Je wazazi Kenya wamejiandaa vipi iwapo shule zitafunguliwa?

Wanafunzi
    • Author, Faith Sudi
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Iliyochapishwa

Ni miezi saba sasa tangu kuanza kwa mlipuko wa janga la corona na kusababisha shule zote kufungwa nchini Kenya na kote duniani.

Hatua hii ya kufunga shule pamoja na vyuo vyote ilikuwa ni njia ya kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo.

Japo awali serikali ilitangaza kwamba shule zitafunguliwa tena mwezi Januari mwaka ujao wa 2021, hili sasa linaelekea kubadilika baada ya wizara ya afya kutangaza kwamba idadi ya maambukizi pamoja na vifo vitokanavyo na Covid-19 inaendelea kupungua.

Juma lililopipta waziri wa elimu Profesa George Magoha aliamuru walimu wote kurejea shuleni Jumatatu terehe 28 Septemba tangazo ambalo limeibua mjadala mkali kati ya washikadau na wazazi.

Katika kipindi chote ambacho wanafunzi wamekuwa majumbani kumetokea changamoto kadhaa kama vile mimba za mapema.

Changamoto nyingine ni wamilki na walimu wa shule za binafsi kupoteza ajira na huku wengi kama vile walimu na wanafunzi waliokuwa wakisubiri mitihani yao ya mwisho wa mwaka wakiachwa bila kujua la kufanya.

Huenda sababu hizi zimechangia wizara ya elimu kuchukua hatua ya kuanza mkakati wa kufungua tena shule, lakini je wazazi wako tayari kwa hili?

Brenda Wekulo ni mzazi na mwalimu kutoka kaunti ya Bungoma.

Ni muhimu watoto kurudi shuleni lakini serikali ihakikishe kila kitu kiko sawa….Wasiangalie tu madawati, wazingatie pia usalama wa watoto, kule watakapocheza watakapokutana nje ya madarasa na uwiano wa walimu kwa wanafunzi ukoje… kwa sababu tukiangalia tu madarasa, hatutakuwa tumekabiliana na shida hiyo".

Kulingana na mwenyekiti wa muungano wa wazazi, Nicholas Maiyo, wazazi wako tayari shule zifunguliwe lakini wao wanataka mambo fulani kwanza yazingatiwe.

"Oktoba tumesema shule zinaweza kufunguliwa iwapo masharti ambayo yanatakiwa kuwekwa kwenye mazingara ya shule yapo kama vile kuweka tenki la kunawa mikono, barakoa za wanafunzi wetu…" Gharama ambayo itakuwa ya wazazi ni barakoa pekee, lakini gharama ya maji na nafasi ya mita mbili kati ya wanafunzi ni gharama ya shule"

Ni changamoto gani zilizopo ikiwa shule zitafunguliwa mapema?

Profesa George Magoha

Chanzo cha picha, Wizara ya Elimu Kenya

Maelezo ya picha, Waziri wa Elimu wa Kenya Profesa George Magoha

Aidha kuna wake watakaoathirika ikiwa shule zitafunguliwa mapema tofauti na ilivyotangazwa awali.

Jamii ya Waluhya kutoka Magharibi mwa Kenya na ile ya Wakalenjin kutoka bonde la ufa kwa msimu huu wako katika shughuli za kuwapeleka watoto jandoni.

Kutokana na tangazo la serikali la awali ambalo lilitoa pendekezo la uwezekano wa shule kufunguliwa mapema mwaka wa 2021, wazazi wengi kutoa jamii hizi walichukua hatua ya kuwapeleka watoto wao jandoni.

Kwa kawaida jamii hizi hufanya shughuli mwezi wa Agosti na Desemba, lakini kutokana na tangazo hilo la awali, kumekuwa na mabadiliko.

Joshua Kenor ni mzazi kutoka mjini Turbo katika kaunti ya Uasin-Gishu. Alikuwa amepanga kuwapeleka watoto wake jandoni msimu huu.

"Kwa kawaida, katika jamii ninayotoka, msimu ambao huwa tunawapeleka watoto jandoni huwa mfupi, lakini mwaka huu tulikuwa tumejipanga kutokana na tangazo la serikali awali la shule kufunguliwa mwaka 2021. Ila kutokana na hili tangazo la juzi, mipamgilo yote imeharibika… Na sio tu kwa hilo, sare na viatu vya shule vimekuwa ndogo. Hii pia ni gharama nyingine.

Kuhusu masuala ya jandoni na mimba za mapema, mwenyekiti huyo anasema kwamba kisheria wanafunzi hao wanaruhusiwa kuenda shuleni wakiwa wajawazito.

"Tuko na changamoto kama wazazi, wazazi wengi waliwapeleka watoto wao jandoni wakijua kwamba shule zitafunguliwa Januari. Wasichana wetu wengine walitungwa mimba na vijana wenzao na sheria ya shule nchini Kenya inakubali msichana wangu akipata mimba, arudi shuleni asome akifika wakati wa kujifungua, ajifungue kisha arejee shuleni, hilo hapa nchini Kenya hatuna tatizo lolote"

"Kuhusu jandoni, tumeogea na wazazi na tukakubaliana kuandika pendekezo kwa wizara ya elimu ituruhusu… Wale watoto wetu wamalize jandoni kwa sababu wanaenda tu kwa mwezi mmoja, na si wengi ni kama wawili au watatu kwa darasa moja."

Iwapo shule zitafunguliwa inasadikiwa kuwa wazazi watakuwa na kibarua kigumu hasa wale ambao watoto wao wanasoma katika shule za binafsi.

Baadhi ya wamiliki wa shule hizo walibadilisha majengo hayo na kuweka biashara zingine kama vile ufugaji na aina nyingine ya kilimo .

Kuna wengine nao walilazimika kuuza majengo yao ambayo yalikuwa ni shule.

Peter Ndoro ni Afisa mkuu mtendaji wa muungano wa shule za kibinafsi.

" Tuliagiza shule hizo kuwaandikia wazazi barua na kuwaarifu kwamba wakati shule zitakapofunguliwa, shule hizo hazitakuwepo. Na tumewashauri wazazi kuwapeleka watoto wao katika shule zingine za kibinafsi ama zile za umma. Sisi kama shule za kibinafsi tumejipanga na kuongeza nafasi ambazo tunahitajika kuzingatia kulingana na masharti ya serikali na kubakisha zingine ambazo tutawapa wanafunzi ambao shule zao zilifungwa"

Wizara ya elimu imeamuru shule ambazo zilitumiwa kama sehemu za kuwatenga wagonjwa wa covid 19 kurejeshwa kwa wasimamizi wa shule ambao watasimamia unyunyizaji dawa kwa ajili ya matayarisho ya kurejea kwa wanafunzi.

Mpangilio uliopendekezwa na jopo-kazi lililoteuliwa na Wizara ya elimu inaaminika kuwa wanafunzi wa mwaka wa mwisho watatangulia kurejea shuleni, kisha wafuatwe na madarasa mingine.

Mwongozo kamili unatarajiwa kutolewa baadae hii leo na rais Uhuru Kenyatta atakapohutubia taifa wakati.

Ni tangazo ambalo linaweza kuvunja wengine moyo huku wengine wakiishia na furaha.