazima uchumi ukue kwa kiwango cha juu kuliko ongezeko la watu.

Chanzo cha picha, EPA
Aidha, utegemezi wa sekta isiyo rasmi upunguzwe na watu wengi wawe wameajiriwa kwenye sekta zenye tija.
"Wakati uchumi unakua, ni lazima kiwango cha ukuaji kiwe kikubwa kuliko ukuaji wa watu. Kwa Tanzania, ukuaji wa uchumi unafaa kuwa asilimia 8 na kwenda juu, na ukuaji huo uwe endelevu," aliambia BBC.
Anasema Tanzania ni lazima iendelee kuongeza viwanda na kilimo kifanywe kuwa cha kisasa umwagiliaji maji na chenye tija.
Kwa sasa sekta ya viwanda huchangia asilimia 9 hadi 12% ya uchumi wa Tanzania lakini ili kufaidi, mchumi huyo anasema kiwango hicho kinafaa kuwa kati ya asilimia 15 hadi 20.
Wanaotegemea kilimo wanafaa pia kupungua kutoka asilimia 60 kwa sasa hadi asilimia 20.
"Ukiwa na viwanda, watu watapata nafasi za ajira na wakulima watapata soko la kuuza mazao yao. Kilimo kitaimarika na wakulima watapata faida zaidi na kuweza kununua bidhaa zinazozalishwa viwandani," anasema.












